The House of Favourite Newspapers

Mawaziri wa Magufuli: Mhe Rais, Kazi Tunaipenda, Tuna Watoto Lakini…

0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’ anakaribia kutimiza miaka miwili madarakani tangu alipoapishwa Novemba 5, mwaka juzi na kuanza kutekeleza sehemu ya sera zake za uboreshaji wa utumishi wa umma na kukuza uchumi.

UCHUNGUZI WA UWAZI

Uchunguzi wa Gazeti la Uwazi ulibaini kwamba, katika utekelezaji huo, baadhi ya wasomi na wanaharakati wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya sera hizo ambapo walieleza kwamba, zina mwelekeo mzuri na kushauri upungufu uliopo udhibitiwe.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba.

Katika kipindi hicho cha uongozi wake, Rais Magufuli alitangaza kubana matumizi serikalini, kuongeza ufanisi katika utumishi wa umma kwa kutumbua watumishi wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu na uzembe huku akidhibiti ukwepaji kodi uliokuwa umeshamiri.

Hata hivyo, kwa upande wao, baadhi ya mawaziri wake waliozungumza na Uwazi kwa nyakati tofauti walitoa kilio chao kwa rais, wakisema kazi wanaipenda na ni njema, wana watoto wanaohitaji malezi kutokana na kipato wanachokipata cha uwaziri, lakini wamekuwa wakifanya kazi kwa wasiwasi mkubwa wa kutumbuliwa hasa linapokuja suala la kuchukua uamuzi mzito kwenye wizara wanazoziongoza.

HOFU YA KUTUMBULIWA

Baadhi ya mawaziri hao waliliambia Uwazi kuwa, wamekuwa katika mikakati ya kuijenga nchi kiuchumi, lakini hali ya utendaji kazi wao siyo wa kufurahia kwani wanaweza kutumbuliwa au kutenguliwa uamuzi wao na uongozi wa ‘ngazi ya juu’.

Walitolea mfano wa jinsi waziri mmoja aliyeshughulikia tatizo la kiutendaji ndani ya wizara yake, lakini akajikuta akitumbuliwa.

Waziri wa Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage.

 

Mwingine aliliambai Uwazi kuwa aliamua kutengua nafasi za baadhi ya watendaji wa moja ya idara za wizara anayoisimamia, lakini uamuzi huo ukatenguliwa na ngazi za juu.

Pia kuna waziri ambaye alitoa sharti kwa wananchi kufunga ndoa, uamuzi ambao haukudumu kwa saa 24, ukatenguliwa hivyo baadhi ya mawaziri nao kuingiwa na hofu au kuchelewa kuchukua uamuzi juu ya jambo fulani.

Hata hivyo, bado mikakati ya pamoja inafanywa na Baraza la Mawaziri ili kuhakikisha nchi inapata maendeleo yaliyokusudiwa, lakini kutokana na hali hiyo hawaonekani wakichacharika na ziara za kushtukiza kama ilivyokuwa mara tu baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli.

Naibu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii na Jinsia, Dk Hamis Kigwangalla.

Uchunguzi huo ulibaini kwamba, sehemu kubwa ya mikakati hiyo inayoendeshwa na Kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’, imepokelewa kwa mikono miwili na wananchi huku baadhi wakionesha wasiwasi kuwa yapo baadhi ya masuala yanayotakiwa kuwekewa mkazo au kurekebishwa ili kuzuia madhara siku zijazo.

UTENDAJI WA AWALI

Baadhi ya mawaziri hao walisema kuwa, utendaji wa Rais Magufuli kwa mwaka mmoja na miezi sita ya awali unaridhisha kwa kiasi fulani katika jitihada za kuwaletea Watanzania maendeleo.

MAWAZIRI WANACHAPA KAZI

Wapo baadhi ya mawaziri wanaotajwa kuwa wanachapa kazi usiku na mchana wakiwemo Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage, Naibu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii na Jinsia, Dk Hamis Kigwangalla, Waziri wa Ardhi, William Lukuvi na wengineo.

Uchunguzi huo ulibaini pia kwamba, kuna maeneo ambayo hayajaguswa ipasavyo kama sekta ya elimu, afya na serikali za mitaa ambako kuna viongozi wachache wanaotumia nafasi zao kuwanyanyasa wananchi na watumishi kwa kufanya ubadhirifu wa mali ya umma.

Waziri wa Ardhi, William Lukuvi.

“Huko ndiko kuna uozo mkubwa na Watanzania wengi wanaishi kwenye halmashauri za wilaya, miji na majiji. Rais aweke nguvu kutumbua viongozi miungu watu,” alisema waziri mmoja.

Katika miezi yake ya awali Ikulu, rais amekuwa katika kampeni kali ya kubana matumizi ambayo imekwenda sambamba na ufutaji wa safari za nje kwa watumishi wa umma hadi kwa kibali maalum, akisema kuwa safari hizo ni mzigo kwa taifa.

Ubanaji huo wa matumizi ulihusisha upigaji marufuku taasisi za umma kutumia kumbi za kukodi kufanyia mikutano na badala yake kutumia majengo ya serikali, jambo ambalo limepingwa na baadhi ya wachumi.

