The House of Favourite Newspapers

WANAWAKE WATUMIKA WIZI WA BAJAJ KIMAFIA

MOROGORO: Ni hatari tupu! Hicho ndicho kinachotokea kwa sasa mjini hapa kufuatia staili mpya ya wanawake kutumika katika wizi wa pikipiki za matairi matatu almaarufu Bajaj. 

 

Kumekuwa na matukio ya sampuli ambayo hayaripotiwi, lakini tukio jipya ni la kijana Omary Ally (32) ambaye ni dereva wa Bajaj katika Manispaa ya Morogoro aliyenusurika kifo baada ya kuporwa chombo chake hicho cha biashara.

 

Kwa mujibu wa mashuhuda wetu, kijana huyo alichanganyiwa ugoro kwenye bia na kuibiwa Bajaj hiyo. Hata hivyo, katika tukio hilo, alinaswa mwanamke mmoja ambaye alikuwa ni abiria wake aliyekuwa amefikia kwenye nyumba moja ya kulala wageni mjini hapa.

 

Tukio hilo lililijiri hivi karibuni kwenye nyumba moja ya kulala wageni (gesti) iliyopo Barabara ya Morogoro-Iringa. Kwa mujibu wa Omary baada ya kuzinduka, aliona amepata ngekewa ya abiria kumbe alikuwa amepatikana. Omary alisema kuwa mwanamke huyo alikuwa abiria wake kwa muda wa wiki mbili hivi ndiyo maana hakumtilia shaka.

Alisema mteja wake huyo alifika eneo analopaki Bajaj yake na kumuomba ampeleke sehemu mbalimbali za starehe huku akimuahidi kumlipa kwa siku nzima. Omary alibainisha kuwa alianza kwa kumpeleka mwanamke huyo katika Ukumbi wa Down Town ambako alifanya mambo yake hadi saa 6:00 usiku ambapo muda wote alikuwa akimsubiri.

 

Alisema kuwa mwanamke huyo alipomaliza starehe zake alimrudisha kwenye gesti aliyofikia ambapo walipofika alimtaka kutokuondoka kwani alitaka ampeleke kwenye ukumbi mwingine wa starehe wa Samaki-Samaki usiku huo. Alisema kabla ya kuondoka, mwanamke huyo alimpa bia mbili anywe wakati akimsubiri wakati akioga na kubadilisha nguo.

 

“Aliniambia wakati akijiandaa niingie nikae kwenye chumba alichofikia huku nikiendelea kunywa bia zangu,” alisema Omary. Alisema kuwa alipoingia chumbani humo, mwanamke huyo alivua nguo huku akimshuhudia kisha aliingia bafuni kuoga na huo ndiyo ulikuwa mwisho wake kumuona.

Alisema baada ya hapo alipoteza fahamu hadi alipozinduka na kujikuta akiwa wodini kwenye Hospitali ya Mkoa wa Morogoro akiwa ametundikiwa dripu huku Bajaj ikiwa imeshaibwa. Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (ACP), Wilbroad Mutafungwa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa jeshi hilo limefanikiwa kumkamata mwanamke huyo aliyefanya kitendo hicho pamoja na mwanaume mmoja ambaye alikuwa akishirikiana naye.

 

Hata hivyo, Kamanda Mutafungwa alisema kufuatia kuibuka kwa wimbi hilo la wanawake, madereva wa Bajaj na pikipiki wanatakiwa kuwa makini kutokana. Pia aliwataka kuacha kutegemea mteremko au ofa zisizokuwa na tija kwao na kuepuka vishawishi vya kimapenzi kutoka wateja wao hao ambao ni wanawake.

 

Kwa Mujibu wa Kamanda Mutafungwa, Omary anaendelea na matibabu na afya yake imeendelea kuimarika huku watuhumiwa hao wakiendelela kuhojiwa ili kujua mtandao huo wa wizi wa Bajaji na pindi upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

Comments are closed.