The House of Favourite Newspapers

Zahera Ataja Siri ya Kuwapiga Township Rollers

KOCHA Mkuu wa Yanga Mkongomani, Mwinyi Zahera ametaja siri tatu za kuwaondoa wapinzani wao, Township Rollers ya nchini Botswana kwa kuwafunga bao 1-0, juzi Jumamosi.

 

Timu hizo zilivaana katika mchezo wa Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Botswana huku bao la Yanga likifungwa na Mganda, Juma Balinya.

 

Yanga mara baada ya kufanikiwa kufuzu hatua inayofuata, inatarajiwa kuvaana na Zesco ya nchini Zambia inayofundishwa na kocha wa zamani wa timu hiyo, George Lwandamina.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Zahera alisema kuwa siri ya kwanza ilikuwa ni kupata bao la kuwatangulia wapinzani wao litakalokuwa la mapema na lengo ni kuwapa presha wapinzani wao hao.

 

Zahera alisema kuwa michuano hiyo ni mikubwa, hivyo lazima wachezaji wacheze kwa kutumia akili na mbinu kwa lengo la kuwazuia wapinzani wasitawale mpira.

 

“Michuano kama hii ni mikubwa, wachezaji wanapaswa kucheza kwa kutumia akili na mbinu nyingi ili ufanikwe kupata ushindi hasa ukiwa ugenini.

 

“Kabla ya mchezo huu, niliwaambia mchezo wa leo (juzi) tunapaswa kufunga bao maana bila kufunga tutatolewa na huo utakuwa mwisho wetu wa michuano hii mikubwa Afrika.

 

“Hivyo, ili tufanikiwe kuendelea hatua inayofuata ni lazima tupate bao la mapema zaidi ili kuwapa presha wapinzani wetu.

 

“Mbinu hizo zilitusaidia kwani, wapinzani wetu walilazimika kushambulia kwa tamaa baada ya sisi kupata bao hilo, uliona walicheza kwa tamaa kubwa ya kushambulia ili warudishe bao hilo kwa haraka.

 

“Walipokuwa wanashambulia walikutana na wachezaji tisa wakizuia golini kwetu, hivyo tuliwapa nafasi watushambulie kwa maana walihitaji kurudisha bao lakini tulikuwa makini mno kuwazuia wasifunge,” alisema Zahera.

 

Zahera Kuhusu Simba Vs UD Songo “Sijui Walivyocheza” – Video

Comments are closed.