The House of Favourite Newspapers

Hadithi ya Eric Shigongo: Dimbwi la Damu-06

ERIC SHIGONGO DIMBWI LA DAMU-05

ILIPOISHIA:

Dakika kumi tu baada ya kukaa kitini na kufungiwa mkanda ndege ilianza kuiacha ardhi ya Tanzania! Akiwa juu aliingalia Arusha na roho ilimuuma sana, picha ya mwisho aliyoagana na dada yake pamoja na Leah uwanjani ilimuumiza kupita kiasi alishindwa kuelewa ni kwanini Vicky alisisitiza kuwa safari yake ingekuwa na matatizo.
“Wasichana bwana anataka tukae tu kuangaliana wakati umasikini unatutesa! Litakalokuwepo mbele acha liwepo Mungu anajua!” Alisema Nicholaus huku ndege ikiondoka.

ENDELEA…

Safari kutoka Tanzania kwenda Iran kupitia Nairobi,Misri, Uturuki na Iraq iliwachukua masaa 16! Wakati Nicholaus anapanda ndege kwenye uwanja wa Kia moyo wake ulijaa furaha kwa sababu ilikuwa ni mara ya kwanza lakini kadri masaa yalivyozidi kwenda alizidi kuchoka na kuichukia safari hiyo.
Ndege ilipotua katika uwanja wa ndege wa Tehran majira ya saa kumi na moja alfariji na abiria wote walianza kushuka kwa kutumia ngazi! Wakati Nicholaus anachukua Sanduku lake alishutkia anaguswa begani, aligeuza uso wake na macho yake yalikutana na sura ya AbdulAziz! Alifurahi kumwona kwa sababu tangu Tanzania hawakuongea kitu chochote walipishana kama wasiofahamiana.
“Tumefika Nicholaus sasa sikiliza, sisi tunatoka na tutakusubiri nje ya uwanja wa ndani ya gari la aina ya BMW jeusi, lililokuja kutupokea sawa si unaifahamu BMW?”
“Ndiyo nilikuwa naziosha sana Arusha, si kama ile ya Frank Mshanga wa Arusha?”
‘Huyo mtu hatumjui ila wewe utatukuta nje mbele ya lango la kutoka sawa?”
“Sawa?”
“Beba vizuri hilo Sanduku lako lisiibiwe!”Alimaliza AbdulAziz na kuondoka.
Kazi yao ilikuwa karibu kufikia mwisho kipingamizi pekee kilichokuwa mbele yao ni uwanja wa ndege wa Tehran! Walijua kitendo cha kukamatwa kwa wauza madawa wengine saba wiki moja tu kabla ya kupigwa risasi kilikuwa kimefanya ulinzi katika uwanja wa ndege uimarishwe zaidi.
“Tukivuka hapa tayari tumetajirika!” Alisema Samwel.
“Lakini kwa ninavyoiona hali siyo rahisi kuvuka!” Walibadilishana mawazo Samwel na AbdulAziz wakati wakitoka nje ya uwanja!
Upekuzi waliofanyiwa siku hiyo haukuwa wa kawaida kulikuwa na mbwa kama kumi walionusa kila abiria aliyepita langoni kutoka nje na walifanya hivyo pia kwa kila mzigo uliotolewa uwanjani.
***

