The House of Favourite Newspapers

Waarabu Waing’ang’ania Yanga Makundi Shirikisho

KABLA ya mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA England kati ya Manchester United na Tottenham Hotspur leo Jumamosi saa 1 usiku, Yanga tayari watakuwa wameshajua wamepangwa na nani kwenye makundi ya Kombe la Shirikisho tayari kwa mechi ya kwanza Jumapili ya Mei 6, mwaka huu.

 

Droo hiyo ya kupanga makundi inachezeshwa saa 9:00 alasiri jijini Cairo, Misri wakati mechi ya ligi baina ya West Bromwich Albion na Liverpool ikiendelea pale England.

 

Mechi zote za Yanga wikiendi italazimika kuzicheza Jumapili na katikati ya wiki ni Jumatano kwa mujibu wa CAF ambao ndio wamiliki wa haki za matangazo ya televisheni.

 

Yanga huenda ikajikuta ikatumbukia kwenye kundi lolote lenye timu za Afrika Kaskazini maarufu kama nchi za Kiarabu ambazo safari hii zimefuzu tano kutoka Algeria, Sudan na Morocco.

 

Vigogo wa Afrika waliofuzu ni USM Alger ya Algeria, Al-Hilal ya Sudan, AS Vita Club ya DR Congo, Enyimba ya Nigeria na Asec ya Ivory Coast.

 

Wengine ni Rayon Sports ya Rwanda, Gormahia ya Kenya, Williamsville AC ya Ivory Coast, Aduana Stars ya Ghana, UD Songo ya Msumbiji, Raja Casablanca, RS Berkane zote za Morocco na CARA Brazzaville ya Congo.

 

Pia imo Djoliba ya Mali na Al-Masry ya Misri iliyowatoa Simba.

 

Yanga imefika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya kuitoa Wolaitta Dicha ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 2-1, wakishinda nyumbani mabao 2-0 na kufungwa ugenini bao 1-0.

Comments are closed.