The House of Favourite Newspapers

Yanga Yamfuata Kipa wa TP Mazembe

RASMI Kamati ya Usajili ya Yanga inayoongozwa na Abbas Tarimba imemfuata kipa wa TP Mazembe, Vumi Ley Matampi kwa ajili ya kukamilisha usajili wa kipa huyo.

Yanga ilikuwa na tatizo kubwa golini msimu uliopita kutokana na Mcameroon, Youthe Rostand kushindwa kukidhi matarajio Jangwani.

 

Yanga imetangaza kumfuata kipa huyo baada ya Mazembe kutangaza kutokuwa na mipango naye kwenye msimu ujao kutokana na mkataba wake na timu hiyo kumalizika.

Kipa huyo alipendekezwa kusajiliwa Yanga na kocha mpya wa timu hiyo mwenye asili ya DR Congo, Zahera Mwinyi ikiwa ni siku chache tangu aanze kibarua cha  kukinoa kikosi hicho.

Kamati mpya ya Yanga ikiwa na matajiri kibao wakiwemo Tarimba mwenyewe na Abdallah Bin Kleb, na inaonekana inataka kushindana na jeuri ya fedha za Mohamed Dewji ‘Mo’ pale Msimbazi.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, mjumbe wa kamati hiyo, ambayo pia inatambulika kama Kamati Maalum ya Kuivusha Yanga katika Kipindi cha Mpito, Hussein Nyika alisema ni wakati sahihi wa wao kumfuata kipa huyo kwa ajili ya mazungumzo ya kumsajili baada ya klabu yake kutangaza kutokuwa na mpango naye.

Nyika alisema, haraka watakamilisha usajili wa kipa huyo baada ya kamati ya usajili kukutana mwanzoni mwa wiki hii katika kuhakikisha wanakisuka kikosi kitakachokuwa imara na kuleta ushindani.

Aliongeza kuwa, wanataka kumsajili kipa huyo kwa ajili ya kumpa changamoto kipa wao Mcameroon, Youthe Rostand ambaye ni kipa namba moja katika kikosi hicho.

 

“Ni nafasi yetu muafaka Yanga kuanza mipango ya kukamilisha usajili wa kipa wa Mazembe ambaye ni Matampi, ni baada ya klabu yake kutangaza kutokuwa na mipango naye katika msimu ujao.

“Hivyo, hizo taarifa tumezipata, kwetu tunaona zimetupa nguvu ya kumfuata kipa huyo rasmi kwa ajili ya kukamilisha usajili wake.

“Kamati yetu imepanga kukutana mwanzoni mwa wiki hii, hivyo ni matarajio yangu mazuri kuona tunakamilisha usajili huo wa kipa huyo na kikubwa tunafanya usajili wetu kutokana na mapendekezo ya kocha wetu aliyoyatoa kwenye kamati ya usajili,” alisema Nyika.

 Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Comments are closed.