Askari waligundua madawa katika Sanduku la Nicholaus kabla halijateremshwa lakini hawakutaka kulichukua waliiacha lipelekwe sehemu ya kupokelea mizigo ili wamwone mwenye sanduku alikuwa nani!
Masanduku na mabegi yalizidi kupita katika sehemu iliyozungukwa na kila abiria alichukua begi au sanduku lake lilipopita mbele yake, makachero wa kitengo cha kupambana na madawa ya kulevya nchini Iran walimwagwa sehemu hiyo kushuhudia ni nani angelichukua sanduku lenye madawa.
Nicholaus alizidi kuangalia wakati mabegi na masunduku yakizidi kuzunguka mbele yake, kwa muda kama dakika tano hakuliona sanduku lake na kuanza kuingiwa hofu lakini ghafla aliliona na kufurahi kwani alikuwa na hamu kubwa ya kutoka nje ya uwanja alione jiji la Tehran lilivyokuwa!
Kwake kuingia katika nchi tofauti na Tanzania akiwa na umri mdogo kama wake yalikuwa mafanikio makubwa mno katika maisha. Lilipomfikia sanduku lake alilichukua na kuanza kutembea kwa haraka kuelekea nje ya uwanja! Kabla hajatoka alishtukia kundi la mbwa kama saba hivi likimvamia na kumwangusha chini na kuanza kumuuma kila mahali.
Nicholaus alilia kwa maumivu aliyoyapata, polisi walikuja na kumkamata wakaanza kumpiga na virungu kichwani huku wakimvuta kumpeleka sehemu asiyoijua.
“Samweeeel! AbdulAziz njooni mnisaidie!” Alipiga kelele Nicholaus lakini hakuna aliyemjali alizidi kuvutwa, waliposikia majina yao yakiitwa Samwel na AbdulAziz walimwamuru dereva wao aondoe gari kwa kasi.
“Jamani mbona mnanipiga? Nina makosa gani mie?” Aliuliza Nicholaus kwa kiswahili lakini hakuna mtu aliyemwelewa, alivutwa na kupelekwa katika chumba kilichokuwa pembeni kabisa mwa uwanja na kuketishwa chini na kuendelea kupigwa bila kulielewa kosa lake.
Nicholaus alilia kwa maumivu akiwaomba askari wamweleze kosa lililowafanya wampige hakuna mtu aliyemwelewa walionekana kutoelewa kiswahili! Muda mfupi baadaye aliingia msichana mmoja mrefu wa Kiafrika na kuchuchumaa mbele ya Nicholaus aliyekuwa amelala chini akilia.
“Ninaitwa Joan Leon wewe mtoto unaitwa nani?” Aliuliza dada huyo katika kiswahili.
Nicholaus alishtuka na kusikia mtu akiongea kiswahili tena Mwafrika kama yeye, aliona amepata mkombozi! Aliruka na kumng’ang’ania msichana huyo miguuni.
“Nisaidie dada wanataka kuniua bila kosa wamenipiga mno bila kosa lolote tafadhali nisaidie dada nimefurahi kukuona mswahili mwenzangu,nisaidie dada wataniua!” Aliongea Nicholaus huku akilia machozi.
“Wewe ni nani?”
“Naitwa Nicholaus!”
“Nicholaus nani?”
“Martin!”
“Tanzania unaishi wapi?”
“Naishi Arusha!”
“Mimi ni Mtanzania naishi hapa Tehran nafanya kazi katika ubalozi wetu hapa, sasa naomba unieleze ni kwanini unafanya biashara ya madawa ya kulevya wakati unajua kabisa katika nchi hii adhabu yake ni kifo cha kupigwa risasi hadharani?”
“Madawa? Madawa gani dada yangu?”
“Haya yaliyomo ndani ya sanduku lako!”
“Ndani ya sanduku kuna madawa?Madawa gani?”
“Ya kulevya!” Alijibu dada huyo na kulifungua sanduku la Nicholaus na kumwonyesha paketi za madawa zilizokuwemo ndani, Nicholaus alitetemeka.
Nicholaus alielewa alikuwa ameingizwa katika mtego bila kujua! Alielewa ni kwa sababu gani Samwel na AbdulAziz hawakutaka kuongea naye tangu Arusha! Kumbe walimtumia kusafarisha madawa yao! Alilia kwa uchungu na aliyakumbuka maneno ya dada yake uwanja wa ndege!
Alipomkumbuka Vicky alilia zaidi alijua sasa alikuwa anakufa tena kwa kupigwa risasi mbele ya halaiki ya watu! Alipofikiria jinsi risasi zingepenya mwilini mwake alizidi kuchanganyikiwa zaidi! Hofu ilimtanda mwili mzima, aliumia kufa na kumwacha dada yake kipofu peke yake duniani, alijua ni shida kubwa kiasi gani iliyokuwa ikimsubiri Vicky mbele yake.
“Kifo changu kitamsikitisha sana Vicky na sijui atajuaje kama nimekufa, masikini yeye ataendelea kujua nipo hai!” Aliwaza Nicholaus huku akilia.
***
MBELE YA HALAIKI

