The House of Favourite Newspapers

Wakili Hashim Rungwe Aishauri Serikali Mambo Mazito

0

rungwe

Wakili Hashim Spunda.

*Azungumzia mbinu ya kupunguza bei ya sukari, asema watu wana njaa!

MMOJA wa wagombea Urais na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Umma (Chauma), Wakili Hashim Spunda Rungwe amefanya mahojiano maalum na wahariri wetu ili kutoa tathmini yake ya utawala wa miezi sita wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Pombe Magufuli tangu ashike madaraka ya kuongoza nchi. Wakili Rungwe ameshauri mambo mazito ya nini cha kufanya ili nchi iweze kusonga mbele kimaendeleo. Hata hivyo, ametoa maoni juu ya mjadala wa Bunge kutooneshwa laivu na sakata la sukari, fuatana nasi katika makala haya ujue kile alichokisema:

Tupe maoni yako kuhusu utawala wa Rais Dk. John Pombe Magufuli ambaye amefikisha miezi sita akiwa madarakani, je, anakwenda vizuri?

Rungwe: Miezi sita ya Serikali ya Awamu ya Tano sijasikia mpango wowote wa kuondoa njaa kwa wananchi. Lazima rais ajue kwamba watu wana njaa na zifanyike juhudi kuhakikisha kipato kwa mwananchi mmojammoja kinaongezeka badala ya kupungua na bei ya vyakula inapungua. Maana yake ni kwamba vyakula vipungue bei badala ya kuongezeka. Kwa mfano, sukari ilikuwa Sh. 1,800 sasa ni zaidi ya Sh. 3,000 kwa kilo. Hili ni tatizo. Nitoe ushauri wa bure kwa Rais Magufuli, asihubiri ubaya wa baadhi ya watu hadharani kwa sababu kunaweza kuwafanya wawekezaji kuogopa kuja kuwekeza nchini.

Yapo mambo ambayo anapaswa kuongea na watendaji wake tu na mambo yakaenda bila kuwafanya watu wa nje kujua kuwa Tanzania ni nchi ambayo unaweza kunyang’anywa mali yako bila kufuata utaratibu wa kisheria. Huu ni ushauri tu, nimeutoa kwa faida ya nchi.

Nini maoni yako kuhusu Bunge kutorushwa laivu?

Rungwe: Kwanza ieleweke kuwa kuzuia Bunge kuoneshwa laivu ni ukandamizaji mkubwa wa vyombo vya habari lakini pia ni kuwanyima wananchi kuwaona wabunge wao wanavyojadiliana juu ya maisha yao. Tusifuatishe nchi nyingine, kama sisi tuliamua kufanya hivyo na wananchi wakaona inafaa, kuna ubaya gani nchi za nje zikituiga sisi? Kwa maneno mengine kutoonesha bunge laivu tunaweza kusema huu ni utemi wa wazi. Hakuna sababu yoyote ya msingi ya kuwanyima wananchi haki yao ya kumuona mbunge wao akitoa hoja zao kwani ndivyo katiba ya nchi yetu inavyosema tofauti na katiba nyingine.

Katika miezi sita hii tumeshuhudia watumishi wa sekta za umma wakitumbuliwa majibu, je, una maoni gani kuhusiana na zoezi hilo?

Rungwe: Mimi kama wakili nashauri viongozi wa serikali wa ngazi zote wasifukuze wafanyakazi hovyohovyo bila kuwasikiliza. Kufanya hivyo ni ukiukaji wa sheria, kwani katika sheria tunaambiwa usihukumu kwa kusikiliza hoja za upande mmoja. Usimhukumu unayemuona muovu kwa kufanya uovu. Ushauri wangu ni kwamba wanaosimamishwa wote, wasikilizwe, huo ndiyo utawala wa kisheria.

Ndani ya miezi sita kuna changamoto nyingi katika serikali, kuhusu sekta ya elimu kuna uhaba wa madarasa na madawati, unasemaje kuhusu hilo?

Rungwe: Ili kumaliza changamoto hiyo niseme tu kwamba serikali iache matumizi makubwa kama vile viongozi kujinunulia magari ya kifahari, fenicha mpya, kujilipa posho nono na kuwasaidia watu kukwepa kodi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, badala yake wajenge nchi kwa kufanya kazi kwa bidiii na kwa kusaidiana na wananchi wenye nia njema kuchangia maendeleo, matatizo hayo yatakwisha.

Hivi sasa kuna tatizo kubwa la mfumuko wa bei ya vyakula, unadhani serikali ifanye nini kuondoa kabisa tatizo hilo?

Rungwe: Serikali isitafute mchawi, mchawi ni yenyewe kutokana na mfumo uliokuwepo tangu zamani. Marais waliopita ni watu wa timu yake Rais Magufuli na nisiwatetee, hao wamesababisha haya. Tulikuwa na mashirika ya umma mengi kama vile Bhesco, RTC, Hosco, NBC na kadhalika lakini mengi yamekufa kutokana na kuwekwa watu kuongoza wasio na uzoefu.

Mfumuko wa bei upo, kwa mfano, hili la sukari ni tatizo kubwa kwa sababu hivi sasa kikombe cha chai ya rangi kwa mama ntilie ni shilingi 500 badala ya shilingi 200. Hii utaona kuwa haijamsaidia mlalahoi, watu wana njaa, serikali itafute mbinu ya kuondoa adha kama hii. Bei ya Dizel, ipungue kila kitu kitapungua bei kwa sababu vyakula vinasafirishwa kutoka shambani kwa gharama kubwa.

Sukari ya nje imezuiliwa kuingia nchini nini ushauri wako?

Rungwe: Mimi ningekuwa mshauri wa rais, ningemshauri asizuie kuagizwa sukari kutoka nje badala yake ningeshauri waitoze ushuru mkubwa na hii inayozalishwa nchini ikaondolewa ushuru. Kwani kuna hasara gani kuondoa ushuru kwa commodity (bidhaa) moja? Ni wazi watu wangekimbilia sukari ya bei nafuu.

KUNUNUA NA KUSOMA MAGAZETI YA GLOBAL PUBLISHERS ONLINE, INGIA HAPA==>VODACOM M-PAPER APP

*********

JIUNGE NA SOCIAL MEDIA ZETU

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

ERIC SHIGONGO INSTAGRAM: @ericshigongo

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: Global TV Online

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE:@shigongotz

Leave A Reply