The House of Favourite Newspapers

Makambo Mfalme Mpya Yanga SC

Mshambuliaji Mcongo, Heritier Makambo.

STAA wa Yanga kwa sasa ni Papy Tshishimbi, hiyo ni kutokana na kucheza kwa kiwango cha juu kwa muda tangu atue kikosini hapo, lakini inavyoonekana upepo unaelekea kubadilishwa.

 

Hali hiyo inatokana na mazingira ya kikosi hicho wakati huu wa maandalizi ya msimu mpya wa 2018/19 am­bapo mshambuliaji Mcongo, Heritier Makambo, ame­onyesha uwezo mkubwa na ni matumaini kuwa atakuwa nguzo muhimu kikosini kama mambo yakiendelea hivyo.

 

Licha ya uwezo huo, kume­kuwa na mipango kadhaa ya kiufundi kuhusu kumfanya staa huyo kuwa ‘mfalme’ kwenye suala la kutupia mabao.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, tayari ameli­fanyia kazi hiyo na amekuwa akijaribisha kombinesheni ya wachezaji wawili watakao­cheza na straika huyo.

 

Makambo amekuwa ak­ibadilishiwa viungo ili kuona nani na nani wanaweza kumfaa, alianza kupangwa na Faisal Salum ‘Fei Toto’ na Raphael Daudi.

 

Akizungumzia hilo, Zahera alisema: “Bado ninaendelea kutafuta pacha nzuri ya Makambo itakayo­cheza vizuri kwa kuelewana.”

 

Anaitaka rekodi ya Can­navaro

Mara baada ya mechi dhidi ya Kilosa Combine iliyopigwa wilayani Kilosa, nyota huyo alisema kuwa anafurahishwa na upendo wa mashabiki jambo linalomvuta kuitu­mikia klabu hiyo kwa muda mrefu zaidi ya Cannavaro.

 

“Yeye amesema kwenye maisha yake ya soka hajawa­hi kuona mashabiki waka­rimu kama wa hapa Yanga jambo ambalo linamfanya atamani kuzeekea Yanga.

 

“Lakini pia amegundua ukarimu huu ndiyo ulimfanya hata Cannavaro aitumikie timu kwa muda wote wa miaka 12, kwani mapenzi yao yanatia hamasa ya kuende­lea kujisikia ni mtu muhimu ndani ya klabu hiyo,” alisema mtoa taarifa.

 

Awafungukia Waarabu

Baada ya kuruhusiwa kucheza kwenye michuano ya kimataifa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Makambo ameweka bayana kuwa atahakikisha anafanya kitu kwenye mchezo huo wa wik­iendi hii ambao watacheza na Waarabu, USM Alger kutoka Alger.

 

Makambo hakuwa se­hemu ya kikosi cha timu hiyo kilichochapwa mabao 3-2 dhidi ya Gor Mahia ya Kenya hivi karibuni kutokana na kuchelewa kufika kwa kibali chake ambapo kwa sasa kimetolewa na Caf.

 

Mshambuliaji huyo am­baye amechagua kutumia jezi namba 19, amezungum­za na gazeti hili na kusema: “Ni mechi ngumu lakini sisi tunaamini kwa asilimia kubwa tutashinda.

“Ninawaomba mashabiki wajitokeze kwa ajili ya kutupa sapoti kwani wao ni muhimu zaidi na tumeona jinsi am­bavyo wamekuja kwenye michezo yetu ya kirafiki wal­ivyotupa nguvu ya kupam­bana na kupata matokeo.”

 

Kuhusu ligi kuu

“Nimesikia na kuzipata taarifa za mashabiki wa Yanga na kikubwa wana­taka kuona timu yao ikipata mafanikio kupitia mimi katika kuelekea msimu ujao wa ligi.

 

“Niwaambie kuwa, waon­doe hofu mimi nipo pamoja nao, watulie na wasubirie ligi ianze ndiyo wataona makali yangu huku nikiendelea kujifua kuhakikisha ninakuwa fiti.

 

“Ninajisikia furaha kuwepo kwenye timu kubwa kama hii ya Yanga yenye idadi kubwa ya mashabiki ambayo sija­wahi kuiona katika maisha yangu ya soka, hivyo niwaa­hidi kuifanyia makubwa timu yangu mpya ya Yanga,” alisema Makambo.

Waandishi: Wilbert Molandi, Musa Mateja & Said Ally, Championi Jumamosi

Comments are closed.