The House of Favourite Newspapers

Hawa Wataenda na Kombe Kwao…Kombe la Dunia

FAINALI za Kombe la Dunia zinatarajiwa kuanza kesho na mataifa mbalimbali yameshawasili nchini Urusi kwa ajili ya kujiandaa kuingia uwanjani.

 

Hizi ni fainali kubwa ambazo zimekuwa zikisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka duniani kote kwa kuwa zimekuwa zikishirikisha timu kutoka kwenye kila bara duniani.

Afrika itaingiza timu tano ikiwa na kumbukumbu kuwa mafanikio makubwa ya timu zao basi ni kufika hatua ya robo fainali.

Championi leo linakuletea timu ambazo zinapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huu mwaka huu, kumbuka kuwa bingwa mtetezi ni Ujerumani ambao waliutwaa ubingwa huo miaka minne iliyopita lakini leo wana makali yaleyale na wanapewa nafasi ileile.

UJERUMANI: STAA: MESUT OZIL

VIWANGO: 1

Ujerumani wameshatwaa ubingwa huu mara nne na wanakwenda kutafuta ubingwa wa tano.

Nchi hii inashika nafasi ya kwanza kwa ubora duniani kwa sasa na inakwenda kwenye fainali hizo ikiwa inapewa nafasi ya juu ya kutwaa ubingwa.

 

Wanapewa nafasi hiyo kwa kuwa mwaka jana walifanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mabara, wakiwa na kikosi chenye vijana wengi wasio na uzoefu.

Ujerumani wakitwaa ubingwa huo watakuwa wamelingana na Brazil kwa kutwaa ubingwa mara nyingi, lakini pia watakuwa wamefikia rekodi ya Brazil ya kutwaa ubingwa huo mara mbili mfululizo.

 

Staa anayepewa nafasi ya kuibeba timu hiyo ni kiungo Mesut Ozil ambaye amekaa kwenye timu hiyo kwa muda mrefu na alikuwepo wakati wanatwaa ubingwa uliopita.

 

BRAZIL:  STAA: NEYMAR

VIWANGO: 2

Bado inakuwa ngumu kuwaeleza mashabiki kuwa Brazil wanaweza kutwaa ubingwa huu kutokana na kile kilichotokea miaka minne iliyopita.

Lakini ukweli ni kwamba Brazil wanaweza kufanya mambo makubwa msimu huu kwa kuwa kwanza wana wachezaji wengi ambao wameshapata uzoefu wa kutosha.

Kikosi cha Brazil kwa sasa kimejaza wachezaji wengi ambao wana uzoefu wa kutosha tofauti na miaka minne iliyopita ambayo walikuwa wanamtegemea Neymar tu.

Timu hiyo ina makombe matano ya dunia na ndiyo nchi iliyotwaa ubingwa huo mara nyingi, kwa sasa inakwenda ikiwa inashika nafasi ya pili kwa ubora duniani, bado staa wao anabaki kuwa Neymar.

 

UBELGIJI:

STAA: EDEN HAZARD

VIWANGO: 3

Ubelgiji wameshaonyesha kuwa wanaweza kufanya mambo makubwa msimu huu kutokana na timu yao kujaza wachezaj wengi wanaocheza ligi kubwa barani Ulaya.

Ubelgiji imeonyesha kiwango cha juu kwenye michezo kadhaa, timu nyingi zimekuwa zikiwahofia kutokana na kuonyesha uwezo wa juu kwenye michezo iliyopita ya kirafiki.

Baadhi ya mastaa wa timu hii ni Thomas Meunier, Nacer Chadli, Dedryck Boyata, Michy Batshuayi, Marouane Fellaini na Axel Witsel.

 

Pia nchi hiyo ndiyo inakwenda kwenye fainali ikiwa na makocha vijana ambao ni Roberto Martinez na msaidizi wake, Thierry Henry, lakini inamtegemea staa Eden Hazard.

 

 

UFARANSA:

STAA: ANTOINE GRIEZMANN

VIWANGO: 7

Nchi nyingine ambayo inatia hofu kwenye fainali za mwaka huu ni Ufaransa ambayo imejaza wachezaji wengi weusi.

Nchi hii imekuwa ikipewa nafasi kubwa kutokana na kuwa na wachezaji wengi wenye uwezo wa hali ya juu ndiyo maana mashabiki wanataka kiungo Paul Pogba awekwe pembeni.

Ufaransa imefanya vizuri kwenye michezo yote ya kirafiki waliyocheza, lakini bado wakionekana kuwa wanapata shida kwenye safu ya ushambuliaji ambayo ina Griezmann na Olivier Giroud, lakini hakuna mwenye hofu kuwa timu hiyo itawika msimu huu, kumbuka kuwa walitwaa ubingwa kwa mara ya mwisho mwaka 1998.

 

HISPANIA: STAA: ANDRES INIESTA

VIWANGO: 10

Kwenye viwango vya soka duniani, Hispania hawapo vizuri kwa kuwa wameshuka hadi nafasi ya kumi, lakini ni timu ambayo inaaminika kuwa itafanya vizuri na inaweza kutwaa ubingwa.

Hispania ina wachezaji wengi mahiri ambao wamefanya vizuri duniani msimu huu, lakini pia ina mshambuliaji Diego Costa ambaye hatabiriki akiwa uwanjani.

Pamoja na Iniesta ambaye anaonekana kuwa atakuwa akicheza fainali zake za mwisho pia nchi hiyo itakuwa ikiwategemea viungo Thiago, Sergio Busquets, Saul, Isco, David Silva na Marco Asensio, ambao wamekuwa mahiri kwenye klabu zao.

 

 

URENO: STAA: CRISTIANO RONALDO

VIWANGO: 4

Ureno walikuwa hawapewi nafasi ya kutwaa ubingwa wa Euro kipindi cha nyuma, lakini wakafanya mambo makubwa na kutwaa ubingwa huo.

Timu hiyo ambayo inam-tegemea staa wao Cristiano Ronaldo pekee imekuwa imara kwa siku za hivi karibuni kutokana na kuzalisha wachezaji wengi mahiri na sasa inaaminika kuwa inaweza kutwaa tena ubingwa wa dunia.

Comments are closed.