PROFESA NGOWI

Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi alisema kuwa, kubana matumizi yasiyo ya lazima ni jambo jema, lakini ubanaji huo ukifanyika kuzidi kiwango, huleta madhara kiuchumi kwa kuwa serikali inahimizwa kutumia nguvu ili kuchochea maendeleo.

“Serikali ni mlaji mkubwa mahali popote ulimwenguni. Wasibane matumizi kupitiliza, uchumi utasinyaa,” alisema Profesa Ngowi.

Hata hivyo, alisema kuwa Rais Magufuli amefanya vyema zaidi katika kudhibiti ukwepaji kodi katika maeneo mbalimbali hususan bandarini ambako hali ilikuwa mbaya.

WASOMI UDSM

Wasomi wengine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wakizungumzia utawala wa Magufuli walisema unaegemea zaidi kutetea watu maskini na kufufua uchumi wa nchi kwa kuondoa wizi serikalini.

Walitolea mfano jinsi anavyoshughulikia suala la makinikia wakisema kuwa uamuzi wa Rais Magufuli wa kuunda Kamati Teule ya Kuchunguza Makinikia maarufu kama mchanga wa dhahabu, ulikuwa sahihi na kwamba alitumia utaratibu wa kawaida wa kuratibu masuala ya serikali.

PROFESA LUOGA

Profesa Florens Luoga wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuwa uamuzi wa rais wa kuunda Kamati Teule ya kuchunguza mchanga wa madini ulikuwa sahihi na kwamba alitumia utaratibu wa kawaida wa kuratibu masuala ya serikali.

“Serikali ilikuwa inahisi kuwa inaibiwa na katika kuthibitisha hisia zake kama ni kweli au la iliunda tume na ndiyo hiyo imetoa taarifa yake,” alisema Profesa Luoga na kuongeza kuwa katika hali hiyo haikuwa na sababu ya kumshirikisha au kumuuliza kwanza mtu au taasisi inayoishuku.

“Serikali ingewezaje kujua kama kuna udanganyifu bila ya kuzuia mchanga ule na kuufanyia uchunguzi?” Alihoji Profesa Luoga.

PROFESA BAKARI

Kwa upande wake, Profesa Mohamed Bakari wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema kuwa, wananchi walikuwa wakiamini kuwa wanaibiwa sana katika nchi hii kwa miaka mingi bila kujua kwa kiwango gani, lakini sasa wamejua hivyo jitihada za rais zinatakiwa kuungwa mkono na kila Mtanzania.

“Tulikuwa tunaamini, kwa miaka mingi, kuwa tunaibiwa na kwa kweli hawakuwa wanaiba, bali wanachukua, lakini hatukujua ni kwa kiwango gani,” alieleza Profesa Bakari na kumpongeza Rais Magufuli kwa uthubutu wake.

“Dk Magufuli amethubutu, kwa hiyo tumpongeze kwa uthubutu wake kwa kuwa umewasaidia wananchi kujua angalau sehemu ya uhalisia wa mambo,” alisema.

THOMAS NGAWAIYA

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Kiraia ya Cegodeta na Mbunge wa Zamani wa Moshi Vijijini, Thomas Ngawaiya alisema kuwa, hadi sasa utawala wa Rais Magufuli una mwelekeo mzuri katika usimamizi wa kiuchumi na kiutendaji, lakini amekosa sera kuu ya uchumi.

“Kueleza kuwa nchi ya viwanda ni sawa, lakini mwelekeo wa uchumi ndiyo unasaidia kwa sababu viwanda hivyo havijengwi na serikali, bali wawekezaji,” alisema kiongozi huyo ambaye ni mfanyabiashara.

Kuhusu utendaji wa serikali kwa jumla, Ngawaiya alisema kuwa, Rais Magufuli anaipeleka nchi katika mwelekeo mzuri kwa kuwa ameitoa kwenye ngazi hasi hadi sasa ambako ufanisi umeanza kuonekana katika utumishi wa umma.

Alisema kuwa, kuna madhara ya muda mfupi ya kiuchumi kutokana na ubanaji matumizi na ukwepaji kodi, lakini ni bora kuliko kuwa na kampuni inayosaidia ukuaji uchumi kwa kuajiri wengi kwa njia zisizo halali.

MSEMAJI WA SERIKALI

Msemaji wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk Hassan Abbas alipopigiwa simu juzi alisema yupo kwenye msiba wa mama yake na ataweza kuzungumzia Utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano atakapomaliza shughuli za msiba wa mama yake mzazi.

Katika kuhahikikisha nchi inakuwa safi, Rais Magufuli alianza utawala wake kwa utumbuaji majipu ambao jamii imeshuhudia vigogo wa mashirika makubwa nchini kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) wakisimamishwa kupisha uchunguzi wa tuhuma za ufisadi na wengine wakipelekwa mahakamani.

Hata hivyo, utumbuaji huo umeonekana kukubalika na wengi, lakini baadhi wamepinga staili ya watumishi hao wanavyotumbuliwa ikiwamo kuuliza wananchi kama mtumishi anafaa kutumbuliwa au la kama alivyofanya rais wakati akimtumbua aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe ambaye sasa ni marehemu.

Leave A Reply