SAA chache kabla ya mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Azam FC dhidi ya Simba kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Azam Complex, kuna mambo yameibuka na inavyoonekana ushindani utakuwa mkali kutokana na upepo ulivyo kwa timu zote hizo.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu kwa kuwa kila upande umejipanga vizuri na umekuwa ukijinadi kuwa upo vizuri lakini gumzo zaidi ni kitendo cha mchezo huo kuchezwa kwenye uwanja huo maarufu kwa jina la Uwanja wa Chamazi, ambao unamilikiwa na Azam FC, ikiwa ni mara ya kwanza baada ya kupita kipindi cha muda mrefu tangu Simba walipocheza kwenye dimba hilo mchezo wa ligi kuu.
Akizungumzia mchezo huo, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, amesema kuwa wanajua uwanja huo sehemu ya kuchezea ‘pitch’ ni ndogo tofauti na ulivyo Uwanja wa Taifa ambao wamekuwa wakiutumia kama uwanja wao wa nyumbani, lakini kuna mikakati mizuri wameipanga kuhakikisha wanapata ushindi.
Akifafanua zaidi Manara alisema: “Tunajua uwanja wao ni mdogo tofauti na Taifa lakini kocha wetu Joseph Omog ni kocha mkongwe na wa kimataifa, ameshawahi kuifundisha Azam kwa mafanikio, anaujua uwanja wao vizuri.
“Hivyo alichoamua kufanya ni kubadili mbinu ili timu iweze kucheza soka linaloendana na uwanja, unajua Simba tumeshazoea kucheza soka la kutanua uwanja, sasa mbinu za jinsi ya kuutumia Uwanja wa Azam Complex zimeshafanyika na tunaamini tutaibuka na ushindi.
“Tuna mifumo mipya kwa ajili ya uwanja huo, tunaamini tutaibuka na ushindi.”
Katika mazoezi ya jana ya timu hiyo, straika John Bocco wa Simba alifanya mazoezi kama kawaida na kuna uwezekano mkubwa akacheza katika mchezo huo.
Kuhusu mapato
Manara pia alizungumzia suala la mapato kwa kusema kuwa ni vema Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) likaamua mfumo wa kuifanya timu ya nyumbani kubeba mapato yote ya mchezo, hoja ambayo ilijibiwa na Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas aliyesema suala hilo anatakiwa kuliwasilisha katika mamlaka husika na linaweza kufanyiwa kazi kuanzia msimu ujao kwa kuwa tayari msimu wa sasa umeshaanza.
Okwi, Juuko ndani ya nyumba
Aidha, Manara alisema wachezaji wao wa kimataifa raia wa Uganda, Emmanuel Okwi na Juuko Murshid walitarajiwa kuwasili jana mchana kujiunga na timu hiyo wakitoka kwenye majukumu ya timu ya taifa na hivyo wanategemewa kuwepo katika mchezo wa kesho.
Kuhusu beki wao Shomari Kapombe, alisema anaendelea vizuri wakati kipa wao Said Mohamed ‘Nduda’ anatarajiwa kuondoka wikiendi hii baada ya safari yake kuchelewa kutokana na suala la visa.
Azam nao watoa neno
Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd upande wake alisema wamefurahishwa na uamuzi wa TFF kupeleka mchezo huo uwanjani hapo na kusisitiza maandalizi yapo na wanaamini watautumia vema uwanja wao.
Kuhusu Tshishimbi
Wakati huohuo, Manara amesema kitendo cha baadhi ya mashabiki wa soka kumshambulia kuhusu ulemavu wake wa ngozi siyo uanamichezo na kuwataka wataniane kwa hoja za kishabiki na siyo kuhusu ulemavu wa mtu.
Manara amesema hayo baada ya hivi karibuni kuibuka kwa kashfa nyingi dhidi yake kutokana na yeye kutumia kurasa zake za kijamii kumtania kiungo wa Yanga, Papy Tshishimbi ambapo amekuwa akiweka picha zinazoonyesha kuna watu wanamuita mchezaji huyo Shishi Baby.
“Mimi nimeshazoea utani, kuna vitu ambavyo wao wanavuka mipaka, utani katika soka ni kitu cha kawaida na hata nilichofanya sikuwa na maana mbaya, lakini wao wanaanza kutukana kuhusu ulemavu, naweza kuvumilia vipi kuhusu hao wengine wenzangu ambao nao wana hali kama mimi.
“Nafikiri kwa kuwa kuna namba zao za simu mitandaoni hao wanaotukana ni vema jeshi la polisi likafanyia kazi suala hilo.”
Stori: Khadija Mngwai na Ibrahim Mressy | Championi