The House of Favourite Newspapers

Serikali isiingilie ndoa za watu

0

AlhadiMussaSalum (1)Toleo lililopita tulisoma ufafanuzi makini wa Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Alhadi Musa Salum kuhusu mambo mbalimbali ya Kiislamu na jamii kwa ujumla, katika sehemu hii ya pili ya mahojiano yetu atajibu kuhusu pikipiki (bodaboda) kwamba mwanamke aliyefunga na kumkumbatia dereva, je ni dhambi? Je ni sahihi mtu kubadili dini kwa malengo fulani na kadhalika. Ungana nasi katika mahojiano haya yaliyofanyika hivi karibuni ofisini kwake:

Kuna kawaida ya Waislamu kutokaribiana kati ya wanawake na wanaume hasa wakati wa kuswali au mikusanyiko, unashauri nini tabia ya wanawake kupanda bodaboda au pikipiki na kuwakumbatia madereva wa usafiri huo hasa kipindi hiki cha Mfungo Mtukufu wa Ramadhani?

Jibu: Kukaribiana wanawake na wanaume hakukatazwi hasa kama ni wakati wa kusafiri. Watu wa jinsia hizo  kukaribiana kwenye madaladala, au mabasi na hata kwenye pikipiki kwa sababu ya safari siyo tatizo kwani hiyo ni dharura, hivyo hata wakigusana, hawaharibu funga yao kwani  hata Waislamu wanapokwenda Hija Maka wanagusana. Kubwa linalotakiwa kuzingatiwa ni dhamira, kama umedhamiria kuwa unasafiri kwa njia ya bodaboda na usiwe na jambo la haramu la kutenda, funga yako si haramu. Uzuri ni kwamba Mungu anajua nia yako hiyo ya kusafiri na bodaboda, kama una nia mbaya atajua tu.

Siku hizi kuna tabia ya watu hasa wasanii kubadili dini kwa nia ya kuoa au kuolewa na baadaye kurudi katika dini zao za awali na wengine wamediriki kufanya hivyo mara nyingi. Unazungumziaje tabia hiyo?

Jibu: Wanaofanya hivyo wanafanya jambo la hatari sana, huko ni kumkufuru Mungu. Niseme tu kwamba, wanaofanya hivyo  wanamchezea Mungu na hakika mwisho wao huwa ni mbaya na katika Uislamu hukumu yake huwa nzito. Anayechezea dini ya Mwenyezi Mungu ana hatari sana. Niwaombe wasanii na wengine wenye tabia hiyo, wasifanye hivyo.

Wapo baadhi ya Waislamu au hata wasio Waislamu huamua kufunga ndoa na wapenzi wao kwa wakuu wa wilaya au ndoa za kimila. Je, hii ni halali?

Jibu:Kwanza kidini kufunga ndoa kwa mkuu wa wilaya siyo halali. Niwaambie tu wakuu wa wilaya kuwa mambo kuhusu ndoa ni mambo ya kidini, wanatuingilia sisi viongozi wa dini shughuli ambayo haiwahusu. Kwa hiyo kufunga ndoa bomani siyo sawa hata kidogo.

Dini zetu zote zimetuelekeza jinsi ya kuoana na ndiyo maana kama kuna Wakrito wamefunga ndoa Kikristo na wote wakaamua kusilimu na kuingia Uislamu, hatuwafungishi tena ndoa.

Na Muislamu anaruhusiwa kufunga ndoa na asiye Muislamu kama alikuwa anaamini katika Injili na wala hasilimishwi. Narudia watu waache kufunga ndoa kwa DC (District Commissioner yaani mkuu wa wilaya) na wakuu wa wilaya au serikali iache kuingilia ndoa za watu wa dini zote.

Mara nyingi kwenye mikutano au mabaraza ya Kiislamu hasa mabaraza ya Iddi au Maulidi wanaalikwa viongozi ambao siyo Waislamu kuhudhuria na pengine kuhutubia, wape elimu wasomaji wetu, kwa nini huwa hivi?

Jibu:  Uislamu unakiri uwepo wao viongozi wa serikali bila kujali dini zao na unakiri mamlaka za serikali chini. Hivyo tunawaalika viongozi hao wa dola katika mabaraza hayo na wanashiriki kwenye Baraza la Iddi au Maulidi na kuhutubia lakini hawashiriki ibada za moja kwa moja.

Tunakushukuru sana kwa ushirikiano wako na karibu ofisini kwetu.

Jibu: Ahsante sana nitakuja siku yoyote na Mungu awabariki wote.

Leave A Reply