The House of Favourite Newspapers

Huduma za Mahakama Kuanzishwa Wilaya Zisizo na Huduma Hizo

Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma Bi. Maria Francis Itala ( wa pili  kushoto) akiwa katika Ofisi ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Chemba kufuatilia upatikanaji wa majengo kwa ajili ya uanzishaji wa Mahakama ya Wilaya ya Chemba.
Muonekano wa nje wa jengo lililopendekezwa kwa ajili ya Mahakama ya Wilaya ya Chemba.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma akitoa maelekezo kwa Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Kondoa Bi. Edna Edward Dushi juu ya kuanza zoezi la upandaji wa miti katika eneo hilo ambapo Mahakama ya Wilaya ya Kondoa inajengwa.
Ujenzi wa Mahakama ya  Wilaya ya Kondoa ukiendelea.
Jengo linalotumika sasa na Mahakama ya Wilaya ya Kondoa ambayo inatoa huduma za kimahakama kwa Wilaya ya Kondoa na Chemba.
Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Chemba (kulia) akionyesha eneo la kiwanja kwa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Chemba ambalo linapakana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo.

 MAHAKAMA  Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma imeanza mpango wa uanzishaji wa huduma za kimahakama katika wilaya zisizo na huduma hizo kwa sasa.

 

Viongozi wa mahakama katika kanda hii wameanza kufuatilia na kukutana na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba na Chamwino ili kupata maeneo ambayo yatatumika na mahakama za wilaya katika kipindi ambacho mpango wa kujenga hizo unafanyiwa kazi.

 

Utekelezaji huu unafuatia agizo la Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania juu ya kufanya jitihada ya kuwa na mahakama hizo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

 

Katika mazungumzo waliyofanya katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo,  ilibainika kuwa huduma ya kimahakama inahitajika sana kwa sasa katika eneo hilo kutokana na umbali mrefu uliopo kufikia eneo ambalo huduma za mahakama ya wilaya zinapatikana kwa sasa (Kondoa).

 

Baada ya mazungumzo hayo viongozi wote wa pande mbili walitembelea na kuona eneo ambalo ofisi ya mkurugenzi imetenga kwa ajili ya matumizi ya mahakama na taasisi nyingine muhimu ambazo hazipo kwa sasa katika Wilaya hiyo.

 

Sambamba na hilo, viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino  walionyesha uhitaji mkubwa wa uanzishaji wa mahakama ya wilaya katika eneo hilo na wameahidi kutoa ushirikiano mkubwa ili kuhakikisha huduma hiyo inaanzishwa mapema katika wilaya hiyo.

 

Aidha kwa sasa wanafanya jitihada za kuhakikisha jengo linapatikana ili kuanzisha huduma hiyo muhimu kwa wananchi wa Wilaya ya Chamwino.

 

Katika zoezi la ufuatiliaji wa suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Wilaya ya Chemba ambayo inahudumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Kondoa kwa sasa, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Maria Francis Itala,  na maofisa wengine wealiambatana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Arnold John Kirekiano, ambapo walitembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Kondoa ambao umefikia hatua ya uezekaji wa paa na shughuli za kukamilishwa kwake zikiwa zinaendelea vizuri.

 

Mahakama ya Tanzania kupitia mpango mkakati wake wa miaka mitano 2015/2016 – 2019/2020 hususani nguzo ya pili ya mpango mkakati huo,  inalenga kusogeza huduma za mahakama kwa wananchi kwa kuhakikisha huduma hizo zinafikika kwa urahisi kwa maeneo yote nchini.

 

Na Stanslaus Makendi, Mahakama Kuu Dodoma.

 

 

 

 

 

Comments are closed.