The House of Favourite Newspapers

Simba Kushusha Majembe Mawili Ya Kenya, Zambia

IMEBAINIKA kuwa Simba ina mpango wa kusajili washambuliaji wawili wa kimataifa ili kuongeza nguvu katika kikosi hicho ambapo wachezaji hao wanatajwa kutokea katika nchi za Zambia na Kenya.

 

Mpaka sasa, tayari Simba imefanikiwa kusajili wachezaji wawili wapya wa kimataifa ambao ni Meddie Kagere raia wa Rwanda na Muivory Coast, Pascal Wawa, huku ikiwa kwenye mazungumzo na Mkongo, Kakule Maghuen Fabrice ambaye tayari ametua ndani ya kikosi hicho.

 

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba, kimeliambia Championi Jumatano kuwa, viongozi wapo kwenye mchakato wa kuhakikisha wanakamilisha usajili wa wachezaji hao ambao watasajiliwa moja kwa moja na si kufanyiwa majaribio kutokana na kuwa na viwango bora.

 

Chanzo hicho kilienda mbali zaidi na kudai kuwa lengo la kuwachukua washambuliaji hao ni kuhakikisha wanafanya vyema na ku­funga mabao mengi hasa katika michuano ya kimataifa ambayo msimu ujao Simba itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

“Simba ipo kwenye mpango wa kuongeza wachezaji wawili wa kimataifa na hao wote wanaweza kuwa ni washambuliaji kwa sababu wanataka kuimarisha zaidi safu ya ushambuliaji.

 

“Wachezaji hao watatoka Zambia na Kenya na ni wachezaji wenye viwango na hawatahitaji majaribio, wao watasajiliwa moja kwa moja,” kilisema chanzo hicho.

 

Championi lilimtafuta Kaimu Makamu wa Rais wa Simba, Idd Kajuna ili kuzungumzia ishu hiyo ambapo alisema: “Siwezi kuzun­gumza lolote, kwa sasa nipo kwenye kikao.”

 

Hata hivyo, Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, hivi karibuni aliliambia gazeti hili kuwa: “Tuna mpango wa kuonge­za wachezaji wawili wa kimataifa. Na hii ni baada ya TFF kuongeza idadi ya wachezaji wa kimataifa kufikia 10.”

Comments are closed.