The House of Favourite Newspapers

Maneno ya Conte Kuhusu Kuwakejeli Man United

_92062085_chelseaMeneja wa klabu ya Chelsea ya Uingereza Antonio Conte amesema hakuwa anakusudia “kumkejeli yeyote” baada yake kuonekana akitaka kumkeresha zaidi Jose Mourinho baada ya Chelsea kulaza Manchester United 4-0 Jumapili.

Conte aliwahimiza mashabiki wa Blues kupiga kelele zaidi kuunga timu yake mkono dakika za mwisho za mechi.

Taarifa zinasema kwamba Mourinho alimwambia mkufunzi huyo kutoka Italia kwamba vitendo vyake “viliiaibisha” United.

Lakini Conte amesema: “Nimekuwa mchezaji pia na najua ninafaa kufanya nini.

“Huwa daima namuonesha heshima yeyote, ikiwemo Manchester United.”

Mabao ya Pedro, Gary Cahill, Eden Hazard na N’Golo Kante yalivuruga safari ya kwanza ya Mourinho Chelsea tangu afute Desemba mwaka jana kutokana na matokeo mabaya.

Mourinho, 53, alikaribishwa vyema na mashabiki Stamford Bridge, lakini mambo hayakumuendea vyema kwenye mechi.

Conte, 47, amesema aliwahimiza mashabiki wa nyumbani wapige kelele zaidi kwa sababu anasema alikuwa anawasikia mashabiki wa United pekee.

Taarifa kwenye vyombo vya habari Italia zinasema Mourinho alimwambia Conte: “Huwa husherehekei hivyo mambo yakiwa 4-0, unaweza ukafanya hivyo mambo yakiwa 1-0, vinginevyo unatuaibisha.”

Mameneja wote wawili walikataa kusema walinong’onezana nini.

“Hakukuwa na kisa, lilikuwa tu jambo la kawaida kwangu. Sikuwa namkejeli yeyote. Siwezi kufanya hivyo,” amesema Conte.

“Leo ilikuwa sawa kuwahimiza mashabiki wangu nilipokuwa nasikia kelele za mashabiki wa Manchester United pekee mambo yakiwa 4-0.

“Wachezaji, baada ya kushinda 4-0, walihitaji kushangiliwa. Ni kawaida.”

“Iwapo tunataka kupunguza hisia, basi tunaweza kwenda nyumbani na kutafuta kazi nyingine.”

Kipigo hicho kutoka kwa Chelsea kilikuwa kibaya zaidi kupokezwa United Ligi ya Premia tangu walipolazwa 6-1 na Manchester City Oktoba 2011.

Aidha, kilikuwa kipigo kikubwa zaidi kwa Mourinho mashindano yote tangu alipolazwa 5-0 na Barcelona alipokuwa Real Madrid Novemba 2010.

Mourinho amewaomba radhi mashabiki wa Manchester United kote duniani.

“Kama kiongozi naomba radhi, na jambo pekee ninaweza kusema ni kwamba mimi ni 100% Man Utd, na si 99% Man Utd 1% Chelsea.”

Comments are closed.