The House of Favourite Newspapers

USTADHI: MO SALAH ALIUMIA KWA KUPUUZA MFUNGO WA RAMADHAN

MHUBIRI Mubarak al-Bathali wa nchini Kuwait amesema kwamba kuumia kwa mcheza soka wa klabu ya Liverpool Uingereza, Mo Salah, ni adhabu ya Mungu kwa kuvunja mfungo wa Ramadhani kabla ya mechi yao dhidi ya Real Madrid ya Hispania.

 

Mchezaji huyo aliumia begani katika fainali hiyo ya Mabingwa ya Ulaya alipokuwa akipambana na mchezaji Sergio Ramos katika dakika ya 31 ya mchezo huo ambapo Liverpool ilishindwa 3-1. Ustadhi huyo alisema siku iliyofuata kwamba mchezaji huyo alipatwa na tatizo hilo kutokana na “Mungu kumuadhibu” kwa kula kabla ya mechi hiyo wakati wa Mwezi Mtukufu.

 

Alisema japokuwa Waislam huruhusiwa kufungua mfungo huo wanaposafiri, kitendo chake kula ili acheze katika mpambano huo wa fainali “haikuwa sababu halali”, hivyo Salah alikuwa amefanya dhambi. Kiongozi huyo wa dini aliongeza kwamba Salah alikuwa amedhamiria kufungua mfungo wake kwa ajili ya mechi hiyo na si kwa vile alikuwa anasafiri kutoka Uingereza kwenda Ukraine, hivyo dhamira yake ndiyo iliyomponza.

Daktari wa masuala ya viungo wa Liverpool, Ruben Pons, alikuwa amethibitisha mapema kwamba Salah angefungua mfungo huo kwa ajili ya mechi hiyo, jambo ambalo lilikuwa limejadiliwa likimhusisha mataalam wa masuala ya vyakula.

 

“Kesho na siku ya mechi hatafunga, hivyo hataathirika kwa vyovyote,” Pons alikiambia kituo cha radio cha Hispania cha Caden SER kabla ya mechi hiyo. Hata hivyo, ustadhi Al-Bathali alisema Salah (25) alipewa ushauri mbaya na ndiyo maana matatizo hayo yalimfika.

 

 

Kuumia kwa mshambuliaji huyo wa Misri kulimweka katika wasiwasi wa kutoshiriki michuano ya fainali za Kombe la Dunia nchini Russia itakayoanza Juni 14 mwaka huu, jambo ambalo ustadhi huyo alisema litamkumbusha mwanasoka huyo kwamba kila kitu hutokea kutokana na utashi wa Mungu.

 

“Usifikiri Waislam wanaamini kwamba maisha huongozwa na hoja na juhudi, bali maisha ni mkono wa Mungu unapofika kwa mwenye juhudi na asiye na juhudi,” alisema. Hata hivyo, viongozi wa soka wa Misri wamesema jana (Jumatano) kwamba Salah atakuwa katika hali njema baada ya muda mfupi na atashiriki michuano hiyo ya Kombe la Dunia.

Comments are closed.