Siku iliyofuata mamia kwa maelfu ya wakazi wa jiji la Tehran walifurika katika uwanja wa Al-akri, uliotumika kuulia wahalifu ili kushuhudia kifo kingine cha muuza madawa ya kulevya biashara iliyochukiwa na kila mtu nchini humo!
Hakuna aliyemsikitikia muuza madawa alipopigwa risasi ilikuwa furaha kubwa kwa watu wa Iran! Nicholaus alifungwa kwenye mti mkubwa kwa kamba nene na nzito huku akiwa amefungwa na kitambaa cheusi usoni! Askari kumi wakiwa na bunduki zilizojazwa risasi kikamilifu walisimama mbele yake wakiwa wamemlenga wakisubiri amri kutoka kwa mkuu wa kitengo cha kuuza madawa!
Nicholaus aliendelea kulia machozi akijieleza ni kiasi gani hakuwa na hatia! Lakini hakuna aliyejali watu wote kiwanjani walionekana kufurahia kifo chake. Mawazo yake yote yalikuwa kwa Vicky, aliumia kufa kumwacha dada yake peke yake duniani aliamini alikuwa akiwafuata baba na mama yake ahera.
“Kama ningemsikiliza dada yangu Vicky haya yote yasingenikuta!” Aliwaza Nicholaus akisubiri risasi ziupenye mwili wake, alihisi ganzi mwili mzima na hakujua jinsi ya kujiokoa.
“Nahesabu moja na nikifikisha tatu wote mtafyatua bunduki zenu mpaka risasi zote ziishe nataka huyu mtoto asambae kabisa! Hatutaki madawa ya kulevya katika nchi yetu au siyo wananchi?” Alisema mkuu na watu wote walishangilia.
Nicholaus alishindwa kuelewa ni kwanini watu wa Iran hawakuwa na huruma kiasi hicho!Aliendelea kumwomba Mungu afanye muujiza ili kumuokoa katika kifo hicho.
“Haya moja….mbili….!” Alihesabu mkuu.
***

Kwa wiki nzima Vicky alishinda na kukesha akilia machozi, alimlilia kaka yake Nicholaus waliyezaliwa naye mapacha! Leah alijitahidi kwa uwezo wake wote kumfariji lakini haikusaidia Vicky aliendelea kulia. Kwa siku tatu mfululizo alikaa bila kula wala kunywa kitu chochote, Leah alikwenda kazini asubuhi na aliporudi jioni alikuta chakula alichokiacha kipo vilevile, Vicky alikonda na kukondeana kiasi kwamba Leah aliogopa na kufikiri Vicky angekufa kwa njaa!
“Sikiliza Vicky maisha yetu unayajua Mungu hata kama ukilia miaka miwili haisaidii kitu kama Mungu amepanga Nicky asafari na kurudi salama atarudi tu! Wala usiwe na wasiwasi kula tu mdogo wangu yote mwachie Mungu kwani yeye ndiye anayeyafahamu maisha yetu, usiache kula utaharibu afya yako bure mdogo wangu!” Kila siku Leah alimbembeleza Vicky ikabidi hata kazini aombe ruhusa na siku ya nne Vicky alikubali kula tena lakini aliendelea kumlilia kaka yake.
***

