The House of Favourite Newspapers

Lukuvi: Wapangaji Nyumba za NHC Wahakikiwe Upya

WAZIRI wa Ardhi, William Lukuvi,  ametoa miezi minne kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakiki wapangaji wa nyumba  na majengo yao na kisha kuanzisha nyaraka za kielektroniki zitakazosaidia kubaini wajanja wanaopangisha na kujimilikisha nyumba za shirika hilo kinyume cha sheria.

Alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam baada ya juzi kutembelea miradi ya shirika na kutaka ifikapo Machi 30, mwakani, uhakiki huo uwe umekamilika.

“Ninajua kuna baadhi ya wapangaji wameanzisha vishirika vya nyumba ndani yenu, kuna watu wana nyumba mbili au tatu kwa ujanja wao na wanakodisha. Tutawaondoa wapangaji hewa na tutawatambua wamiliki hewa wa nyumba zilizotaifishwa.

“Kuna watu wakihama kwenye nyumba wanaziuza kwa gharama kubwa wanachukua fedha juu ya mgongo wa shirika hili kwa sababu inaelekea hatuna utunzaji wa kisasa wa takwimu za wapangaji na nyumba,” alisema.

Akitaka shirika hilo kuanzisha mfumo wa kijiditali kutunza kumbukumbu zake, alisema:

“Taarifa hizi ziingie kwenye mfumo wa Mamlaka ya Vitambulisho Vya Taifa (Nida), wapangaji wote lazima wafanyiwe uhakiki taarifa zao zifanane na taarifa za Nida.

“Kila mpangaji anapohamia kwenye nyumba tumjue anafanya kazi wapi, jina lake kamili kama alivyojiandikisha Nida,” alisema akiongezakwamba anawajua baadhi ya watu wanaomiliki zaidi ya nyumba moja kwa majina tofauti na wengine wanaozitumia kuzikodisha huku wakiwa kwenye majengo mengine.

“Wote watambuliwe, najua kuna vishoka ambao wanaowatumia kuzikodisha; mfanye uhakiki upya wa kielektroniki. Wakati wa uhakiki hakikisheni maofisa na mameneja wa Mkoa wa Dar es Salaam wanaondolewa na kuwekwa watu wengine,” alisema na kuongeza kwamba nyumba za shirika hazitolewi kwa familia kama urithi baada ya aliyepangishwa kufariki, bali waliobaki hutakiwa kwenda NHC kwa ajili ya kuomba upangaji mpya.

Comments are closed.