Mnaokwenda Simba, Rudisheni Matumbo Yenu Nyuma
GUMZO la uchaguzi wa Simba limekuwa si kubwa sana, kwa kiasi fulani linaonekana kupunguzwa na kasi ya masharti kutoka katika katiba mpya.
Uchaguzi mkuu wa Simba ambao umepangwa kuchagua viongozi kwa mara ya kwanza chini ya mfumo mpya wa uwekezaji, utafanyika Novemba 3, mwaka huu.
Sote tunajua, katiba mpya ya Simba imewabana baadhi ya viongozi wa klabu hiyo kushiriki.
Mambo mawili yamewaengua baadhi ya viongozi kushiriki. Elimu halafu suala la umri kwani inaonekana mwenye umri kuanzia miaka 65, haruhusiwi kushiriki.
Hii imewafanya baadhi yao kushindwa kuingia, hasa wale maarufu ambao tumekuwa tukiwajua na walikuwepo ndani ya Simba.
Lakini pia, suala la elimu, suala la shahada au digrii pia limekuwa kikwazo kwa wengi hasa waliotaka kuwania nafasi ya mwenyekiti wa klabu hiyo.
Haya mambo mawili kwa kiasi kikubwa, yamesababisha ukimya na hali ya utulivu. Kama unakumbuka mwanzoni ilikuwa ni vigumu kwa wengi kujitokeza.
Baada ya kelele za hapa na pale, baadhi wakaanza kujitokeza huku ikionekana bado kuna ugumu.
Kama mdau wa mpira Tanzania na hasa kwa wale wanaotaka kuona maendeleo, nilieleza wazi ambavyo nilikuwa nikiamini itakuwa sahihi na hasa suala la kuhusiana na watu wengi kujitokeza na pia wajitokeze ambao watakuwa wamelenga kusaidia maendeleo ya Klabu ya Simba.
Simba ambayo inakwenda katika mfumo mpya, kwani kuunda bodi ya wakurugenzi, itawakutanisha upande wa klabu na upande wa mwekezaji. Lazima upande wa mwekezaji utakuwa na watu makini.
Hivyo ni lazima upande wa klabu nao uwe na watu makini wanaoeleweka na wenye nia ya kuikomboa klabu hiyo badala ya matumbo yao au kuangalia mwekezaji pekee anataka nini.
Mjadala wangu wa leo unaanzia hapo. Kwamba wakati wale wanaokwenda kuwania uongozi tunaamini ni watu imara, basi niwakumbushe tena kwamba wanapaswa kurudisha matumbo yao nyuma ili watangulize mioyo yenye nia njema ya kuisaidia Simba kubadilika na kupata maendeleo zaidi, jambo ambalo limekuwa kilio cha milele.
Kilio cha maendeleo kinaonekana kukosa namna njema kwa kuwa viongozi wengi wameingia kuongoza klabu wakiwa wamelenga zaidi kujisaidia au kujifaidisha wao.
Nataka nieleweke, sijasema waliopo sasa wanataka kujifaidisha. Ila wapo waliowahi kujifaidisha na huenda wamerejea kwa kuwa wamejirekebisha.
Sasa tunataka kuwakumbusha mapema kabisa kuhusiana na hilo kuwa maendeleo ya Simba yatapatikana kwa nia njema na wale waliolenga kuisaidia klabu hiyo.
Kama wanaoingia kugombea uchaguzi wa Simba na waliwahi kuongoza, halafu kukawa hakuna mafanikio. Naamini hawa ni wazuri na watakuwa wana jambo jipya wanataka kurudi nalo.
Lakini lazima tukubali, pamoja na hivyo nao wanapaswa kujua Simba ni ya watu na wanapaswa kubadilika na watakapopata nafasi basi wafanye kile ambacho kinakusudiwa na wengi.
Haitakuwa sahihi kuwa na viongozi fuata mkumbo, viongozi fuata upepo au viongozi walio tayari kutekeleza yale ambayo yanaweza kuwafaidisha wao na watu wao.
Badala yake wawe viongozi imara, si kwa kupinga kila kitakachotolewa na upande wa mwekezaji. Badala yake wale ambao wanataka Simba iendelee na wao kubaki kwenye rekodi na historia kupitia mabadiliko waliyoyafanya.
Simba haitapiga hatua kama wanaoiongoza nia yao haitakuwa njema. Kama Simba itashindwa kupata mafanikio katika mabadiliko ya sasa, hakuna maana ya mabadiliko hayo, na hakuna klabu itaona kuwa mabadiliko yana manufaa.
Kuna kila sababu ya kuliona hili mapema na kama wewe ni kiongozi unaona unataka kutanguliza tumbo, basi mapema ukae kando. Kama unaona nia yako ni kujifaidisha, imetosha. Waachie wenye nia nzuri na wewe unaweza kufanya mambo yako mengine.
Comments are closed.