Kwa Vicky maisha hayakuwa kamili bila kaka yake Nicholaus! Kila siku baada ya kwake ilijaa mawazo na simanzi!Kila mara alilia akimlilia kaka yake! Leah alijitahidi kufanya kila kilichowezekana kumsahaulisha fikra juu ya kaka yake lakini haikuwezekana, Vicky alizidi kupoteza uzito wa mwili wake!
Kipande cha noti alichoachiwa na kaka yake ndicho kilichomhuzunisha zaidi, hakuwa na uwezo wa kufanya nacho jambo lolote, asingeweza kukitumia kununua kitu chochote mpaka kipande cha pili kipatikane, kipande alichoondoka nacho Nicholaus.
“Mpaka Nicholaus arudi ndio pesa hii itatumika tena!”
Alishinda nacho na kulala nacho mkononi mwake, kwake kipande hicho kilikuwa ni kaka yake mara kwa mara alikibusu na kukisemesha kama anaongea na binadamu! Vicky alikuwa tayari kupoteza kitu kingine chochote katika maisha yake lakini si kipande hicho cha noti!
Kila jumapili siku ambayo Leah hakwenda kazini, alijitahidi kumchukua Vicky na kwenda nae mjini kutembea ili kumsahaulisha machungu aliyokuwa nayo lakini haikusaidia bado Vicky aliendelea kumlilia kaka yake kadri siku zilivyokwenda.
“Hakuna kilichobaki kwangu! Sina baba, sina mama na sina hata kaka mtu pekee niliyenaye ni wewe Leah na ninakushukuru sana bila wewe sijui maisha yangu yangekuwaje!” Alisema Vicky.
“Watu wote tunaweza kukuacha Vicky lakini rafiki mmoja tu hawezi kukuacha, unajua rafiki huyo ni nani?”
“Ni wewe!”
“Siyo mimi Vicky ni Yesu Kristo!”
“Ha! Leah ina maana na wewe ipo siku utaniacha?”
“Hakuna kinachoweza kunitenganisha na wewe ninakupenda mno Vicky!”
Tangu siku hiyo Vicky alijifunza kumtegemea Mungu katika kila kitu alichofanya, kila siku ya jumapili Leah alimchukua na kumpeleka kanisa ambako alimwomba Mungu amlinde kaka yake popote alipokuwa ili siku moja awakutanishe tena! Alishindwa kuelewa siku ya kukutana na Nicholaus angekuwa na furaha kiasi gani.
Hakuna hata siku moja aliyotembea bila kukichukua kipande chake cha noti, alikwenda nacho kanisani alikwenda nacho chooni na kwa kufanya hivyo aliamini alitembea na kaka yake na kufurahisha moyo wake, kila kumbukumbu za maisha yake ya zamani akiwa na wazazi wake, akiwa na macho yake mawili na jinsi ajali ilivyotokea zilipomwijia alishindwa kuvumilia na kulia machozi!
Maisha yake yalikuwa yamebadilika mno, kupoteza familia na ndugu lilimuumiza sana na kutoka katika familia yenye maisha ya kifahari hadi kuishi katika chumba kimoja ambacho yeye na Leah wakitandika na kulala kwenye jamvi kulikuwa ni kushuka kwa hali ya juu!
Leah alilifahamu jambo hilo lakini siku zote hakuwa tayari kuliongelea kwa sababu kwa kufanya hivyo alijua angemuumiza sana moyo Vicky! Siku zote alikaa kimya na kujifanya maisha yalikuwa yakienda kama kawaida.
“Usijali Vicky ipo siku maisha yetu yatakuwa kama zamani hasa Nicholaus akirudi!”
“Kweli dada?”
“Ndiyo!”
Kwa Vicky, Leah hakuwa hausigeli tena bali baba, mama na kila kitu alichohitaji.
***

Siku, wiki, miezi ilizidi kupita hatimaye mwaka ukapita Leah akiendelea kufanya kazi nyumbani kwa tajiri yake wa Kihindi aliyeitwa Shabir Hussein, alikuwa Mhindi tajiri na mwenye roho nzuri sana, alisaidia Leah kwa kila kitu alimiliki mali nyingi sana mjini Arusha, mashamba ya Mkonge mkoani Tanga ilisemekana pia alimiliki viwanda nchini Canada na Uingereza.
Siku ya kwanza aliyofika nyumbani walipoishi Leah na Vicky, Shabir alilia hakuamini Leah aliishi sehemu chafu kiasi kile, alimwonea huruma sana hasa alipomwona mtoto wa kike kipofu Vicky aliyeishi naye.
“Tangu sasa nitakusaidia Leah wala usiwe na wasiwasi wowote!”
“Nashukuru sana baba!” Hivyo ndivyo Leah alivyomwita mzee Shabir siku zote, alikuwa ni mzee mwenye umri wa miaka kati ya hamsini na sitini.
Wiki mbili baadaye Leah na Vicky walihama katika chumba kimoja walichoishi kwenda maeneo ya Sanawari ambako Shabir Hussein alimnunulia Leah nyumba ya vyumba vitatu iliyokuwa na uzio kabisa! Ilikuwa ni nyumba nzuri ya kifahari yenye kila kitu ndani mpaka seti ya televisheni, aliwawekea pia mfanyakazi wa ndani aliyepewa kazi ya kumtunza Vicky!
Kwa Leah hiyo ilikuwa ni bahati kubwa ambayo hakutegemea kuipata, siku ya kwanza aliyoingia katika nyumba hiyo na kulala kwenye kitanda na godoro kubwa wala hakuamini! Alifikiri ilikuwa ni ndoto! Kwa upande wa Vicky pamoja na kuwa kipofu bado alielewa kuwa nyumba waliyoishi ndani yake wakati huo ilikuwa ya kifahari, sauti za televisheni na redio zilimkumbusha maisha yake na wazazi wake kabla ya kifo chao kilichochukua kila kitu kutoka kwake na kumwacha masikini.
“Hivi ni kwanini Shabir ameamua kutusaidia kiasi chote hiki?” Hilo ndilo swali ambalo Leah alimuuliza Vicky mara kwa mara.
“Katuonea huruma!” Ndilo lilikuwa jibu la Vicky
“Kweli?”
“Ndiyo dada inaonekana ana roho nzuri sana!”
“Lakini nina wasiwasi kidogo!”
“Kwanini?”
“Basi tu!”
***

