The House of Favourite Newspapers

Lipuli yamkazia Seleman Matola kwenda Simba

Kocha Seleman Matola

 

WAKATI Simba ikipanga kuanza kumtumia Kocha Seleman Matola kwenye michuano ya Kombe la Kagame, uongozi wa Lipuli FC umesema hautakuwa tayari kumuona kocha huyo anaondoka kikosini mwao kama Amri Said aliyetua Mbao FC.

 

Matola ambaye msimu uliopita aliifundisha Lipuli na kuisaidia kumaliza katika nafasi ya saba kwa sasa yupo huru baada ya mkataba wake kumalizika.

 

Taarifa zinasema Matola anakwenda Simba akawe msaidizi wa Kocha Masoud Djuma ambaye yeye anapandishwa na kuwa kocha mkuu baada ya Mfaransa, Pierre Lichante kutimuliwa. Michuano ya Kagame inatarajiwa kuanza Juni 29, mwaka huu jijini Dar.

 

Mwenyekiti wa Lipuli, Ramadhan Mahano ameliambia Championi Jumamosi kuwa, hawapo tayari kumuacha Matola.

 

“Mkataba wa Matola umefikia ukingoni na tunaendelea na mazungumzo naye tuna imani tutakuwa naye msimu ujao. Tumekuwa tukisikia taarifa za kuhusishwa na Simba, lakini kwa upande wangu kama mwenyekiti sijapewa taarifa yeyote iliyo rasmi, hivyo tunategemea kuwa naye katika msimu ujao kupitia makubaliano tutakayoafikiana,” alisema Mahano.

 

Naye Matola alisema: “Mazungumzo kati yangu na Lipuli yanaendelea vizuri lakini bado sijasaini, kuhusu Simba bado sijafanya mazungumzo yoyote na uongozi wa timu hiyo kuhusiana na suala hilo ila mambo yakiwa sawa nitaweka wazi.”

 

Matola ambaye alikuwa nahodha wa Simba wakati akicheza soka ndiye nahodha pekee aliyewahi kuipeleka timu hiyo kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003.

Waandishi Wetu Khadija Mngwai na Musa Mateja.

Comments are closed.