The House of Favourite Newspapers

POGBA APIGA MBILI TENA MAN U IKIUA

Paul Pogba akishangilia

NI mechi ya tatu kwa kocha mpya, Ole Gunnar Solskjaer na ni ushindi wa tatu mfululizo kwa Manchester United kwenye Premier. Lakini Paul Pogba kazaliwa upya, kwani jana alipiga mabao mawili wakati Manchester United ilipoichapa Bournemouth 4-1 kwenye Uwanja wa Old Trafford. Sasa Pogba kapiga mabao mawili katika mechi mbili mfululizo. Alifunga mabao mawili dhidi ya Huddersfield na jana karudia tena.

 

Kabla ya hapo, katika mchezo wa kwanza wa Solskjaer dhidi ya Cardiff alitoa asisti mbili. Bao jingine la Man United lilifungwa na Marcos Rashford dakika ya 44 na Romelu Lukaku akafunga dk ya 72, zikiwa ni dakika mbili tu baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Rashford, na sasa United wamefunga mabao 12 katika mechi tatu zilizopita wakionekana hawashikiki chini ya Solskjaer.

Bao la Bournemouth lilifungwa na Nathan Ake
sekunde chache kabla ya mapum ziko. Mashabiki wa Manchester United sasa wanaamini timu yao imerudi, na tayari ipo katika nafasi nzuri ya kutinga top 4, ikiwa sasa imezidiwa na Arsenal iliyo nafasi ya tano kwa pointi tatu tu.

Dakika ya 79, Eric Bailly alipewa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kucheza rafu mbaya, atakosekana katika mechi mbili zijazo. Kwenye mchezo wa mapema, Chelsea iliongeza pengo lake la pointi dhidi ya Arsenal, baada ya jana Jumapili kuwachapa wabishi walioitungua Man City, Crystal Palace bao 0-1 ugenini.

 

Bao hilo pekee la Chelsea lilifungwa na Mfaransa N’Golo Kante dakika ya 51. Matokeo hayo yanaifanya Chelsea ibakize pointi mbili tu kabla ya kuifikia Tottenham katika nafasi ya tatu.

Katika mchezo wa jioni, Manchester City ikiwa na urejeo wa kiungo wake Fernandinho ilirudi kwenye mbio za ubingwa baada ya kuichapa Southampton 1-3 ugenini, shukurani kwa mabao ya David Silva na Sergio Aguero huku Ward-Prowse akijifunga kwa upande wa Southampton ambao kipigo hicho kimewafanya wadidimie hadi nafasi ya nne kutoka chini. Awali, Southampton waliwapa hofu Man City baada ya kusawazisha bao la Silva, lakini City wakafunga mabao mengine mawili kabla ya mapumziko.

Comments are closed.