Tangu tajiri Shabir atoe msaada wake kwa Leah tabia yake nyumbani ilibadilika kiasi kikubwa, kila mara alimsifia Leah kwa nguo alizovaa na alimzuia kufanya kazi chafuchafu kama kuosha vyombo na kupiga deki chooni! Muda mfupi baadaye alileta wasichana wengine wawili kutoka Sengerema kufanya kazi za ndani Leah akawa anashinda bila kazi yoyote.
Kwa sababu hiyo Shabir aliamua kumhamishia kwenye moja ya maduka yake katikati ya mji wa Arusha akawa anamsaidia kuuza mali mbalimbali!
Miezi michache hali hiyo ilimfanya mke wa Shabir ahisi kulikuwa na kitu fulani kati ya mume wake na Leah, ilitokea hali ya kutoelewana kati yao nyumba ikawa haina amani Leah akilalamikiwa kuingilia ndoa yao jambo ambalo halikuwa na ukweli wowote.
Baadaye mke wa Shabir, Sandra alimshinikiza mumewe ili amfukuze kazi Leah au yeye aondoke kurejea kwao Bombay! Shabir hakukubaliana na hilo mkewe akaondoka kurejea kwao India! Hofu ilimsumbua Leah kuwa angeweza kudhurika lakini Shabir alimwondolea wasiwasi huo na maisha yaliendelea kama kawaida.
Shabir na mkewe waliishi katika ndoa kwa miaka ishirini bila kupata mtoto, hivyo alipoondoka kurudi India mkewe aliondoka na mabegi peke yake.
Kuondoka kwa mkewe kulimfanya Shabir awe mpweke katika maisha yake na ni kipindi hicho ndicho alianza kumwangalia Leah kwa jicho tofauti! Alianza kugundua alikuwa msichana mzuri, kwa mara ya kwanza aligundua alikuwa na mahipsi na alikuwa na chuchu zilizosimama.
Hakuwahi kugundua kuwa Leah alikuwa na mwanya na alipocheka aliyaacha vishimo katika mashavu vyake! Aliyagundua yote hayo kuanza kuchanganyikiwa kimapenzi taratibu, hakuvumilia kwa muda mrefu sana na kujikuta akitoboa kila kitu kwa Leah siku moja usiku wakifunga duka.
“Mimi penda veve Leah, wewe iko taka nini?Taka jumba? Au taka gari? Wewe sema mimi iko pesa bana, mimi taka veve zalia mimi toto juri sawa?”
“Hapana mzee Shabir haiwezekani mimi nakuheshimu sana siwezi kufanya hivyo!” Alikataa Leah tena akinyanyuka.
“Oho! Veve pana taka mimi siyo? Basi veve toka dani ya jumba yangu keso!” Mzee Shabir alipiga mkwara
Jibu la mzee Shabir lilimshtua Leah kwa maisha aliyokwishazoea isingekuwa rahisi kuyaacha tena! Alipofikiria kuondoka katika nyumba kubwa aliyopewa alishindwa, hakutaka kurejea katika maisha yake ya zamani.
Pamoja na kuwa umri wake ulikuwa mdogo mno alipoyafikiria hayo alijikuta akilegea mzee Shabir alipomkamata na kumtupa juu ya meza! Aliyoyafanya mzee Shabir kwa binti mdogo kama Leah siku hiyo yalikuwa ni unyama usioelezeka kwa kalamu wala karatasi.
Baada ya ukatili wa kumbaka alimbeba Leah hadi ndani ya gari lake kumrudisha nyumbani usiku huo huo, siku iliyofuata Leah alishindwa kunyanyuka kitandani na kwa siku nyingine tano zilizofuata alibaki ndani amelala chali! Vicky alipouliza juu ya kilichompata hakuwa tayari kusema ukweli, ilikuwa siri yake tena siri ya kufa nayo moyoni mwake.
Katika siku zote hizo tano Shabir alilala nyumbani kwa Leah akimuuguza kama mtu na mke wake na huo ndio ukawa mwanzo wa penzi lao zito! Miezi mitano baadaye Leah alijikuta mjamzito jambo lililomfurahisha sana mzee Shabir. Hicho ndicho kitu alichokitaka siku zote kutoka kwa mwanamke.
Mapenzi yake kwa Leah yalizidi ingawa wahindi wenzake walimtenga kwa sababu ya kuoa mwanamke wa Kiafrika bado hakujali alichotaka ni mtoto wa kurithi mali zake nyingi na tayari alikuwa amempata.
Leah akawa si mfanyakazi wa Shabir tena bali mpenzi wake na watu wote mjini Arusha walilielewa jambo hilo, haikuwa siri tena kuwa Shabir alimuoa mfanyakazi wake Leah! Mimba ilizidi kukua na hatimaye miezi tisa ilipotimia Leah alijifungua mtoto wa kiume mwenye sura sawasawa na baba yake waliyemwita Lanjit.
Maisha yao yaliendelea vizuri katika familia yao kitu pekee kilichomsumbua Vicky akilini mwake kilikuwa ni fikra juu ya kaka yake Nicholaus, alikuwa bado hajamsahau na bado alikitunza kipande cha noti alichoachiwa na kila siku alimkumbuka katika maombi yake ili Mungu ampe uzima.
“Leah mimi sasa taka chukua wewe moja kwa moja! Taka veve kuwa mke yangu ili tufunge doa yetu lakini lazima veve badili dini yako kuwa Muislam sawa?”
“Sawa tu haina shida! Naweza kubadili!”
“Kweli veve naweza?”
“Ndiyo naweza sababu Mungu ni mmoja!”
Wiki moja iliyofuata tayari Leah alishabadili dini yake na kuingia katika dini ya Uislamu jina lake likabadilika kuwa Fatma Shabir! Mpango wa kubadili dini ulifanywa kwa siri ili Vicky asielewe, lakini hicho hakikuwezekana kwani siku mbili tu baadaye Shabir alirudi nyumbani na kumwita Leah kwa jina la Fatma! Ilibidi Vicky aulize juu ya jambo hilo na kuelezwa wazi kuwa Leah alibadili dini!
Vicky alilia sana baada ya kusikia habari hiyo alihisi kusalitiwa na Leah, alijaribu kumuuliza ni kwanini alifikia uamuzi huo.
“Ninampenda Shabir na pia mwanangu Lanjit!” Hilo ndilo lilikuwa jibu lake.
Baada ya ndoa yao tabia ya Leah ilianza kubadilika, Vicky aliligundua hilo mapema! Mapenzi yake yalihamia kwa mtoto wake na mume wake zaidi kuliko ilivyokuwa siku za nyuma. Kila siku ya Ijumaa Leah alikwenda msikitini na siku za kawaida aliswali sala tano kama ilivyo taratibu katika Uislamu akawa ni mama wa Kiislamu haswa!
***

