The House of Favourite Newspapers

‘First Eleven’ Simba Yakunja Milioni 500

KIKOSI cha Simba kikiwa bado kwenye mchakato wa kuimarishwa, imeelezwa kuwa, mpaka sasa wachezaji 11 ambao sawa na idadi ya kikosi cha kwanza ‘first eleven’ waliosajiliwa na kuongezewa mikataba hivi karibuni, wamekunja zaidi ya Sh milioni 500.

 

Kikosi hicho cha Simba ambacho hivi sasa kipo chini ya Kocha Mrundi, Masoud Djuma, baada ya kuondoka Mfaransa, Pierre Lechantre, kinaendelea kufanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Kagame inayofanyika jijini Dar es Salaam.

 

Mpaka sasa, Simba imeshasajili wachezaji wapya saba ambao ni Muivory Coast, Pascal Wawa na Mnyarwanda, Meddie Kagere. Wengine ni wazawa, Adam Salamba, Mohammed Rashid, Abdul Mohammed, Deogratius Munish ‘Dida’ na Marcel Kaheza.

 

Ukiondoa wachezaji hao, wale walioongezewa mikataba ni wanne ambao ni Shiza Kichuya, Mzamiru Yasin, Mohammed Ibrahim na Said Ndemla.

 

Kwa mujibu wa chanzo chetu, wachezaji hao wote katika usajili wao, kila mmoja alikuwa na dau lake, lakini jumla yao ni Sh milioni 535.

 

Ipo hivi; Wawa amesajiliwa kwa Sh milioni 30, Kagere (Sh milioni 115), Salamba (Sh milioni 40), Mo Rashid (Sh milioni 30), Abdul Mohammed (Sh milioni 20), Dida (Sh milioni 50), Kaheza (Sh milioni 30). Hao wote wamesajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili.

 

Waliongezewa mikataba ambao ni Kichuya, alipewa Sh milioni 80, Mzamiru(Sh milioni 50), Mo Ibrahim (Sh milioni 30) na Ndemla (Sh milioni 60).

 

Simba inajiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika inayoanza Novemba mwaka huu ikishirikisha timu ngumu za Misri kama Ismailia na Al Ahly ambazo zinayajua vizuri makali ya Simba.

STORI: SWEETBERT LUKONGE, CHAMPIONI

Comments are closed.