The House of Favourite Newspapers

MKURUENZI KILUWA STEAL GROUP AFIKISHWA MAHAKAMANI

Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiluwa Steal Group. Co.ltd na Kiluwa Free Processing Zone, Mohamed Kiluwa (50) ( wa kwanza mbele kushoto) anayetuumiwa  kutoa rushwa ya Shilingi Milioni 90 kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi.

 

 

 

TAASISI  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imemfikisha kizimbani Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiluwa Steal Group. Co.ltd na Kiluwa Free Processing Zone, Mohamed Kiluwa (50) kwa tuhuma za kudaiwa kutoa rushwa ya Shilingi Milioni 90 kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi.

 

 

Mtuhumiwa huyo amepandishwa kizimbani katika Maakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi na kusomewa shtaka moja la kujihusisha na vitendo vya rushwa.

 

 

Akisomewa shtaka hilo, Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Maghela Ndimbo amedai kwamba mnamo Julai16, mwaka huu kati ya saa 6 na 8 mchana mshtakiwa huyo akiwa Mkurugenzi wa kampuni hizo mbili alitoa rushwa ya Dola za kimarekani 40,000 sawa na Sh. Milioni 90 kwa Waziri Lukuvi.

 

 

Wakili huyo amedai mshtakiwa huyo alitoa fedha hizo kwa lengo la kutowasilisha hati ya umiliki wa kiwanja namba 57 ‘Block B’ na ‘Block D’ kilichopo eneo la viwanda Kibaha mkoani Pwani.

 

 

Baada ya kusoma shtaka hilo, Wakili Ndimbo ameiomba mahakama kuwapangia tarehe ya kutajwa kwa shauri hilo na kwamba  upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na hawana pingamizi kuhusiana na mshtakiwa huyo kupewa dhamana.

 

 

Naye Wakili Upande wa Utetezi, Imani Madega amedai kuwa kwa kuwa upande wa mashtaka hauna pingamizi na dhamana dhidi ya mshtakiwa wanaiomba mahakama itoe dhamana kwa kuzingatia masharti.

 

 

Hakimu Shaidi amesema ili mshtakiwa huyo apate dhamana anatakiwa kuwa na wadhamini 2 na mmoja atoe fedha taslimu mahakamani hapo kiasi cha Sh. Milioni 45 na kama hana awasilishe hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.

 

 

Masharti ambayo upande wa utetezi umeyatekeleza na mshtakiwa akaachiwa kwa dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 15, mwaka huu.

 

Comments are closed.