The House of Favourite Newspapers

Julio: Aikata, Aifunua TFF Ya Malinzi, Asema Hawajui Mpira

0
Kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.

KOCHA na mchezaji wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye kwa sasa anaendelea na shughuli zake binafsi jijini Dar es Salaam, amezungumza na Championi Ijumaa katika mahojiano maalum kuhusu mambo mbalimbali yanayoendelea nchini katika soka.

UCHAGUZI WA TFF

Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) chini ya Rais Jamal Malinzi linatarajiwa kufanya uchaguzi baadaye mwaka huu, Julio ana kitu cha kuzungumza kuelekea uchaguzi huo: “Unajua wajumbe wanaopiga kura hawatakiwi kuangalia urafiki wala maslahi binafsi, wazingatie faida ya nchi kama alivyofanya Rais John Magufuli.

“Magufuli anachojali ni uzalendo kwanza, hana muda wa kufikiria nani alifanya nini akiwa nani, yeye ni mkweli na ndiyo maana anafanya mambo mazuri mengi kwa faida ya taifa, yupo tayari kufa kwa ajili ya Watanzania, lakini k w a viongozi wetu hawa wapo tu wa naoongoza na hawajui mpira.

Rais John Magufuli.

“Sisi wachezaji wa zamani tutawapa msimamo wetu kuelekea uchaguzi huo, mfano Ali Mayay ameshatangaza nia ya kuwania urais wa TFF, tutamuunga mkono, tunataka watu wa soka waongoze soka, siyo mnatuletea watu wavaa suti kwenye soka. “Sisi watu wa mpira tunajijua, lakini kwa sasa tunanyang’anwa uhuru wetu, haki yetu, fedha zinaliwa na hakuna kilichofanyika cha maana.

Rais wa shirikisho la Mpira wa miguu nchini TFF Ndugu Jamal Malinzi.

KUHUSU TAIFA STARS YA SASA

“Binafsi siwezi kumlaumu (Salum) Mayanga, ni kocha mzuri tu, nalaumu waliomzunguka, Mayanga amesoma na ana elimu nzuri ya ukocha anajua anachokifanya ndiyo maana hata Mtibwa Sugar ilikuwa ikifanya viziri wakati akiifundisha. “Mimi nawalaumu waliomzunguka na wanaomuongoza, hawana mipango endelevu, kama unakumbuka huko nyuma kulikuwa na programu za vijana zilizotengenezwa na Sunday Kayuni lakini zikafa kwa kuwa waliziua wao.

“Kayuni alikuwa anaendesha mipango mingi mizuri, akaja akaondolewa kwa kuwa hawakumtaka, yule ni mtu wa misimamo na hana utani. “Unakuja kumpa mtu ukurugenzi wa ufundi ambaye hana hata mipango endelevu, yupo kwa roho mbaya tu, anawaweka watu anaotaka yeye kwa maslahi binafsi.

“Ukiwauliza wanachokifanya cha maana, eti utasikia wanasema wameleta kozi nyingi, kozi nyingi zipi ambazo zinatoa walimu wanaoweka vyeti ukutani, ndiyo maana mpira wa Tanzania unafeli. “Mfano mdogo, siyo kwamba namponda (Fulgence) Novatus, ni kocha mzuri lakini angefaa kuwepo kocha mwingine pale kwenye nafasi ya kumsaidia Mayanga (ndani ya Taifa Stars).

“Mimi sihitaji nafasi hiyo kwa kuwa wapo wanaoweza kusema nazungumza haya kwa kuwa ninataka nafasi hiyo, ila ninasema ukweli.

“Kama unakumbuka huyo ni kocha ambaye ametoka kuinusuru timu kushuka daraja halafu unampeleka timu ya taifa. “Mimi Julio nilishawahi kufundisha Coastal mara mbili ikiwa katika hali mbaya, mara ya kwanza ilikuwa na pointi nne, mara ya pili pointi saba na nikawabakiza, huo ni uwezo binafsi wa kuweza kufanya kazi na siyo kila mtu kwenye nafasi hiyo anaweza kuwa kocha mzuri.

KUHUSU UONGOZI WA JUU WA SOKA

“Tatizo majungu tu ndiyo mengi, ukikosana na mtu mtaani anaingiza kwenye kazi, ukitaka nafasi anakwambia nenda kaonane na (anamtaja), mimi uwezo ninao inakuwaje niende nikamfuate (anamtaja) ili nimbembeleze.

