The House of Favourite Newspapers

Waamuzi Wamefikia Hatua Ya Kuharibu Utamu Wa Ligi

TAYARI tume­shashuhudia viwan­ja kadhaa hapa nch­ini mechi za Ligi Kuu Bara kwa msimu huu zikichezwa. Ni kwa muda mrefu burudani hiyo ya soka ilikuwa ikisubiriwa.

 

Timu 20 zimeanza kuonyesha uwezo wao ambapo baadhi yao zimecheza mechi mbili tayari huku zingine zikishuka dimbani mara moja.

 

Muamko wa mashabiki kwen­da viwanjani bado hauridhishi kwani wengi wao wameamua kubaki kuangalia kwenye run­inga, kuna umuhimu pia kwa mashabiki kuweza kufika katika viwanja kutoa sapoti kwa timu zao.

 

Kwa kufanya hivyo itakuwa rahisi kuweza kujenga imani na hali ya kujituma zaidi kwa wachezaji kwa lengo la kupata matokeo mazuri kwa kuwa uwepo wa mashabiki, wache­zaji wanapata nguvu ya kupam­bana.

Mambo mengi yanayotokea katika ligi hiyo ambayo inaen­delea, kuna umuhimu wa ku­chukua hatua mapema kwa yale ambayo si sahihi kabla ya matukio mengine makubwa hayajawa sugu wakati ligi ikien­delea.

 

Kabla sijakupeleka kwenye jamvi la leo, kuna umuhimu wa kuweza kuwapongeza vi­jana wetu wa Timu ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 17, Serengeti Boys, ambao wame­shiriki mashindano ya kufuzu kwa michuano ya Kombe la Mataifa Afrika chini ya umri huo (Afcon U17) kwa Ukanda wa Af­rika Mashariki na Kati (Cecafa) ambayo yalikuwa yana mvuto wa kipekee.

Ninachotaka kusema ni kwamba muda huu ni lazima Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liweze kuweka mikakati maalumu ya kuwatunza hawa vijana ili siku za usoni waweze kutumika kwenye timu ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars.

 

 

Kwa kuweza kuwekeza kwa hawa vijana kutafanya tuwe na kizazi ambacho kitakuwa na ushindani hasa kwenye mashindano ya kimataifa kwa kuwa tayari wana kitu cha kipe­kee walichonacho.

 

Tusikubali tukawapoteza kwani kwa kufanya hivyo haku­takuwa na maana yoyote ile hasa kwa maendeleo ya soka letu hapo baadaye kwa kuwa ni kizazi ambacho kinafundishika na kinaweza kuwa na manufaa makubwa kwetu sote.

 

Nikirudi kwenye kile nilic­holenga kukisema ni kwamba, katika mechi za awali zilizo­chezwa mpaka sasa, kuna mala­lamiko yamejitokeza kwa baa­dhi ya waamuzi juu ya uamuzi wao.

Tutambue kuwa vile utakavy­oanza ndivyo utakavyomaliza, ni muhimu kutatua mapema tatizo ambalo lipo ili kuendelea na ligi itakayokuwa na ushinda­ni na sio maneno kila siku.

 

Waamuzi wameonekana kuanza na makosa ambayo yamejitokeza waziwazi na kila mmoja ameyaona.

Jambo la kushangaza sana ni kwamba, waamuzi hao wengi wamefanya makosa ambayo yanafana kuhusiana na kutatua sheria ya kuotea.

Inapotokea timu imenyimwa haki yake, makocha, wachezaji na hata viongozi wa timu huwa kwenye maumivu makubwa jambo ambalo linawakatisha tamaa.

 

Mfano wa wazi ni katika mechi ya Coastal Union dhidi ya Biashara, mwamuzi alikataa bao lililofungwa kwa njia ya faulo na Biashara hali ambayo inaleta maswali ambayo mengi hayana majibu.

Pia hata ile mechi ya Ruvu Shooting dhidi ya KMC, tuliona kwamba kuna bao lilifungwa na Ruvu Shooting nalo lilikataliwa kwa madai kwamba mfungaji kabla ya kufunga, alikuwa am­eotea.

 

Inafahamika wazi kwamba waamuzi nao ni binadamu kama walivyo wengine, hivyo kuna kupitiwa, lakini kuna mambo mengine yanayojitoke­za yanakera sana kwa sababu huwa yanajirudiarudia.

Sitaki kuhusisha ishu hizi na mambo ya rushwa, bali nina­chotaka kusema ni kwamba, tunahitaji umakini katika kila idara ili kuifanya ligi yetu iwe na ushindani mkubwa.

 

Kigezo cha kukosekana kwa mdhamini mkuu kisitumike kwa baadhi ya timu kuanza ku­nunua mechi, kama kuna timu zinafanya hivyo zitakuwa zina­kosea sana.

Kumekuwa na dhana kwamba kwa timu ambazo zina uwezo wa kifedha ni rahisi kutengene­za mazingira ya kushinda mechi zake kwa njia yoyote ile jambo ambalo halikuzi soka letu bali linazidi kudidimiza.

 

Kama Shrikisho la Soka Tan­zania (TFF) litakubali ligi kuen­delea hivi bila ya kuwa na md­hamini kuna mambo mengi ya ajabu tutayashuhudia msimu huu ambayo yatashusha hadhi ya ligi yenyewe.

Suala la rushwa litazun­gumzwa sana msimu huu kwa kuwa kutakuwa na dalili nyingi juu ya suala hilo, hivyo ili kuwe­za kujiepusha katika hili kuna umuhimu wa kuweza kutafuta mdhamini ambaye ataweza kuzipa nguvu klabu katika ku­jiendesha na kuifanya ligi kuwa na ushindani wa kweli.

 

Kwa mazingira ambayo tunayapitia kwa sasa kuna uwezekano mkubwa sana kila timu itakaposhindwa ikaanza kuwashushia lawama waamuzi kwa kuwa tayari wameanza kuonyesha dalili ambazo zina­leta mashaka na kuwahusisha na masuala ya rushwa.

 

Pia msimu huu nadhani haku­takuwa na ule msisimko am­bao uliweza kuonekana msimu uliopita kutokana na ukweli kwamba timu nyingi ambazo zinashiriki ligi hazina mdhamini zaidi zinajiendesha zenyewe na suala la kuendesha klabu tuna­tambua kwamba si jambo dogo.

Comments are closed.