The House of Favourite Newspapers

SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (3)

0

SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (3)

ILIPOISHIA JANA

 

Nilifika nyumbani, nikafungua mlango nikiwa siamini kama nilipona katika tukio lile. Niliingia ndani. Nilipowasha taa, sikuamini nilichokiona, yule mtu aliyekuwa akinikimbiza, alikaa juu ya godoro, kashika panga lake mkononi…

 

ENDELEA KUISOMA…

 

NILIANZA kukimbia tena kuelekea barabarani. Alinikimbiza. Nilikunja kona ya Sakubimbi, naye akakunja! Alinikimbiza kwa bidii kimyakimya. Nilikimbia mpaka nikaishiwa nguvu, nikaanguka chini. fahamu zikapotea.

 

Nilishtuka asubuhi, nikajikuta nikiwa nimelala mahali palepale nilipoangukia. Viungo vyote vya mwili viliuma. Watu walikuwa wakinishangaa, wapo waliosikika wakisema: “Mlevi huyo… pombe siyo chai.”

 

Sikuyajali maneno yao, niliwaza jambo moja tu, ni  nani mtu yule aliyenifukuza na kwa namna gani ningeweza kumwepuka.

 

Nilijizoazoa taratibu, kisha nikaikamata njia ya kuelekea nyumbani, nilikiogopa chumba changu, lakini sikuwa na namna nyingine ila kurejea.

 

Nilifika, nikakuta mlango uko wazi, wapangaji wenzangu walinishangaa. Nilisoma akilli zao, waliwaza nilifanya vile kwa sababu ya pombe, hawakujua kilichojificha nyuma ya pazia.

 

Nilipoingia ndani, jambo la kwanza lilikuwa ni kulitupa jicho katika godoro… nilihofu yale mambo ya jana usiku yasije kujirudia. Nilitabasamu, mtu yule wa ajabu hakuwako.

 

Niliamua kujilaza nikishtukashtuka. Sikula kwa muda mrefu lakini sikuhisi njaa. Akili ilikuwa katika mapambano makali. Sikupata usingizi, badala yake likaja  wazo moja. Niende kwa mganga, nisipofanya hivyo, mtu wa ajabu atanitoa roho.

 

Haraka nilikamata begi lililokuwa juu ya kabati bovu. Nikafungua zipu ndogo nikatoa kiasi cha fedha ambacho niliamini kingetosha.

 

Nilikuwa ndani ya gari dogo kuelekea kijijini. Mkononi nilibeba maandazi saba makubwa na niliendelea kuyatafuna taratibu. Mtoto mdogo aliyekaa pembeni aliyakodolea macho maandazi yale. Sikumpa.

 

Haikuwa safari ndefu. Nilifika kijijini, haraka nikaikamata njia kuelekea kwa mtaalamu wa tiba za asili. Nilitembea kwa hofu na woga! Nilihisi muda wowote ningeanza kukimbizwa.

 

Nillifika kwa mganga nikiwa na matumaini makubwa ya kupata tiba. Sifa za mganga huyu zilitapakaa pande zote nne za dunia, alikuwa fundi asiyeshindwa kitu. Nilimtegemea.

 

Baada ya kuingia ndani ya chumba cha mganga, nilieleza shida zangu haraka. Sikuacha jambo hata moja. Mganga aliyevalia mavazi mekundu, mkononi akitikisa kibuyu, na shingoni alisheheni hirizi kubwa zilizopumua.

 

Nilimaliza kuzungumza, ikawa zamu ya mganga kusema: “Nimekusikia mwanangu… kinachokusumbua ni mzimu wa huyo marehemu ambaye hakufurahishwa na kitendo kichafu ulichokifanya mahali alipolala. Hakuna tiba nyingine ila kwenda kuomba radhi katika kaburi lake.”

Itaendelea kesho…

Leave A Reply