HAKUNA asiyemfahamu Mzee Akilimali kutokana na umaarufu wake ndani ya Klabu ya Yanga ambako amekuwa akivutana na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo huku wakidai kuwa ndiyo anakwamisha maendeleo ya klabu.
Jina lake halisi ni Ibrahim Akilimali. Huyo ni Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga ambaye amekuwa akitoa maneno ya shombo kwa wachezaji au hata viongozi wa timu hiyo anapoona hawafanyi vizuri. Siyo kwamba haipendi Yanga, bali huyu ni Yanga lialia.
Lakini wapenzi wa soka nchini wamekuwa wakijiuliza mambo kadhaa kuhusiana na mzee huyo ambaye haishiwi vituko kila kukicha kama.
Championi limefanya naye mahojiano maalum ili kujua mambo kadhaa muhimu kuhusiana na Klabu y a Yanga.
LIGI IMEMALIZIKA NA YANGA IMESHIKA NAFASI YA TATU, UNASEMAJE?
“Lazima turidhike na yaliyotokea kwa sababu asiyekubali kushindwa siyo mshindani na siku zote mchezo wa mpira ni kama mchezo wa kupokezana kijiti.
“Naridhika na matokeo yaliyotokea katika mchezo japo hatakuwa vizuri, hata hivyo, niwashukuru wachezaji na viongozi wetu kwani hapa tulipofikia si pabaya zaidi, turidhike, lakini tukumbuke mwisho wa ligi ndiyo mwanzo wa ligi.
“Haya yaliyotokea katika msimu mzima yawe funzo ya kuona tulikosea wapi ili msimu ujao tusirudie tena makosa yaleyale, ni lazima tujiimarishe ili tuweze kuirejesha Yanga katika nafasi yake ya kimataifa.
UNADHANI YANGA ILIKOSEA WAPI MSIMU HUU?
“Kiukweli Yanga ilikosea sehemu nyingi tu na zipo dhahiri, sehemu ya kwanza kulikuwa na tofauti kwa viongozi na wakati huohuo aliyekuwa mwenyekiti wetu, Yusuf Manji alijiuzulu, mambo ya kipesa yalikwenda ndivyo sivyo kwa hiyo tukikosea sehemu nyingi.
“Unafahamu wachezaji ni sawa na watoto ambao hawawezi wakajua kwamba leo baba hana kitu maana siku zote wanafurahi kuona chungu kinachemka na wao wanapata chakula, sasa kwa viongozi wetu ambao wapo hadi leo walishindwa ile hekima ya kizee ya kujua wafanye nini ili watoto wapate chakula kama kawaida.
“Viongozi waliposhindwa hilo, wakawa wanapiga kelele kwamba hakuna pesa, mara Mzee Akilimali zile pesa ulizotuahidi zipo wapi, wale wafadhili wapo wapi? Jamani hivi ni kweli mimi Mzee Akilimali niliahidi wafadhili nitawaleta Yanga? Hamnisaidii hata nyinyi waandishi wa habari au niliwaahidi mimi ninazo pesa za kuwapa Yanga?
“Mimi nilikataa jamani uendeshaji wa klabu badala ya kuitwa Yanga Afrika iitwe Yanga Yetu, hicho ndicho nilichokataa, sikukataa labda kama ninawafadhili au nitawaleta kina nani, hapana, tusisingiziane, nilikataa Yanga kukodishwa ila sikusema hayo yaliyosemwa.
“Narudia tena, nilisema kwamba Yanga hii haikodishwi na hatuna sababu ya kupoteza, tathmini ya wazee wetu ambao ni waanzilishi wa Yanga Afrika, leo tuitoe huko tukaiite Yanga Yetu, hilo haliwezekani, wakaniuliza labda mimi sitaki maendeleo ya Yanga, kiukweli mimi nataka maendeleo.
“Mimi ni mhanga wa maendeleo kwa sababu nakumbuka nimetembea nusu ya Tanzania kwa lengo la kutaka Yanga ianzishe kampuni itakayojulikana Yanga Afrika Sports Cooperation Limited, iwe kampuni ya hisa tena itakuwa ya umma na kwa upande wa hisa klabu ibaki na asilimia 51 na wanahisa wawe na asilimia 49.
WEWE NDIYO SABABU YA MANJI KUONDOKA NDANI YA YANGA?
“Wanasema kuyumba kwa Yanga, Mzee Akilimali ndiyo chanzo mpaka Manji kuachia ngazi kwa sababu nilikataa Yanga isikodishwe wala hakuna jingine ambalo nilikataa na mimi na Manji tulipata kukaa hivi nikamueleza baba unapotupeleka wapi, kwa nini hurudi nyuma.
“Na kilichomuondoa Manji Yanga lazima niwaambie Watanzania, siyo Mzee Akilimali, Akilimali mimi nani kwanza, hivi mende anaweza kuangusha kabati? Mimi sina hela, mimi ni lofa, hata hapa ninapokaa barabarani naonekana sina kitu, yaani mimi naweza kumpindua Manji kwa kipi labda.
“Ki l ichompindua Manji alikuwa hapendi kushirikiana na w e n z a k e w a k a w a sawa, amejiuzulu baada ya SportPesa walipokubaliwa na uongozi wa Yanga kuwa wadhamini wa timu na siyo kwa sababu ya Mzee Akilimali.
