The House of Favourite Newspapers

Prof. Ndalichako Akutana na Ugeni Kutoka Canada, Finland Wazungumzia Elimu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako alipokutana na Mkuu wa DFID nchini,  Beth Arthy,  jijini  Dar es Salaam leo kujadili masuala  ya  elimu.
…Akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Afrika Mashariki na Kusini wa Canada, Mars Andre Fredette (kushoto) na Balozi wa Canada nchini Tanzania,  Pamela O Donnell.

 

SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia zimekubalina kuendelea kuimarisha programu za  Mpango wa Elimu kwa Walioikosa (MEMKWA) na Mpango wa Elimu Jumuishi baada ya Kumaliza Elimu ya Msingi (IPPE), ili kuwawezesha wanafunzi wanaokatisha masomo kabla ya kumaliza shule waweze kuendelea na masomo yao.

 

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Afrika Mashariki na Kusini wa Canada, Mars Andre Fredette, aliyeambatana na Balozi wa Canada nchini, Pamela O Donnell,  ambapo wamejadili masuala mbalimbali ya kuendelea kuisaidia Tanzania katika  sekta ya elimu.

 

Ndalichako amesema nia ya serikali ni kuona kila mtoto nchini anayepaswa kupata elimu anaandikishwa na kubaki shule mpaka anapomaliza masomo yake ingawa kumekuwepo na changamoto ya baadhi wa wanafunzi kukatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali.

 

“Ukitembea barabarani unakutana na watoto wadogo wakifanya biashara ndogondogo unapoongea nao wanakwambia wameacha shule ili kusaidia wazazi kufanya biashara hizo, wengine utawakuta wapo mashambani wanawasaidia wazazi kulima hivyo changamoto ya watoto kukatisha masomo ni kubwa, na ndiyo maana serikali inaona namna bora ya kuhakikisha wale wote wanaokatisha masomo wanajiendeleza,”alisisitiza.

 

Amesema programu ya MEMKWA inamwezesha mtoto ambaye hakwenda shule kabisa kusoma na kisha kufanya mtihani wa darasa la nne na baadaye anapofaulu huandikishwa katika  mfumo rasmi na kuendelea na masomo kama wanafunzi wengine wakati mfumo wa IPPF ni kwa ajili ya wanafunzi wanaokatisha masomo ya sekondari  unawawezesha kumaliza masomo hayo na kuendelea na elimu juu.

 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Afrika Mashariki na Kusini kutoka Canada, Mars Andre Fredett,  amesema Canada inajivunia uhusiano wa muda mrefu uliopo katika ya Tanzania na Canada ambao umewezesha nchi kupata misaada mbalimbali ya kuendeleza sekta ya elimu ambayo imewezesha watoto wa kike na kiume kupata elimu bora pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu.

 

 

Ndalichako pia amefanya mazungumzo na Balozi wa Finland nchini,  Pekka Hukka,  na Mkuu wa Kitendo cha Maendeleo Kimataifa  (DFID) nchini, Beth Arthy,  ambapo wamezungumzia masuala mbalimbali ya namna bora ya kuboresha elimu nchini ikiwepo masuala ya kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu bora kwa kila mtoto wa Tanzania.

 

 

Comments are closed.