visa

WALIOKUFA KABLA YA NDOA, MABWANA HARUSI WAO WAPEWA TAHADHARI

DAR ES SALAAM: Hii inauma sana! Ndani ya wiki mbili zilizopita yametokea matukio mawili ya kusikitisha ya wasichana waliokuwa kwenye mipango ya kufunga ndoa kufariki dunia, jambo lililowaacha wenza wao kwenye wakati mgumu.

 

Moja ya misiba hiyo ni ule wa Doris Christiandus (35), mkazi wa Kijitonyama jijini Dar aliyefariki siku chache baada ya kuvishwa pete na mchumba wake aliyefahamika kwa jina la James. Doris alifariki dunia ghafla ambapo alianza kubanwa na kifua na alipokimbizwa hospitalini, mauti yakamfika.

 

“Alikuwa haumwi, alikuwa na furaha na mtu aliyeisubiri kwa hamu siku yake ya ndoa, lakini ghafla alianza kulalamika kubanwa na kifua mwisho akapoteza maisha,” alisema rafiki wa marehemu.

 

Mwili wa marehemu Doris ulisafirishwa hadi nyumbani kwao Songea kwa mazishi ambapo mumewe mtarajiwa aliwaliza wengi huku baadhi wakijiuliza jinsi atakavyoishi bila mwanamke wa maisha yake. Msiba mwingine ambao hata kupoa haujapoa ni wa bibi harusi Diana Jackson aliyefariki dunia wakati akienda kwenye sherehe ya ‘send off’ yake jijini Dar akitokea Mbeya.

 

Akizungumzia tukio la mkewe mtarajiwa kufariki dunia ajalini, bwana harusi aliyefahamika kwa jina la Elisante Edward alisema:

“Baada ya kuambiwa mchumba wangu amefariki, sikujua kilichoendelea, nilijiona sipo duniani kwa kuwa nipoteza fahamu.

“Nilipozinduka na kukutana na taarifa ileile ya kifo, niliishiwa nguvu, nikawa natamani isiwe kweli lakini haikuwezekana.

“Kila nilipokaa na kufikiria uhusiano wetu, mipango yetu ya maisha, nilikosa sababu ya kuendelea kuishi. Nikawaza kujimaliza na mimi ili uchungu niliokuwa nao uishe,” anaeleza Elisante akionesha jinsi alivyoumia.

 

MWANASAIKOLOJIA AWATAHADHARISHA ELISANTE, JAMES

Akizungumza na Uwazi, mwanasaikolojia Chris Mauki alisema kuwa, miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakiwaumiza sana binadamu ni kufiwa na wenza wao hivyo akatoa tahadhari kwa kusema:

 

“Jambo la kwanza linalohuzunisha zaidi ambalo lina kiwango cha asilimia 100 ni mtu kufiwa na mke au mume. Rekodi zinaonesha kuwa, watu wanaofiwa na wapenzi wao huwa na huzuni kubwa kiasi cha kutishia maisha yao.

“Msongo wa mawazo, mauzauza huwatokea na uchunguzi unaonyesha kuwa, wengi kati ya wanaofiwa na waume au wake nao hufariki siku, miezi au miaka michache baada ya kufiwa.

 

“Vifo hivyo husababishwa na msongo wa mawazo (stress). Mtu wa mfano aliyewahi kuniomba ushauri juu ya tukio la kufiwa na mchumba wake ni Jafari Hamza wa Mwanza. Huyu alipata ajali akiwa na mchumba wake, bahati mbaya mwenzake akafariki yeye akapona, ila tangu hapo halali, hali na anahuzunika kila kukicha.

 

“Jafari, pamoja na mamia ya watu wenye tatizo kama hili wanatakiwa kufuata muongozo nitakaoutoa leo ili waweze kuishi kwa amani na furaha, vinginevyo nao watatamani wafe tu.

“Kwanza ni kukubaliana na ukweli kwamba mwenza wako amefariki na hatarudi, kulia na kuhuzunika hakusaidii. Pili ni kuziondoa taratibu kumbukumbu zote zinazokuja na kutawala mawazo yako kuhusu mkeo/mumeo aliyekutoka.

 

“Usiyazamishe mawazo kwenye tukio hilo, ukiona unaanza kuwaza jishughulishe kwa kuondoka sehemu yenye upweke. Usipende kukaa peke yako kwa muda mrefu. Usiangalie picha na kutembelea kaburi lake kila mara.

 

“Usivute taswira ya maisha mliyokuwa mkiishi zamani. Kaa karibu na watu uwapendao, tembelea sehemu zenye kuvutia. Epuka kumzungumzia. Badili kabisa mazingira ya chumba mlichokuwa mkilala, kuwa bize na majukumu yako na andaa mipango ya kumtafuta mwenza mpya.”

 

Gazeti hili linatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na misiba hiyo na linawaombea mabwana harusi walioachwa na wenza wao Mungu awape nguvu na mioyo ya subira katika kipindi hiki kigumu.

Tukumbuke tu kwamba sisi ni wa Mungu na kwake tutarejea. Maalim anapatikana Magomeni Mwembechai-Dar.
Toa comment