The House of Favourite Newspapers

GLOBAL TV: KUHAMIA KWENYE VING’AMUZI

BAADA ya kutamba kwa muda mrefu, chaneli namba moja online kurusha live matukio yote yanayotikisa Tanzania kisha wengine wakafuata baadaye, Global TV ipo katika mipango ya kuhamia kwenye ving’amuzi na kuwafikia watu wote ndani na nje ya nchi.

 

ITAKUWAJE?

Akizungumza na Ijumaa, Mkuu wa Idara ya Global TV, James Range anasema kwamba moja kati ya mipango mikubwa inayotarajiwa kuletwa na Global TV ni kutoka kuwa online na kuingia moja kwa moja kwenye ving’amuzi.

“Mipango ya kuingia katika ving’amuzi ipo mbioni kutimia na hii ni kwa sababu tumekuwa tukipata maoni mengi hasa kutokana na baadhi ya vipindi vinavyoruka Global TV Online kama vile taarifa ya habari inayoruka kila siku saa

12:30 Jioni ikiwa ndani yake na uchambuzi chini ya mtangazaji Elvan Stambuli pamoja na habari za kimataifa zinazounganishwa moja kwa moja na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (VOA),” anasema Range.

 

MIPANGO MINGINE

Range anaendelea kuwa, mbali na Global TV kuanza kupatikana kwenye ving’amuzi, mipango mingine ni kutanua wigo wa watangazaji wake.

“Tuna wawakilishi wa Global TV sehemu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania, ndiyo maana nikasema Global TV ni online pekee yenye wawakilishi wengi ndani na nje ya nchi.

“Tayari mpaka sasa tunaweza kurusha matukio yote moja kwa moja kupitia wawakilishi wetu wa Amerika, Ulaya, Afrika na Asia. Mfano sasa hivi ukiwa nchini Marekani tuna wawakilishi wa Global TV, ukienda Uingereza, Kongo (DRC) na Kenya kote

huko wapo wawakilishi,” anasema Range.

Range anasema pia, lengo kubwa ni Global TV kutanua wigo wa kuwa na wawakilishi sehemu kubwa ya dunia.

“Mipango iliopo sasa ni kuongeza wigo kila siku, mfano sasa hivi tunamipango ya kutanua wigo Oman, China na Uganda.”

 

VIPINDI VYA GLOBAL TV

Global TV imedhamiria kukata kiu ya watazamaji wa vipindi tofauti vya online ambapo mbali na Global Habari, kila siku saa 12:30 Asubuhi kuna kipindi cha Amka na Global TV kinachoongozwa na mtangazaji Aron Felix.

 

“Kuna kipindi namba moja cha michezo online kiitwacho Spoti Hausi kinachojiri kila siku ya Alhamisi kuanzia saa 10:00 kamili Jioni kikiongozwa na watangazaji mahiri, Wilbert Morand, Phillip Nkini pamoja na Saleh Ally ‘Jembe’.

Vipindi vingine ni Global Entertainment ambacho hukuangazia yale yote yanayojiri kwa upande wa burudani kila siku ya Jumamosi saa 5:00 Asubuhi kikiongozwa Given Mashishanga, kipindi cha Beauty & Styles kinachoongozwa na Catherine Kahabi.

 

VOA WAPO

Wale wapenda kujua yanayojiri nje ya nchi, Global TV kwa kushirikiana na VOA wamekuletea vipindi ba’kubwa kama vile Shaka Ssali Extra Time kinachoruka kila siku ya Jumatano saa 5:00 asubuhi na Straight Talk Africa kila Alhamisi saa 5:00 Asubuhi.

“Kila siku ya Jumanne saa 5:00 Asubuhi tuna kipindi cha Washington Bureau kinachoongozwa na mtangazaji mkongwe na mahiri, Sunday Shomari,” anasema Range.

 

UNAIPATAJE SASA HIYO GLOBAL TV?

Ni rahisi sana, ili uwe unapata habari papo hapo kuanzia kwenye simu yako, tableti, laptop au kompyuta yako, ingia kwenye Mtandao wa Youtube kisha andika Global TV Online baada ya kuingia jisajili (subscribe) bila kusahau kubonyeza kengele pembeni yako ili uwe unajulishwa kinachoendelea.

 

APP PIA IPO

Global TV pia inapatikana kupitia Application ‘App’. Unachotakiwa kufanya ni kuwa na simu yako au tableti kisha ingia kwenye Play Store kwa wale watumiaji wa Adroid na utafute Global Publishers (utaona neno GP la rangi nyekundu) baada ya hapo install kisha utaweza kuona kila kitu humo ndani kuanzia Global TV, Magazeti ya Global Publishers na vingine vingi.

MAKALA: Andrew Carlos.

 

BOFYA ==> GLOBAL TV ONLINE

Comments are closed.