“Mambo kama hayo ndiyo yametufikisha hapo, tunafanya mambo kwa kutaka kukomeshana, ndiyo mana hatufanikiwi. “Tujifunze kwa Rais Magufuli jamani, siyo kwamba Jakaya (Kikwete) kafanya mabaya, amefanya mazuri mengi tu lakini haya anayoyafanya Magufuli ni muendelezo wa yale yaliyofanywa na Jakaya.

“Wanalazimisha tufanane kila kitu, mimi siwezi kusema mbili mara mbili jibu ni nne, nawe ufanye hivyohivyo, unaweza kutumia njia nyingine mfano mbili jumlisha mbili na jibu likawa ni lile lile lakini njia tofauti.

WANAOIPOTEZA TAIFA STARS

“Tunamlaumu Mayanga bure, wale ambao wapo kwa ajili ya maslahi yao binafsi ndiyo tatizo, ndiyo maana nasisitiza wapiga kura wa uchaguzi ujao wawe makini. “Mimi nasema ukweli kwa kuwa siogopi kufa, ukiniua Julio kwa kusema ukweli, kesho na wewe utakufa, kila mtu atakufa kisha tutakutana huko mbele ya safari afu tuone sasa!

“Nakumbuka wakati tunamuingiza (Leodegar) Tenga madarakani, tulipita mikoani kuwashawishi wajumbe na tukamuomba hadi waziri mkuu wa wakati huo alikuwa (Frederick) Sumaye, akasema kabisa ‘Watanzania wanataka zawadi ya Krisimasi’ akimaanisha tumpe nafasi Tenga.

“Lakini ajabu wapiga kura wakawapa kura nyingi Ndolanga na Wambura, kwa kuwa kura hazikutosha zikarudiwa na kwa sababu wawili hao hawakuwa na uhusiano mzuri ndipo wapiga kura wakageuka na kumpa Tenga. “Huwa najiuliza hivi hao wajumbe hawaoni hayo mambo yanayofanyika humo ndani!

RUFAA YA SIMBA

“Wanalalamika kuhusu pointi tatu za Simba dhidi ya Kagera Sugar, ajabu kabisa, hivi wamesahau kuwa Kagera walishawahi kupata pointi tatu dhidi ya Simba enzi hizo mimi nikiwa kocha! Hivi hawajui hata Serengeti Boys imeenda Afcon kupitia dirishani sababu ya sheria?

KUTUMIA MADARAKA VIBAYA

“Mtu unataka kukifanya chama chako binafsi, kufanya kila kitu ukijiona upo juu ya sheria, ‘who are you by the way in this country? (wewe ni nani katika nchi hii?). Wanatakiwa kumuogopa Mungu kwa mambo wanayoyafanya. “Hata ile kambi ya Morocco mimi najua nani aliyeiwezesha na siyo wao kama walivyojitangaza, nitampa hilo bomu Ali Mayay ili apigie kwenye uchaguzi kama akigombea.

“Achana na hilo, hata bajeti za kambi za timu huwa zinazidishwa ili watu wapate pa kupigia. “Mfano mimi siamini Mayanga kama anahusika katika kutoa maoni ya timu kwenda Misri kwa ajili ya kambi ya siku saba, piga hesabu kwenda na kurudi wamepoteza siku mbili njiani. Sasa mipango gani hiyo! Unaweza kukuta hata kikosi huwa anapangiwa ohh!

KUINGILIA MAAMUZI YA KAMATI

Tumeona hivi karibuni, Rais Magufuli aliunda kamati zake za makalakala sijui makolokolo, uliona ameziingilia? Lakini wewe niambie kuna kamati gani ya TFF imefanya kazi bila kuwekewa mkono. “Chukulia lile tukio la rufaa ya Simba, aliyetangaza maamuzi ya kuipa Simba pointi ni mwenyekiti wa Kagera Sugar na Mtibwa Sugar ambaye yeye ndiye mlezi wa zile timu na anaziombea bajeti kila mwaka, yeye ana uchungu nazo kuliko mtu mwingine yeyote, iweje wewe uibuke na kuingilia.

“Unachagua kamati kisha unakuja unazipinga, na siyo mara moja wala mara mbili tumeona imetokea mara nyingi tu. “Andikeni ili watu wajue.

Dawa ni chungu lakini ili upone lazima uinywe, ndiyo maana namuunga mkono Ali Mayay kwa asilimia elfu tatu kama zipo!

(NA JOHN JOSEPH | CHAMPIONI IJUMAA | MAKALA)

Leave A Reply