The House of Favourite Newspapers

Viporo Vimeimaliza ligi kuu, Haina Mvuto Tena

Wachezaji wa timu ya Simba.

UKISEMA Ligi Kuu Bara ya nini tena utakuwa sahihi kabisa. Maana inakwenda kupoteza mvuto na lazima tujiulize, tatizo liko wapi? Nani anaweza kukataa kwamba waendeshaji wa Ligi Kuu Bara si watu makini? Maana hawana sababu ya msingi kufanya mambo yaende kama yanavyoenda sasa.

 

Nitakuambia kwa nini leo unaona hii athari na viongozi wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) na wale wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hawakuwahi kuwa na hesabu za maana. Hesabu zao zinaonyesha zilikuwa hazina imani na timu za Tanzania. Upangaji ratiba ni kabla ya ligi kuanza.

 

Hivyo kuna mambo mengi sana ya kuangalia, moja wapo ni michuano ya Caf upande wa klabu. Wapanga ratiba hawakuwa na imani na Simba, hili ni jambo baya na ndilo linalowatesa sasa na kuifanya ligi kuu kuwa mbaya na inayoshangaza na mwisho kabisa iliyopoteza mvuto.

 

Kwa kuwa hawakuiamini Simba, yaani walijua haina jeuri ya kwenda makundi, hivyo hawakuangalia ratiba ya makundi ya Caf inachezwa wakati gani. Upangaji wao haukuwa na tahadhari. Sasa Simba imevuka, kwao unakuwa msala unaozidi kuwafanya waonekane si watu makini.

Maana unaona Yanga inakwenda kucheza mechi ya 20. Hii maana yake inaingia mzunguko wa pili wa ligi. Kwa kuwa timu ni 20, kila timu inatakiwa kucheza mechi 19.

Yanga imecheza hizo 19 wakati Simba ikiwa na 14, Azam FC ina 17 lakini kuna timu kama Lipuli, Mbao FC zina 21 na KMC imefikisha 22. Maana yake hizi zilishavuka na kuingia mzunguko wa pili wakati Simba wana mechi tano za mzunguko wa kwanza mkononi. Yanga wanaongoza wakiwa na pointi 53, Azam FC wanafuatia wakiwa na 40 na Simba wana 33. Utamu wa ligi uko wapi sasa?

Kama zingekuwa zinalingana michezo au angalau kutofautiana miwili kama ilivyo kwa Azam na hasa kutokana na jukumu la kitaifa. Angalia Azam FC wanapishana na Yanga michezo miwili kwa sababu zipi za msingi. Au Yanga wanazidiwa michezo na KMC kwa sababu ipi hasa?

 

Hapa kuna kila sababu ya kupima uwezo wa wanaoendesha ligi na mimi niseme bila ya kupepesa. Kwa mara ya kwanza ndani ya zaidi ya miaka sita au nane, ligi hii itakuwa haina mvuto kabisa. Ukisema Simba wana majukumu ya kimataifa, angalia England, Italia, Hispania, Ujerumani na kadhalika.

Utajifunza jambo kwamba zipo timu zina majukumu ya kimataifa, tena si moja, zaidi ya manne na bado tofauti ni mechi moja au michezo yote iko sawa kabisa. Ligi inakuwa na ushindani kuanzia na pointi zinazoingia. Lakini pia lazima uangalie timu zimecheza michezo mingapi.

Ukiangalia ile P, yaani michezo waliyocheza, unaona kuna tatizo kubwa sana kwa kuwa kuna tofauti ya michezo zaidi ya mara nne katika timu, hili si sawa. TFF mnatakiwa kulisimamia hili maana kwa sasa mnasumbuka kupata mdhamini. Sidhani kama kampuni sitaonyesha nia ya kuingia kwa kuwa hakuna tena mvuto. Mnazifanya pia timu zinakosa watazamaji kwa kuwa hakuna watakaokuwa tayari kwenda uwanjani wakati wanajua kuwa kuna mwelekeo unaoonyesha ushindani umeporomoka.

 

Mkitaka mlibadilishe hili, basi kwanza mkubali mmekosea na inawezekana kufanya marekebisho kuiondoa hii hali. Mwisho niwape tahadhari kwamba, angalieni msije kuingia katika mgogoro mkubwa na Simba kama mtataka kuwalazimisha kucheza mechi nyingi mfululizo ili mfunike makosa yenu yanayotokana na uzembe wa kimahesabu

Comments are closed.