UNAWEZA KUSEMA KIPINDI CHA MANJI KULIKUWA NA MATATIZO KAMA HAYA?
“Kuhusu suala la mishahara hata wakati wake watu walikaa hadi miezi miwili hawajalipwa kitu lakini kulikuwa na mtu anadhamini kila kitu na aibu hiyo ilikuwa haitoki.
“Lakini kulikuwa na udhamini na kulikuwa na mtu wa utunzaji wa pesa, hivi leo tuseme Yanga ni masikini kiasi hicho, Yanga siyo masikini, tuna Sportpesa wanatoa mamilioni mangapi, tuna watu sasa hivi wamekuja kuingia mikataba na Yanga kwa ajili ya kuuza jezi na wamesema watatoa bilioni sijui ngapi, sasa mipango ipo wapi.
WANADAI HALI YENU MBAYA INAZIDI KILA KUKICHA
“Hao kwa Yanga hii au nyingine, sisi tunachosubiri sasa hivi ni kuruhusiwa kufanya uchaguzi wetu na tukishafanya uchaguzi tu, Yanga itawekwa sawasawa, itakuwa klabu inayotisha Tanzania na Bara la Afrika kwa sababu mipango itakuwepo.
“Hawa viongozi wetu w a liokuwepo sasa mipango yao imefeli, walikuwa hawawezi kufanya mipango kwa kuwa walikuwa wategemezi lakini hao tutakaowachagua tutawaambia dira yetu ndiyo hiyo, ipelekeni Yanga na wao watakuwa hawana tegemezi na watafanya mipango thabiti ya kuipeleka Yanga mbele.
Unasema mambo ya uchaguzi, lakini uongozi umetangaza mkutano mkuu, hapa vipi?
“Wanapingana na serikali, serikali imewaambia hawataki mikutano isipokuwa wafanye uchaguzi ila wao wanasema hawatafanya hivyo.
UNATAKA UCHAGUZI, UNA MPANGO WA KUGOMBEA?
“Kama kweli uchaguzi utafanyika safari hii basi Mzee Akilimali atakuwa Rais wa Yanga, hivyo lazima nigombee, nikiwa rais hakuna atakayelia njaa Yanga.
LAKINI SIYO MARA YA KWANZA KUSEMA HIVYO
“Wakati ule nilikuwa nimemuachia Manji lakini safari hii naingia mimi mwenyewe hakuna hata mchezaji wangu ambaye atapiga kelele kuhusu kulalamikia kucheleweshewa pesa zake.
LAKINI MWANZONI ULISEMA WEWE NI LOFA?
“Nasema hivi ukisikia mbwa anabweka basi ujue yupo kwao au nyuma yupo bwana wake au nikwambie, siwezi kuongea hilo, lakini kikubwa tuijenge Yanga yetu kutokana na haya tuliyoyavuna ndani ya msimu huu.
“Naamini tukifanya hivyo kwenda katika uchaguzi halafu tukachagua viongozi wapya basi tutatisha msimu ujao na kurudisha heshima yetu.
YANGA INAKWENDA KUWA WA MCHANGANI MSIMU UJAO, UNAZUNGUMZIAJE?
“Tunakwenda kwenye msimu mpya sawa kwani hata Simba haikuweza kushiriki michuano ya kimataifa kwa muda wa miaka mitatu mpaka tumewaita wazee wa mchangani unadhani walikuwa hawajipangi kwa ajili ya kuleta mafanikio.
“Basi na sisi tutajipanga na hatuwezi kuwa wa mchangani kama walivyokuwa wao kwa sababu Simba haitoweza kuchukua ubingwa mara mbili mbele yangu nikiwa rais wa Yanga, hiyo mara moja itakuwa inamtosha kabisa na wakipanda ndege na sisi tunapanda ndege.
UNAZUNGUMZIAJE DONALD NGOMA KUONDOKA?
“Ngoma muache aende tu kwa sababu hata msimu huu ameshindwa kuwa msaada katika timu kwa kuwa amecheza mechi nne pekee kati ya 30 za msimu mzima.
“Pia mkumbuke Ngoma wakati yupo kule FC Platinum nilibahati kwenda kule waliweza kusema uwezo wake ndani ya uwanja na pia walitoa angalizo kuhusiana naye kuwa ni msumbufu na ni kweli yamekuja kutokea yale ambayo tuliambiwa kule na wakati ule sikuwa na uwezo wa kuongea na viongozi lakini ngojeni tufanye uchaguzi na mimi nitakuwa pale kama kiongozi.
“Na hao wachezaji wengine wa kimataifa wakitaka kuondoka waondoke wote tu, mfano, Chirwa (Obrey) amejiita mzee wa kulima ndiyo akawa amepotea kabisa.
“Wameondoka wengi Yanga waache waende mbona Niyonzima (Haruna) ameondoka.
VIPI KUHUSU KELVIN YONDANI?
“Kiukweli kama kweli Kelvin Yondani ataondoka Yanga nitaumia na nitalia sana kwa sababu ni mmoja kati ya wachezaji ambao walikuwa wanacheza kwa kujituma sana, ni bora waende wote ila yeye abaki pale Yanga na kipindi hiki ndiyo alitakiwa abaki kurithi mikoba ya Cannavaro (Nadir Haroub) kuweza kuwaongoza wenzake.
Comments are closed.