The House of Favourite Newspapers

Kocha Yanga Adai TFF Wanaipendelea Simba

Mwinyi Zahera.

KOCHA pekee mwenye uraia wa Ufaransa na DR Congo kwenye Ligi Kuu Bara, Mwinyi Zahera anayeinoa Yanga amesema anaona wazi kwamba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linataka kuibeba Simba msimu ujao wa ligi kuu kutokana na ratiba kuwa rafiki kwao.

 

Ratiba ya ligi kuu ambayo imepangwa kuanza kutimua vumbi Agosti 22, inaonyesha Yanga itaanzia ugenini katika michezo yake mitatu ya ugenini ambapo ni dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro itakayopigwa Agosti 23, kisha watakwenda Bukoba kuvaana na Kagera Sugar Agosti 25 halafu Septemba 2, watakwenda Shinyanga kucheza na Mwadui FC.

 

Lakini hata hivyo Yanga baada ya kucheza mechi na Kagera Agosti 23, watalazimika kuanza kujiandaa na safari ya kwenda Rwanda ambapo watakuwa na mechi ya hatua ya makundi ya Shirikisho Afrika dhidi ya Rayon Sports.

 

Simba yenyewe itacheza mechi tatu nyumbani ambazo ni dhidi ya Prisons itakayopigwa Agosti 22, kisha Agosti 25 watacheza na Mbeya City halafu Septemba Mosi watakipiga na Lipuli.

 

Hivi karibuni TFF ilitangaza kuwa timu mwenyeji ndiyo itakayokuwa inachukua mapato yote hali ambayo Yanga wanaona kama wanaonewa kwani hawatopata chochote kwenye mechi hizo.

 

Kutokana na ratiba hiyo, Zahera amesema anaona wazi kuwa TFF inataka kuibeba Simba kwani haiwezekani wao wakapangwa kucheza mechi tatu mfululizo ugenini tofauti na ilivyo kwa Simba na Azam ambao ni wapinzani wao wa karibu ambao wao watacheza mechi tatu nyumbani.

 

“Ni mara ya kwanza kuona kitu hiki kinatokea dunia nzima, huwezi kuanza kucheza mechi tatu ugenini huku wenzako ambao mnapigania kuwania kombe wanaanzia nyumbani.

 

“Hii inaonyesha wazi kuwa TFF inaisaidia timu ya Simba, sijui kwa nini wamefanya hivi inaumiza kwa nini Azam na Simba waanzie nyumbani mechi tatu na sisi ugenini tu, kuna sababu gani,” aliwaka Zahera

Stori na Ibrahim Mressy, Championi Jumamosi

Comments are closed.