Shabir alimpiga marufuku mkewe Leah kukanyaga kanisani hilo lilimfanya ashindwe kumpeleka Vicky kanisani kusali kila jumapili, akawa anashinda nyumbani kwa sababu asingeweza kutembea peke yake akiwa kipofu!
Roho ilimuuma sana Vicky na kumfanya awe anasali chumbani kwake kila Jumapili kitu ambacho hakutaka kukifanya, zilipopita wiki mbili mfululizo bila Vicky kuonekana kanisani waumini waliamua kufuatilia, aliwasimulia kila kilichotokea walisikitika na siku iliyofuata ulipangwa utaratibu wa mtu kuwa anakwenda nyumbani kwao kumchukua na kumrudisha nyumbani baada ya ibada.
Jambo hilo lilimkera sana Shabir na hata Leah ambaye tayari alishaanza kumgeuka Vicky kwa sababu ya mume wake! Wao walitaka familia yao yote iwe ya Kiislamu lakini Vicky akakataa kufanya hivyo, jambo ambalo Shabir alilichukulia kama dharau na chuki yake dhidi Vicky iliongezeka maradufu hata salamu yake akawa hapokei.
Vicky alihisi tatizo lilikuwa likija mbele yake, kumbukumbu juu ya kaka yake ziliongezeka lakini alimwomba Mungu amuepushe na mabaya! Mara nyingi alimlilia Nicholaus lakini wakati huo hapakuwa na mtu aliyemjali wala kumbembeleza tena kama alivyofanya Leah kabla hajabadilika! Hali hiyo ilimzidishia Vicky machungu.
***

