The House of Favourite Newspapers

Majipu yakaa mkao wa kutumbuliwa

0

MagufuliMwandishi wetu, Risasi Jumamosi

DODOMA: Huku leo Rais Dk John Magufuli akitarajiwa kukabidhiwa Uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka kwa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, viongozi na makada wenye makandokando, maarufu kama majipu wamekaa mkao wa kutumbuliwa wakati wowote.

Habari kutoka kwa wajumbe ambao tayari wameshawasili mjini hapa, wanasema baadhi ya viongozi ndani ya chama hicho wana kashfa ya kuhodhi ardhi na mashamba kwa kutumia nafasi zao, kitu kinachowapa hofu kuwa mara tu baada ya Magufuli kuchukua nafasi hiyo, watakuwa wa kwanza kuondolewa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Ukiangalia viongozi hawa wamekuwa wafujaji wakubwa wa mali za chama, miradi mingi wameigeuza kuwa yao, wametumia ofisi za chama kupiga dili chafu, sasa mtu kama Magufuli ambaye hataki mchezo na hacheki na watu wajanjawajanja, wana hofu kubwa sana,” alisema mjumbe mmoja kutoka mikoa ya Kaskazini.

“Baadhi ya viongozi wa CCM wamefanya ubadhirifu mkubwa katika miradi ya chama, wametumia maeneo yake kwa manufaa yao, utakuta ofisi imepangishwa wafanyabiashara mbalimbali, lakini fedha hazieleweki zinakwenda wapi, wakati mwingine wanafanya biashara zao kwenye majengo ya chama bila kulipia kodi, kwa moto huu wa JPM, sidhani kama watapona hawa watu,” alisema mjumbe mwingine wa Dodoma.

Mji wa Dodoma umekuwa na wageni wengi wanaotokana na mkutano huo, wakiwemo wajumbe, wageni waalikwa, watendaji wa taasisi mbalimbali za kitaifa ambao wanahusika kwa namna moja au nyingine na mkutano huo ambao msingi wake mkubwa ni kung’atuka kwa Mwenyekiti Kikwete na kukabidhiwa kwa Magufuli.

Leave A Reply