The House of Favourite Newspapers

Makocha Hawa Kazi Wanayo Msimu Ujao

Hans Van Pluijm.

MSIMU wa 2017/18 ukiwa hata haujapoa vizuri tangu ulipofikia tamati Mei 28, mwaka huu, tayari baadhi ya timu zimeshaanza maandalizi kwa ajili ya msimu ujao wa 2018/19.

 

Timu nyingi zimeanza maandalizi kwa kufanya marekebisho ndani ya vikosi vyao kwa kushusha majembe ambayo wanaamini yatawasaidia.

 

Japo dirisha rasmi la usajili halijafunguliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lakini tayari timu zimeshaanza kuonyesha vurugu zao kwenye suala zima la kusajili wachezaji ambapo hadi sasa Azam, Simba na Singida United wanashindana kwenye kuongeza nyota wapya kwenye timu zao.

 

Wakati zoezi la usajili wa wachezaji likiendelea kuna baadhi ya timu ambazo zenyewe zimeenda mbali zaidi kwa kuwaajiri makocha wapya ambao ndiyo watakuwa mstari wa mbele kwa kuzipigania timu zao.

Championi linakuchambulia juu ya makocha hao na ugumu ambao watakutana nao msimu ujao.

 

HANS VAN PLUIJM-AZAM

Mholanzi huyu ameula kuinoa Azam baada ya kuwa na msimu mzuri Singida United ambayo aliifikisha fainali ya FA na kukamata nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi. Matumaini makubwa ya viongozi wa Azam kumuongeza Pluijm kwenye benchi lao ni kutaka kuifanya timu hiyo iongeze makali yake sambamba na kutwaa ubingwa.

 

Pluijm ameonyesha uwezo mkubwa akiwa na Yanga na Singida United, hivyo mashabiki watakuwa na hamu ya kumuona ni kwa namna gani ataendeleza rekodi zake za kutamba kwenye ligi akiwa na timu mpya. Mholanzi huyu amesaini mwaka mmoja kwenye timu hiyo inayodhaminiwa na Benki ya NMB na sasa itakuwa ikijulikana kama kampuni.

 

AMRI SAID-MBAO FC

Amezoeleka kwa jina la utani la Jaap Stam, ambalo ni la nyota wa zamani wa Manchester United na AC Milan. Mabosi wa Mbao FC wameona juu ya uwezo wake na kuamua kumchomoa pale Lipuli na kumpa majukumu ya kuwa kocha wao mkuu baada ya kuondoka kwa Mrundi, Etienne Ndayiragije.

 

Katika msimu ujao, Amri Said atakuwa na kibarua pevu cha kuonyesha ujuzi wake ambao aliounyesha akiwa na Lipuli FC na kuifanya kushika nafasi ya saba kwenye msimu wake wa kwanza, lakini safari hii atakuwa peke yake tofauti na alivyokuwa katika klabu yake ya zamani akisaidiana na Selemani Matola.

 

ETIENNE NDAYIRAGIJE-KMC

Msimu wa 2018/19, utakuwa wa tatu kwake tangu alipokanyaga ardhi ya Tanzania. Kwa misimu miwili alikuwa na kikosi cha Mbao FC cha Mwanza ambacho aliachana nacho katikati ya msimu uliomalizika hivi karibuni, lakini kama bahati amepewa nafasi ya kuiongoza timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC).

 

Ndayiragije kwa msimu ujao atakuwa na wakati mgumu wa kuiongoza kwa mara ya kwanza timu hiyo kucheza ligi kuu na kuona inafanya vizuri na kusalia katika ligi kwa misimu mingine zaidi. Mashabiki wake watataka kuona kama ana uwezo wa kurudia tena maajabu ya kufika fainali ya kombe la FA kama ambavyo alifanya miaka miwili nyuma akiwa na Mbao FC.

 

HEMED MOROCCO-SINGIDA UNITED

Mzanzibar huyu ndiye amekabidhiwa avae viatu vya Mholanzi Hans van Pluijm ndani ya kikosi cha Singida United. Tayari ameshaanza kazi ndani ya timu hiyo ambapo alikuwa nacho kwenye michuano ya SportPesa Super Cup iliyofanyika nchini Kenya.

 

Kocha huyu mwenye rekodi mbalimbali visiwani Zanzibar ndiye atakuwa na wakati mgumu zaidi miongoni mwa makocha wapya kutokana na rekodi ambazo zimeachwa na mtangulizi wake ambaye aliifanya timu hiyo kucheza fainali ya FA, pia kukamata nafasi ya tano katika ligi, hivyo wengi wanatarajia kuona kama ataweza kufikia rekodi hizo ama la.

 

JEAN BAPTISTA KAYIRANGA – ALLIANCE

Ni wageni kwenye ligi kuu kwa msimu ujao, lakini tayari wameamua kuongeza nguvu kwenye timu yao kwa kumshusha kocha wa kigeni ambaye ataiongoza timu hiyo ambapo zali limemshukia Mnyarwanda, Jean Baptista Kayiranga.

 

Kazi kubwa aliyonayo Mnyarwanda huyo ni kuhakikisha anaushusha utawala wa Mbao FC katika Mkoa wa Mwanza kisha kupambana na timu nyingine kuwania nafasi ya kuendelea kubakia kwenye ligi.

Comments are closed.