The House of Favourite Newspapers

WEMA AANDIKA HISTORIA

Wema Isaac Sepetu

 KUFUATIA maandalizi baab’kubwa ya shughuli yake ya kukata na shoka ya kuzaliwa (birthday), staa grade one Bongo, Wema Isaac Sepetu ameandika historia, Ijumaa limeelezwa.  

 

Wema ambaye ni mkali wa sinema za Kibongo, inasemekana ameandaa sherehe hiyo ya kufa mtu ambayo itafanyika leo katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar.

Inakadiriwa kuwa maandalizi yake yamegharimu mamilioni ya shilingi. Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika, Wema alikuwa anasubiria atimize umri wa miaka 30 ndipo afanye shughuli kubwa.

 

Ilielezwa kuwa, pati hiyo imeambatana na uzinduzi wa vitega uchumi kadhaa vya Wema kama sinema ambayo amefanya na mwigizaji mkubwa barani Afrika kutoka nchini Ghana, Van Vicker ambaye naye amemshusha Bongo kwa ajili ya uzinduzi huo.

“Hivi mnakumbuka Wema zamani alivyokuwa anafanya pati kubwa kwenye birthday zake? Imepita kama miaka miwili sasa, hajafanya pati kubwa kwenye birthday zake, alikuwa amepanga kuifanya mwaka huu ambapo ndiyo atakuwa anatimiza miaka 30, tena alikuwa amepania hasa maana atafanya uzinduzi pia wa sinema yake ile aliyocheza na Van Vicker.

 

“Kifupi ni shughuli bab’kubwa itakayoandika historia mpya kwenye maisha ya Wema,” alisema mmoja wa timu yake ambaye hakutaka jina litajwe gazetini. Ilifahamika kwamba mbali na uzinduzi wa sinema hiyo, pia atatumia shughuli hiyo kuzindua duka lake kubwa lililomgharimu mamilioni lililopo Kinondoni jijini Dar.

Kufuatia uzinduzi wa vitega uchumi hivyo na shughuli hiyo ya kukata na shoka, mashabiki wa Wema wamekuwa wakifurahishwa na jambo hilo kwani anakuwa amemziba mdomo hasimu wake, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ ambaye ni mzazi mwenza wa msanii Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ aliyewahi kuwa mwandani wa Wema. Baada ya kulambishwa ubuyu huo mtamu wa mjini, Ijumaa lilimtafuta meneja wa Wema ambaye alizungumza kwa niaba yake.

 

Akizungumza na Ijumaa, meneja wa Wema, Neema Ndepanya kuhusu gharama za shughuli hiyo na miradi mipya, mbali na kukiri kutumia mamilioni alisema hana kiasi kamili cha mamilioni yaliyotumika kuandaa shughuli hiyo. Alisema kuwa ni pesa nyingi zilizotumika kuandaa shughuli hiyo kwa sababu kulisha watu zaidi ya 600 siyo mchezo.

 

“Unajua sisi pale tunaenda kufanya kazi, hatuendi kuharibu pesa kwa sababu ya birthday peke yake na siku hizi Wema hafanyi kitu cha kupoteza tu pesa kama zamani. “Sasa hivi ukiona Wema anafanya kitu maana yake hata akigharamia anaingiza pesa siyo kama zamani.Image result for van vicker

“Zamani Wema alikuwa anapoteza pesa bila sababu, kwa hiyo sisi pale Mlimani City ni kwa ajili ya kufanya kazi, kuzindua sinema aliyofanya na Van Vicker na vitu vingine vikubwa sana ambavyo hata watu wakiviona watamkubali.

 

“Pesa zitakazotumika siyo ndogo ni pesa nyingi kwa sababu unajua mtu kulipia ukumbi, kulipia bendi ‘live’, kugharamia chakula na vinywaji ili kila atayeingia ale na kunywa kwa zaidi ya watu 600, hiyo haiwezi kulingana na kiingilio cha shilingi 50,000, wewe mwenyewe unajua, huwezi kula wala kunywa ukatosheka kwa hiyo 50,000 kwa sababu ni self-service, kila mtu anajipakulia anachokitaka na bado wataona uzinduzi wa sinema. Kwa hiyo ni bajeti kubwa tu ya kutosha,” alisema Neema.

Comments are closed.