The House of Favourite Newspapers

Tambwe: Huyu Kichuya ni Hatari Aisee

Amissi-Tambwe

KASI ya kuzifumania nyavu ya winga wa Simba, Shiza Kichuya aliyonayo sasa katika Ligi Kuu Bara, imempagawisha mshambuliaji wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe (pichani juu) ambaye amekiri kuwa jamaa anatisha.

Tambwe amedai kuwa kwa sasa Kichuya yupo vizuri lakini anatakiwa kuwa makini kuhakikisha analinda kiwango chake hicho kwa kuzingatia misingi na maadili ya soka.
Hivi sasa Kichuya ndiye gumzo la mtaa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuzifumania nyavu ambao amekuwa akiuonyesha uwanjani tangu alipojiunga na Simba akitokea Mtibwa Sugar.
Kichuya anayetumia mguu wa kushoto, ndiye kinara kwenye chati ya ufungaji, akiwa na mabao saba aliyoyafunga kwenye mechi tisa alizoitumikia Simba.
Nafasi ya pili inashikiliwa na Omary Mponda wa Ndanda FC akiwa na mabao matano wakati Tambwe ambaye msimu uliopita ndiye aliyekuwa mfungaji bora anashika nafasi ya tatu akiwa na mabao manne.

kichuya

Shiza Kichuya.

Akizungumza na Championi Jumatano, Tambwe alisema Kichuya yupo vizuri na ni msaada mkubwa kwa timu yake ya Simba hivyo kama hatabadilika anaamini anaweza kufanya maajabu msimu huu.
“Asibweteke na sifa kwa mafanikio hayo machache aliyoyapata hivi sasa kama anataka kudumu.
“Kazi anayoifanya uwanjani ninaona, yupo vizuri kwa sasa kama ataongeza juhudi zaidi mazoezini na kuzingatia miiko na maadili ya soka atapata mafanikio zaidi.
“Kuhusu kuibuka mfungaji bora msimu huu hilo siwezi kutabiri kwa sababu ligi bado mbichi na kuna wachezaji wengi ambao wanafanya vizuri kama yeye lakini ukweli ni mchezaji hatari,” alisema Tambwe ambaye ni shabiki mkubwa wa Liverpool na Barcelona.

Na Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam

Comments are closed.