UTATA WAIBUKA MGAO MALI ZA MONDI

BAADA ya hivi karibuni msanii maarufu wa muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kuposti kwenye ukurasa wake wa Instagram kwamba siku akifa ule mjengo wake wa Madale na nusu ya mali zake zimilikiwe na mama yake mzazi, Sanura Kassim ‘Sandra’, utata umeibuka juu ya wosia wake huo.

ALIANDIKAJE?

Katika kumwandikia mama yake maneno ya kuonesha upendo kwenye siku yake ya kuzaliwa, Diamond aliandika hivi: Nasikitikaga sana wanapojaribu kulinganisha thamani yako kwangu na mtu yoyote…na kusahau kuwa pasipo wewe kunizaa na kunilea kwa shida na tabu, leo hii hakuna yoyote ambaye angeniona wa maana…..

 

Ikiwa wewe ndio ulonifanya mie nikawa duniani, basi you will always be my first priority then the rest will follow…Dharau na manyanyaso ulopitia kwenye kunilea hakuna anayejua, tabu na shida ulizopitia kufanya hadi leo walau nionekane mtu mbele za watu.. eti mtu kirahisi tu anatokea na kukulinganisha na mtu. Mama MADALE is your house! Ikitokea kesho nimekufa pia nusu ya mali zangu zote ni zako.

UTATA WAIBUKA

Baada ya Diamond kuposti maneno hayo, utata ukaibuka kuhusu mgawanyo huo huku baadhi ya watu wakihoji kwa nini aandike maneno hayo wakati ana watoto na pia baba yake mzazi yu hai.

Wadau hao walienda mbele zaidi na kueleza kuwa, kwa sheria za dini yake ya Kiislam, watoto wote wa Diamond hawana chao kwani wamezaliwa nje ya ndoa na kwamba ikitokea amekufa, wazazi wake na ndugu zake wa kuzaliwa nao ndiyo wanatakiwa kurithi mali zake.

 

“Unajua kwa alichosema Diamond kuna sheria za dini ya Kiislam na zile za serikali. Kwa mfano leo hii Diamond akifariki, kwa mujibu wa dini yake ya Kiislam mali zake zinatakiwa kurithiwa na wazazi wake kwa kuwa hajaoa, watoto alionao hawana vigezo vya kurithi mali zake.

“Sasa kwenye hili utata unakuja hivi, yeye anasema akifa nusu ya mali zake achukue mama, vipi kuhusu baba yake ambaye yupo? Na vipi kuhusu nusu ya mali ambazo zinabaki, zitamilikiwa na nani? “Kifo tunatembea nacho, kesho na keshokutwa akifa anaweza kuleta mkanganyiko, kwa hiyo alitakiwa kuweka wazi mgawanyo kamili wa mali zake. Je, anataka nusu ya mali zake wapewe dada zake au apewe nani?” alisema Sued wa Kinondoni jijini Dar baada ya kuona maneno hayo ya Diamond.

 

BABA DIAMOND HANA CHAKE?

Kuna wakati Diamond aliwahi kusema kuwa, yeye na baba yake wamemaliza tofauti zao licha ya baadhi ya watu kuhisi bado hawako sawa, imekuwaje leo aandike kuwa mali ziende kwa mama asimtaje kabisa baba wakati kidini baba naye ana sehemu yake?

Hata hivyo imeelezwa kuwa, kwa kuwa Diamond hakumtaja baba yake kwenye wosia wake huo, endapo akifa mzee huyo hatakuwa na chake labda aambulie chochote kupitia kwa mama au wale wengine watakaoambulia nusu ya mali zake.

Utata mwingine ni kutokana na watu kuhoji kuhusu hatua yake hiyo ya kuongea mambo ‘siriasi’ mitandaoni kama amemaanisha au ni kiki na kama alimaanisha, kwa nini asilifanye jambo hilo likawa siri ili kuepusha manenomaneno kwa ndugu zake wengine wanaozitolea udenda mali zake? Lakini wapo waliopata utata kuhusu wosia na kuhoji kwamba, amesimamia sheria gani, za dini yake ya Kiislam au za kiserikali?

 

KWANI DINI INASEMAJE?

Katika kujua taratibu za mirathi kwa dini ya Kiislam, mwandishi wetu alimpigia simu Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar, Alhad Mussa ambaye alisema hakuwa kwenye nafasi nzuri ya kulifafanua hilo lakini Mnajimu na Mtabiri maarufu nchini, Maalim Hassan Yahya Hussein alipoulizwa alisema hivi;

“Mwanaume wa Kiislam akifariki dunia, kama ameoa, mke wake anatakiwa kurithi thumni ya mali ya mumewe ikiwa na maana ya moja ya nane ya mali zote. “Kama mwanaume huyo amejaaliwa watoto wa kike na kiume, watoto wa kiume hupewa theluthi mbili za mali na watoto wa kike hupata theluthi moja.

“Mtoto wa kike hupewa theluthi moja kwa sababu anaweza kuja kuolewa na mumewe akifariki dunia, huko atapata moja ya nane ya mirathi lakini huyu wa kiume hana nafasi hiyo tena,” alisema na kuongeza: “Lakini kama kuna mtoto kazaliwa nje ya ndoa, haambulii chochote labda baba yake kabla ya kufa ampe sehemu ya mali zake za zawadi au aandike tu kuwa, nikifa mtoto wangu flani wa nje ya ndoa apewe kitu flani, siyo kwa kurithi bali zawadi tu.”

 

KUHUSU MOBETO NA ZARI

Kutokana na wosia alioandika msanii huyo, baadhi ya wadau walihoji kuhusu wanawake waliozaa na Diamond, Zarinah Hassan ‘Zari’ na Hamisa Mobeto kwamba watanufaikaje lakini Maalim Hassan akasema, wao kama ni kunufaika basi iwe ni kwa kipindi hiki Diamond akiwa hai, akifa nao hawana chao.

DIAMOND ASHAURIWA

Katika hili la wosia wa Diamond, baadhi ya watu walisema si jambo baya kama alichokiandika alimaanisha lakini ni vyema akakiweka kwenye maandishi na kuwashirikisha wanasheria ili kuepusha migogoro pale ambapo Mungu atakuwa amemchukua.

 

DIAMOND ANASEMAJE?

Jitihada za kumtafuta Diamond ili kuzungumzia kuhusu wosia huo hazikuzaa matunda kufuatia simu yake ya mkononi kuita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

KWANI DIAMOND ANAMILIKI MALI GANI?

Gazeti hili linachimba ili kujua kwamba, kwa sasa mbali na Diamond kumiliki studio ya Wasafi Records, Nyumba ya Madale ana nyumba zipi nyingine na ziko wapi? Ana magari gari na mangapi hadi sasa? Je, ni kweli ana daladala, bajaj na bodaboda kadhaa kama inavyodaiwa? Na je, kuna mali gani nyingine ambazo anamiliki? Haya yote utayasoma kwenye matoleo yajayo ya gazeti hili.

STORI: Mwandishi Wetu, Risasi Mchanganyiko

Loading...


Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment