Zahera Amkimbiza Kiungo Yanga
KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Martin ameondoka kwenye timu hiyo na kwenda kujiunga na Ruvu Shooting katika usajili huu wa dirisha dogo la usajili.
Hiyo, ikiwa ni siku mbili zimebaki kabla ya usajili wa dirisha dogo kufungwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Martin alijiunga na Yanga katika msimu wa 2016/2017 akitokea JKU inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar akisaini mkataba wa miaka miwili.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, kiungo huyo mkataba wake umemalizika tangu mwezi Novemba kabla ya uongozi kusitisha mpango wa kumuongezea mkataba mwingine.
Mtoa taarifa huyo alisema sababu iliyosababisha kiungo huyo kutoongezewa mkataba ni baada ya kushindwa kumshawishi kocha mkuu wa timu hiyo Mkongoman, Mwinyi Zahera.
“Martin rasmi siyo mchezaji wa Yanga na tayari amesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea Ruvu Shooting baada ya kufikia makubaliano ya kuondoka Jangwani.
“Anaondoka Yanga baada ya mkataba wake kumalizika na viongozi kusitisha mpango wa kumuongezea mwingine kutokana na kocha kutoonekana kumhitaji.
“Kabla ya kuondoka, Martin aliulizia hatma yake kwa viongozi wa Yanga akaona kimya, hivyo katika kujinusuru akaona aondoke zake Ruvu,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Martin kuzungumzia hilo alisema: “Nipo katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wangu huku Ruvu Shooting ni baada ya kuona viongozi wa Yanga wapo kimya.
“Nikiri mkataba wangu kumalizika, hivyo ninakwenda huko Ruvu kwa ajili ya kupata nafasi ya kucheza baada ya Yanga kutopata kwa muda mrefu, hivyo ninaamini nikiwa huku nitakirejesha kipaji changu,” alisema Martin.
STORI: Wilbert Molandi
Comments are closed.