The House of Favourite Newspapers

Kagera, Majimaji Zamtia Kiwewe Okwi

Mshambuliaji hatari wa Simba, Emmanuel Okwi.

MSHAMBULIAJI hatari wa Simba, Emmanuel Okwi raia wa Uganda amefunguka kuwa anazihofia timu ambazo watakutana nazo kwenye mechi zijazo kwa sababu timu hizo watawapa­nia kwa ajili ya kutaka kuvunja rekodi yao ya kutokufungwa.

 

Kinara huyo wa mabao ligi kuu ame­waongoza Simba kutwaa ubingwa kwa msimu huu lakini pia wakiwa hawajafungwa kwenye mechi zao 28 ambazo wamezicheza hadi sasa huku wakiwa wamebakisha mich­ezo miwili pekee.

 

Simba inayonolewa na Mfaransa, Pierre Lechantre imebakisha michezo dhidi ya Kagera Sugar ambao wataucheza kwenye Uwanja wa Taifa, Mei 20, kabla ya kwenda kuhitimisha msimu wao ugenini kwa kucheza na Majimaji ya Songea.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Okwi aliyefunga mabao 20 kwenye ligi amesema wanatakiwa kupambana zaidi kwenye mechi hizo mbili kwa ajili ya kutafu­ta matokeo mazuri kwa sababu wapinzani wao wataingia uwanjani wakiwa na wazo moja la kuwatibulia rekodi yao ya kutoku­fungwa hadi sasa.

 

“Kwetu bado hatujamaliza ligi tunatakiwa kupambana zaidi kuhakikisha kwamba tunashinda kwenye mechi hizi ambazo zimebakia, ni muhimu kuendelea kutafuta matokeo mazuri kwa ajili ya kuitunza rekodi ya kutofungwa kwa msimu huu.

“Najua wapinzani wetu wanaofuata Kagera na Majimaji watakuja uwanjani kwa kupania mechi na kucheza kwa nguvu ili tu waweze kututibulia rekodi yetu ya kuto­fungwa, hivyo itatulazimu sisi kupambana kushinda mechi hizo,” alisema Okwi.

Stori na Said Ally, Dar es Salaam

Comments are closed.