The House of Favourite Newspapers

Unatamani Uhusiano wa Wenzako, Wako Majanga? Soma Hapa!


VUTA picha ni watu wangapi sasa hivi hawafurahii uhusiano wao. Wanatamani uhusiano wa wengine kwa jinsi wanavyoutazama, wengi sana wapo hivyo na wao wenyewe hawajijui kama wapo hivyo. Utasikia;

“Jamani natamani na mimi mtu wangu angekuwa ananijali kama vile fulani anavyomjali mtu wake. Fulani bwana anajua kupenda. Anamdekeza kwelikweli mpenzi wake. Natamani ningekuwa mimi nadekezwa kiasi kile. Mpenzi wake hapendi kumuona mwenzi wake hana furaha.

“Anamfurahisha muda wote. Anamsikiliza mwenzi wake, anamsahauri. Hamfokeifokei mbele za watu. Wanasikilizana hadi raha. Ni nadra sana kusikia wemegombana. Ikitokea wamegombana, hawachukui muda mrefu kupatana.

“Ni muda mfupi tu wanakuwa na furaha kama zamani. Mara nyingi wao kila siku ni sherehe, wana amani. Maisha yao ni furaha tele. Kama ni viwanja vya starehe wanaenda pamoja. Kila mmoja anajivunia kuwa na mwenzake.

“Wana maisha ya kawaida lakini wanajivunia. Sijui kwa nini mimi kila siku matatizo. Sijui lini nitampata mtu sahihi kama mwenzangu. Ili na mimi nipate angalau pumziko la moyo, kila siku ni mateso hadi najuta kupenda.”

KUNA KITU CHA KUJIFUNZA

Kwanza marafiki zangu mnapaswa kujua, kutamani uhusiano wa wenzako ni kosa kubwa ambalo watu wengi wanafanya. Wanashindwa kujua kwamba kila mwanadamu ana upungufu wake. Unaweza ukawa unatamani uhusiano

wa mwenzako, kumbe mwenzako naye anatamani uhusiano wako. Yawezekana ana matatizo lukuki. Angekusimulia, ungeona yako yana nafuu.

Kila mtu ana mapungufu yake hivyo si sahihi sana kuamini mwenzako amekamilika. Yawezekana nje akawa anajionesha hivyo kumbe nyumbani kwake kunawaka moto. Ugomvi mtindo mmoja, hakulaliki. ISHINI MAISHA YENU Mnapaswa kuishi maisha yenu.

Mnapaswa kujitukuza wenyewe. Kujipa thamani wenyewe, mjikubali. Mkijikubali wenyewe, wenzenu nao watawakubali nyinyi. Kila siku jisahihisheni wenyewe udhaifu wenu. Rekebisheni pale mnapoona mmekosea. Mueleze mwenzako unapoona hakutendei haki na usithubutu kumwambia kwa kumlinganisha na watu wengine.

Wao ni wao na nyinyi mbaki kuwa nyinyi. Mtakapofanikiwa kujitengenezea heshima, watu nao wataanza kuwaheshimu. Mwanafalsafa wa China, Laozi aliwahi kusema:

“When you are content to be simply yourself and don’t compare or compete, everyone will respect you.” Akimaanishaa, kama

ukiridhika kuwa wewe ndiyo wewe, na hutaki kujilinganisha na kushindana na mtu mwingine, kila mtu atakuheshimu.

Maisha yao yanakuvutia wewe kwa sababu wao waliamua kuyatengeneza. Waliamua kuishi watakavyo na si wanavyotaka watu. Kumbe na wewe unayo nafasi ya kuishi na mwenzako kadiri mnavyotaka, kitakachofuata ni watu kuvutiwa na uhusiano wenu na kuuheshimu.

TABIA MBAYA INAONDOLEWA NA TABIA NZURI

Kama umebaini mwenzako anafanya jambo ambalo siyo zuri, usilikimbie. Hiyo ni changamoto. Hupaswi kuikimbia, unapaswa kuishughulikia.

Itazame katika mlengo chanya Kama ni wewe unakosea au mwenzako, mwisho wa siku mnapaswa kuchagua kujipa furaha, Kuamua kujipa amani ya moyo.

Kuamua kuishi maisha yenu, Kuamua kufanya mambo ya kuvutia ambayo mnaamini yatawafurahisha. Mnapaswa kubadilishana ninyi kwa ninyi kwa kuoneshana tabia nzuri. Kama mwenzi wako hakujali, muelekeze namna ya kujali bila kujilinganisha na watu fulani. Wao ni wao na ninyi mnapaswa kuwa na utambulisho wenu.

Mpende mwenzako. Mjali na yeye afanye vivyo hivyo. Usiwe sehemu ya tatizo. Mkikoseana, msiwafurahishe watu kwa ugomvi wenu. Mmoja ajishushe, amuombe msamaha na msameheane. Msishindane. Mpigania haki za binadamu maarufu duniani, Martin Luther King Jr aliwahi kusema;

“Darkness cannot drive out darkness; only light can do that. Hate cannot drive out hate; only love can do that.” Alimaanisha, chuki haindolewi kwa chuki bali chuki huondolewa kwa upendo. Kama mwenzako anapanda mbegu ya chuki, wewe panda ya upendo na amani. Hakika utaona matokeo mazuri.

Save

Comments are closed.