The House of Favourite Newspapers

JAJI KIONGOZI APEWA ELIMU YA ‘VIDEO CONFERENCE’

Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akiongea jambo katika kikao hicho.
Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akiongoza majadiliano mara baada ya uwasilishwaji wa mada ya mfumo wa ‘Video Conferencing’.
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Beatrice Mutungi (mwenye suti nyeusi) akichangia jambo katika kikao hicho.
Mtaalamu kutoka ‘Invention Technologies’ akiwasilisha mada.
Wajumbe wakifuatilia mada katika kikao hicho.

 

 

 

Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amewasihi Watumishi wa Mahakama kuwa na utayari katika matumizi ya mifumo mbalimbali ya Teknolojia inayoanzishwa Mahakamani ili kuendelea kuboresha  huduma ya utoaji haki nchini.

 

 

Aliyasema hayo Agosti 02, alipokuwa akiwasilishiwa mada juu ya mfumo wa ‘Video Conferencing’ utakavyofungwa na utakavyofanya kazi katika Mahakama husika iliyowasilishwa na Mkandarasi atakayefanya kazi  ya ufungaji wa mfumo wa ‘Video Conferencing’, Kampuni ya ‘Invention Technologies.’

 

“Mahakama yenyewe inatakiwa kuwa tayari kutumia mifumo mbalimbali inayowekwa ili hata Wadau wengine kama Magereza, Polisi waweze kwenda sambasamba na Mahakama katika kuboresha huduma ya utoaji haki,” alisisitiza Mhe. Feleshi.

 

 

Aidha Wajumbe wengine waliohudhuria katika kikao hicho, ambao ni Majaji wawili wa Mahakama Kuu, Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Msajili Mahakama ya Rufani, Mkurugenzi wa TEHAMA-Mahakama, na Maafisa wengineo waliunga mkono juu ya Mahakama kuwa na mfumo huo na kumtaka Mkandarasi kutekeleza kazi hiyo kwa wakati kama alivyoahidi.

 

 

Kwa kuanzia mfumo wa ‘Video Conferencing’ utafungwa maeneo yafuatayo; Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu, Kanda ya Bukoba, Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto na Gereza la Keko.

 

 

Aidha; Mkandarasi anayefanya kazi hii ameahidi kukamilisha kazi hii mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2018.

Kwa sasa mfumo wa ‘Video conferencing’ Mahakamani umefungwa katika Kituo cha Mafunzo-Kisutu pamoja na Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya.

 

 

Mfumo wa ‘Video conference’ Mahakamani utasaidia na utakuwa ni chachu kubwa ya kuharakisha uendeshaji wa mashauri, kupunguza gharama za mashahidi watokao mbalina Mahakama husika na vilevile utasaidia hata katika kuendesha mafunzo mbalimbali ya Watumishi wa Mahakama katika vituo vyao vya kazi.

 

 

Mahakama ya Tanzania kupitia Mradi wa Maboresho ya huduma za Mahakama chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia inaendelea na miradi mbalimbali ya maboresho yote yakiwa na lengo la kuwapa wananchi huduma bora ya upatikanaji wa haki zao.

 

 

 

Picha stori:  Mary Gwera, Mahakama.

 

 

 

Comments are closed.