The House of Favourite Newspapers

AKILI ZA KICHAGA NDANI YA KICHWA CHA UWOYA

MACHO yake yanaweza kukubabaisha kwa jinsi yalivyo mazuri, ukamchukulia poa. Mwonekano wake wa kipekee, umbo la kike la kuvutia vinaweza kukuhadaa kuwa ni mrembo anayetegemea kuletewa!  Hayupo hivyo. Ni mpambanaji wa nguvu. Ana akili za Kichagga! Nani hawafahamu Wachagga kutoka mkoani Kilimanjaro? Sifa yao kuu ni kupambana hadi kufanikiwa.

Ni watu ambao wanasifika kwa biashara na wametapakaa katika mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi. Ukiwa jijini Dar na mikoa ya jirani, ukienda dukani, hata kama mwenye duka siyo Mchagga, utasema unakwenda dukani kwa Mangi.

Ni watafutaji. Wapo popote ilipo biashara. Ingekuwa tunazungumzia kwa levo ya duniani, tungesema ni Wahindi. Hawa wapo kila nchi wakifanya biashara. Yes! Namzungumzia diva wa Bongo Muvi, Irene Uwoya, mama wa mtoto mmoja wa kiume – Krish. Kwa muda mrefu amekuwa akifanya filamu, huku akiendelea kuhifadhi heshima yake katika kiwanda hicho.

Kazi zake zinadhihirisha ubora wake. Kama unabisha tafuta Oprah, Offside au Dj Ben, utajua nazungumzia nini. Uwoya anajua. Ameweza kupenya katikati ya mastaa kama Yvone Cherry ‘Monalisa’, Blandina Chagula ‘Johari’, Jenifer Kyaka ‘Odama’ na wengine wengi. Filamu ya Diversion of Love ndiyo iliyomtambulisha. Wakati huo akitokea Miss Tanzania mwaka 2006 akishika nafasi ya tano.

Ilikuwa kosa director kumruhusu asimame mbele ya kamera. Aliposema, “action” akaua na kutoboa jumla. Mpaka sasa Uwoya yupo juu na inaelezwa kuwa anakunja mpunga mrefu kwenye kiwanda cha filamu. Ni kati ya waigizaji wa kike wenye mvuto na wanaogombewa kushiriki filamu nyingi. Kwa sababu hiyo, Uwoya angeweza kuridhika, kuwa sanaa inatosha. Pengine uzuri wake unamtosha. Lakini wapi. Siyo kwa mtoto wa Kichagga.

Amejiongeza na kufungua kiwanja maridadi cha maraha, kilichopo pande wa Sinza, Mori jijini Dar es Salaam. Kinakwenda kwa jina la Last Minute Lounge. Ni hatari kile kiwanja. Watu kama wote. Mastaa ndiyo usiseme. Watu wanaangamiza fedha kupunguza stresi za kugombania mwendokasi! Mwandishi wetu alifika katika Pub hiyo na kufanya mahojiano na staa huyo, ambaye alifunguka kuhusiana na biashara yake hiyo.

Risasi Jumamosi: Hongera sana Uwoya. Mh! Pazuri sana.

Uwoya: Asante sana, namshukuru Mungu kwa hilo.

Risasi Jumamosi: Mwanzoni ulikuwa na Pub ndogo hapa hapa, sasa umeamua kufungua kubwa zaidi, iliyoboreshwa na yenye nafasi zaidi. Vipi, ulipata faida kubwa zaidi au uhitaji wa wateja ulikuwa mkubwa zaidi?

Uwoya: Kiukweli niseme ni wazo nililokuwa nalo muda mrefu, ilikuwa ni suala la muda tu. Ingawa ni kweli nafasi yangu awali ilikuwa ndogo na wateja walikuwa wengi. Vyote vikanisukuma kuharakisha wazo langu.

Risasi Jumamosi: Biashara hii inahitaji uwepo muda mwingi, vipi sasa kuhusu filamu au umeacha?

Uwoya: Ni kweli nakuwepo hapa muda mwingi, lakini hiyo hainiharibii kazi yangu. Ikitokea nafanya.

Risasi Jumamosi: Pub yako inaonekana ni ya kisasa, umetumia kiasi gani kuitengeneza na kuonekana pa kisasa kiasi hiki?

Uwoya: Siwezi kusema nimetumia fedha kiasi gani, ila ni nyingi na vitu vyangu vingi nimevinunua nje ya nchi.

Risasi Jumamosi: Wateja wako wengi ni kina nani?

Uwoya: Ni watu mchanganyiko, maarufu na wasio maarufu.

Risasi Jumamosi: Vipi wasanii wenzako wanakuunga mkono?

Uwoya: Wasanii wenzangu kwa kweli wananipa sapoti sana, nawashukuru sana.

Risasi Jumamosi: Wateja wengi wanaokuja hapa, wanatamani kukuona. Je, huwa unakuwepo hapa siku zote?

Uwoya: Ndiyo! Hata kama mtu akitaka nimhudumie mimi, huwa nafanya hivyo.

Risasi Jumamosi: Kwa nini umeamua kufungua Pub na kuacha biashara nyingine zote?

Uwoya: Sio mara ya kwanza kufungua biashara, nilishawahi kufungua duka la nguo na vitu vingine vingi lakini ndoto yangu kubwa ilikuwa kufanya hivi. Nafurahi kuona ndoto yangu imetimia.

Risasi Jumamosi: Kabla ya kufungua rasmi hapa, ulifanya usaili kwa wafanyakazi. Kwa nini ulifanya hivyo, wakati wengine huwa wanachukua watu mitaani bila masharti yoyote?

Uwoya: Nilitaka kufanya kitu kizuri chenye hadhi na kuthaminika. Unajua wengi wanapenda kuwadharau wahudumu, kitu ambacho mimi nimekipinga kabisa. Nimewachuja wanaonifaa na kweli nilionao wanajielewa na wanafanya kazi yao vizuri.

Risasi Jumamosi: Ok! Irene, asante sana kwa ushirikiano.

Uwoya: Nawe asante pia kwa kujali, karibu tena.

MAKALA: Imelda Mtema

Comments are closed.