VITABU vitakatifu vinasema kila mwenye pumzi na amsifu Mungu. Nami sina budi kusema asante Mungu kwa uhai na afya njema ambayo ametujalia mimi na wewe msomaji wangu. Utafiti unaonesha kwamba, kumekuwa na mimba nyingi zisizotarajiwa katika jamii yetu huku waathirika wa mimba hizo wakiwa ni mabinti na wanawake wengi.
Lawama zao nyingi zimekuwa zikielekezwa kwa wanaume ambao waliwapa ujauzito na pengine kuwatelekeza. Lengo la mada hii ni kukuonya, kukusaidia na kukufundisha wewe msichana au mwanamke mwenye tabia ya kujibebesha mimba kwa makusudi, ukiamini ni kigezo tosha cha kuolewa hata kama hujakubaliana na mwanaume husika kuhusu kubeba mimba.
Tabia hiyo ya kujibebesha mimba imewafanya wanawake wengi kujikuta wakiangukia pua hasa baada ya kugundua kuwa mimba aliyobeba mhusika wake hashiriki kwa namna yoyote katika kumsaidia kulea na vitu vingine. Mbaya zaidi hata alipomwambia wala mshipa haukumcheza kisha akaingia mitini.
Hapa ninamaanisha kuwa, unaweza kujibebesha mimba kwa kuamini kuwa itakuwa rahisi au itamsukuma mpenzi au mchumba kukuoa lakini mwisho wa siku hakuna muoaji. Matokeo yake unaishia kulalalamika na kutapatapa kuwa umetelekezwa, umesalitiwa bila
kujikumbusha kuwa wewe ndiye uliyekuwa chanzo cha mimba isiyokuwa na makubaliano. Kufanya hivyo kuna mambo mawili ambayo yanaweza kujitokeza; Mosi unaweza kufanikiwa jambo lako kwa asilimia zote kama mwenza wako naye atakuwa kweli anakupenda na ana dhamira ya dhati ya kuzaa na wewe au kukuoa. Kwa upande mwingine, unaweza kufanya mchezo huo wa kujibebesha mimba lakini ukaishia kula za uso kwa jamaa kuuruka ujauzito wako. Hili nalo unapaswa uliweke akilini mwako ili kama likikutokea usimtafute mchawi.
Wasichana wengi wamekuwa wakifanya tabia hizo za kujibebesha mimba pengine kwa kumpa penzi mwenza wake wakati akifahamu fika kuwa yuko kwenye siku za uwezekano wa kupata mimba, lengo likiwa ni kushika ujauzito ili aolewe na mhusika. Wengine hufanya makusudi kushika mimba kwa sababu tu mpenzi wake anaamini ana maisha mazuri.
Kwa mwanamke mwenye tabia ya kufanya hivyo anakuwa na hatari kwani anaweza kujikuta akibeba mimba hovyo akitegemea kuolewa, kumbe aliyechepuka
naye ni mume wa mtu au hana nia ya kuwa na mtoto au kuoa. Nilichokibaini katika utafiti wangu wa kawaida ni kwamba mimba hizo zisizokuwa na makubaliano ya pande zote ndizo hasa husababisha wanawake kutelekezwa na wanaume waliowapa ujauzito.
Ndizo hasa huwafanya wanawake kunung’unika kwa kuona kuwa baadhi ya wanaume ni watu wabaya, wauaji na wanyama lakini anasahau ukweli kuwa yeye ndiye sababu ya kutelekezwa.
Yapo mambo mengi ya kujiridhisha kwanza kwa mwanaume ambaye unatamani kuzaa naye. Lazima ujue kama kweli yuko tayari kuzaa na wewe? Je, anaweza kumuhudumia mtoto?
Je, mwanaume unayetaka kuzaa naye hana mke au ana mke ili kila kitakachokutokea katika maisha yako ya mimba hiyo usiwe na lawama juu yake. Kuolewa na kupata ujauzito ni vitu viwili tofauti, ndoa ni makubalino na hata kupata ujauzito ni
suala la kukubaliana na mweza wako. Unaweza kubeba mimba, kumbe mwenza wako hayuko tayari kifedha, kiafya na mambo mengine.
Hivyo ni vyema kumshirikisha katika kila jambo. Unapojibebesha mimba ili uolewe, unaweza kuangukia pua kwa kujikuta ukiolewa na mtu ambaye hana mapenzi ya dhati na wewe na hata ndoa yako itashindwa kudumu kwa sababu tu mwanaume uliyemlengeshea hakuwa chaguo lako.
Kikubwa cha kujifunza hapa ni kwamba suala la kubeba mimba huwa ni makubalino baina ya wapenzi, lakini kama wewe mwanamke utaamua kufanya kusudi kupata mimba ukiamini kuwa utaolewa ni kujidanganya na kujisababishia ugumu wa maisha baada ya kupata ujauzito. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri na yenye mafunzo ndani yake.
Comments are closed.