The House of Favourite Newspapers

Wilaya ya Nzega yakabiliwa na changamoto ya Uharibifu wa Mazingira

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Ngukumo, Kata ya Nkiniziwa Wilayani Nzega, Mkoani Tabora kuhusu changamoto kubwa inayokabili Kijiji hicho  ya ukataji ovyo wa rasilimali za misitu. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Mazingira ya Kijiji cha Ngukumo na kuwakumbusha wajibu wao katika kusimamia mazingira. 
Makamba akimwagilia mti baada ya kuupanda.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akipanda mti kuunga mkono jitihada za upandaji miti kwa wakazi wa Kijiji cha Nkiniziwa. Mti huo pia ameukabidhi kwa mtoto Masoud Maganga ili aweze kuutunza kama kielelezo cha kutunza mazingira.

 

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwambaha, Wilayani Nzega wakijibu maswali mbalimbali ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba mara baada ya kutembelea Shule hiyo kupanda miti na kuimarisha Club ya Mazingira Shuleni hapo kwa kuiwezesha kuanzisha kitalu cha miche ipatayo Elfu tano.

 

 

Changamoto kubwa inayoikabili Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora ni uharibifu mkubwa wa mazingira utokanao na uvunaji holela wa rasilimali za misitu na shughuli za kilimo.

 

 

Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Nzega Bw. Godfrey Ngukuwa wakati akiwasilisha taarifa ya Wilaya yake kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba katika Kijiji cha Ngukumo na Mwambaha, Wilayani Nzega.

 

“Wilaya yetu imekuwa na ongezeko kubwa la wavamizi kutoka Mikoa jirani wanaojihusisha na shughuli za ukataji miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na kilimo kisichoendelevu, kwa kiasi kikubwa wanachangia uharibufu wa Mazingira, kwa kuwa hivi sasa Nzega imekuwa soko la Mkaa kwa Shinyanga na Mwanza” alisisitiza Bw. Ngukuwa

 

Akielezea jitihada zilizofanywa na Ofisi yake Bw. Ngukuwa amesema kuwa doria za mara kwa mara zianaendelea Kijiji hapo kwa kushirikiana na wananchi wenyewe kubaini wavamizi hao.

 

Naye Waziri mwenye dhamana ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Nchini Mhe. January Makamba amewataka wakazi wa vijiji hivyo kuwa wakali kwa rasilimali zao na kuhakikisha mazingira kwa ujumla wake yanatunzwa kwa sheria kali zaidi.

 

 

Pia, ameagiza kufanyika kwa operesheni kali na kuwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na uharibifu huo. “Ndugu zangu sina budi kuwakumbusha kuwa siku hizi kuna wakimbizi wa Mazingira, watu wanaharibu mazingira katika maeneo yao na kuhamia maeneo mengine, jitihada za maendeleo zote hazitakuwa na maana kama hatutatunza mazingira” Makamba alibainisha.

 

Waziri Makamba amewaeleza wakazi wa Vijiji vya Ngukumo na Mwambaha kuwa na uhifadhi wenye tija ni ule ambao wananchi wako tayari kushiriki kwa nguvu zote. Katika kuunga mkono shughuli za maendeleo, Waziri Makamba amechangia kiasi cha Shilingi Milioni Moja kwa ajili ya Ujenzi wa Zahanati na matundu ya Choo katika Shule ya Msingi Mwambaha.

 

Waziri Makamba amehitimisha ziara yake Mkoani Tabora na amewasili Mkoani Geita ambapo atatembelea Kisiwa cha Magafu.

Comments are closed.