The House of Favourite Newspapers

Zahera Abakisha saa 24 Yanga

Kocha wa Yanga Mkongomani, Mwinyi Zahera.

MCHEZO wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids FC ya nchini Misri umezuia kikao cha Kamati ya Utendaji ya Yanga kilichotarajiwa kikae juzi kujadili hatma ya kocha wao Mkongomani, Mwinyi Zahera.

 

Hiyo, ikiwa ni siku chache tangu mashabiki wa timu hiyo waushinikize uongozi wamtimue kocha huyo kutokana na matokeo mabaya waliyoyapata ya kufungwa mabao 2-1 na Pyramids katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa kwenye Uwanja CCM Kirumba, Mwanza.

 

Wakati mashabiki wakishinikiza kutimuliwa kwa kocha huyo, tayari baadhi ya makocha wanatajwa kuja kuchukua nafasi yake, kati ya hao ni kocha wa zamani wa Yanga, Mholanzi Hans Pluijm aliyeipa mataji mawili ya Ligi Kuu Bara.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, ndani ya Kamati ya Utendaji na Ufundi ya Yanga, ni ngumu kwao kuchukua maamuzi ya kusitisha mkataba wa Zahera hivi sasa wakiwa wanakabiliwa na mchezo mgumu mbele yao dhidi ya Pyramids.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa hatima ya Zahera itajulikana baada ya kumalizika kwa mchezo huo utakaochezwa keshokutwa Jumapili zikiwa zimebaki saa 24 wakijiandaa na mchezo huo ambao timu hiyo inahitaji ushindi wa mabao 2-0 ili wafuzu makundi.

 

Aliongeza kuwa mara baada ya mchezo huo wa Pyramids, haraka Kamati ya Utendaji na Ufundi ya Yanga itakutana na kocha huyo na kuomba ripoti nzima ya michuano hiyo mikubwa, pia Ligi Kuu Bara.

 

“Tunafahamu makocha wengi wanatajwa kuja kuchukua nafasi ya Zahera akiwemo Pluijm, lakini ukweli ni kwamba haitawezekana kwa sasa kumleta kocha mpya wakati hakuna mipango yoyote iliyofanyika katika kumleta mbadala wake,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Upande wa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela alipoulizwa alisema: “Ni mapema kulizungumzia hilo.”

Stori na Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Comments are closed.