Mabadiliko ya mfumo wa ukusanyaji wa kodi na kuanzishwa kwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) nchini Tanzania kuliwaogopesha wafanyabiashara wakwepa kodi! Wengi walidai kodi ya Tanzania ilikuwa hailipiki.
Miongoni mwa wafanyabiashara hao alikuwemo Shabir, hakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kuamua kuhamia Canada nchi ambayo wafanyabiashara wengi wa Kiasia walikimbilia! Ilidaiwa Shabir alikuwa na nyumba aliyonunua miaka ya themanini, aliuza kila alichokuwa nacho na kuzituma pesa zote nchini Canada.
“Mke wangu nataka hamia Canada lakini iko kitu moja nataka veve saidia mimi! Mimi hapana jua kama veve itakubali”
“Kitu gani mume wangu?”
“Veve najua kuwa mimi hapana taka Vicky siyo!”
“Ndiyo!”
“Mimi na veve hamia Canada lakini mimi hapana taka ondoka na hiyo kipofu!”
Leah alishindwa kujibu swali hilo na kukaa kimya kwa muda akifikiria jinsi ya kufanya uamuzi! Picha ya wazazi wa Vicky na Nicky zilimwinjia kichwani mwake ghafla, aliukumbuka wema ambao walimfanyia, kwake bila wao asingefika alipokuwa! Roho ilimuuma sana alishindwa aamue nini kwani kumwacha Vicky peke yake nchini Tanzania akiwa kipofu ilikuwa ni sawa na kumtupa jalalani!
“Sikia?” Shabir alimuuliza tena.
“Ndiyo nimesikia mume wangu!”
“Sasa veve sema nini maana mimi tayari kwisha uza kila kitu kwa Karimjee na pesa imetangulia Canada, si ajabu tukaondoka wiki ijayo!”
Kabla hajajibu swali hilo mlango wa chumbani kwa Vicky ulifunguliwa akatembea peke yake huku akipapasa ukuta kuelekea sebuleni, alijikwaa na kuanguka mguuni kwa Leah! Alikuwa ameyasikia maongezi yao.
“Dada Leah, tafadhali kataa, usiniache peke yangu, nakupenda dada ni wewe pekee niliyekubakiza duniani usiniache tafadhali!” Aliongea Vicky huku akilia.
“Weee hebu nyamaza pesi hapana piga kelele, kama wewe taka mimi ondoka na wewe lazima ubadili dini vinginevyo utabaki hapahapa! Mpumbavu wewe tabadili au no?”
“Mimi! Mimi! Mimi!……!” Vicky hakumaliza sentensi yake kwikwi ikamshika akamwaga machozi.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumanne hapahapa.

Tu-Follow kwenye mitandao ya kijamii;

Facebook @Globalpublishers

Twitter @GlobalHabari

Instagram @GlobalPublishers

YouTube @GlobalTVTZ

Endelea kutembelea website ya Global Publishers kila siku, tutaendelea kukusogezea kila news inayotokea mahali popote duniani.

Comments are closed.