The House of Favourite Newspapers

Simba Yajichimbia Ufukweni Ili Kuimaliza Yanga

Wachezaji wa simba wakiwa mazoezini.

KIKOSI cha Simba leo jioni kinaingia kambini kujiandaa na mchezo wa Jumapili wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Kambi hiyo ya Simba ya kujiandaa na mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa soka hapa nchini, itakuwa katika Hoteli ya Sea Scape iliyopo Mbezi Beach jijini Dar es Salaam karibu kabisa na ufukwe wa Bahari ya Hindi.

 

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba ambazo Championi Jumatano limezipata zimedai kuwa, uamuzi huo wa Simba kubakia Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo, umetokana na maelekezo ya kocha mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems.

“Awali uongozi ulipendekeza kuwa twende kisiwani Unguja kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo, lakini kocha amekataa, hivyo kambi yetu itakuwa palepale Sea Scape ambapo tumekuwa tukipiga kambi yetu kila siku.

 

“Sababu ya kocha kugoma kwenda Unguja ni kile alichodai kuwa, mechi hiyo haina tofauti na zile ambazo imecheza ikitokea katika kambi hiyo kwa hiyo haina haja ya kwenda mbali,” kilisema chanzo hicho cha ha habari na kuongeza:

 

“Mazoezi yetu yatakuwa yakifanyika katika Uwanja wa Boko Veterani na tutaanza kesho (leo) jioni, baada ya mazoezi hayo timu itaingia kambini.”

 

Alipoulizwa Aussems kuhusiana na hilo hakuwa tayari kusema chochote, lakini walipotafutwa viongozi wa Simba ili waweze kuzungumzia hilo, hawakuweza kupatikana.

 

Hata hivyo, hiyo itakuwa ni mara ya pili kwa Simba kutotoka nje ya Dar es Salaam kujiandaa na mechi yake dhidi ya Yanga katika miaka ya hivi karibuni, baada ya kufanya hivyo msimu uliopita katika mechi yake ya mzunguko wa pili ilipokuwa chini ya Mfaransa, Pierre Lechantre.

Stori na Sweetbert Lukonge, Championi Jumamosi

Comments are closed.