The House of Favourite Newspapers

Zamalek wamtengea Kagere mil 919

Mshambuliaji hatari wa Simba, Meddie Kagere.

 

WAPINZANI wa Al Ahly ya Misri, Zamalek wameingilia kati ishu ya kutaka kumsaini mshambuliaji hatari wa Simba, Meddie Kagere na wapo tayari kumwaga mamilioni.

 

Hivi karibuni klabu kadhaa kutoka nchi za Kiarabu kama Raja Casablanca ya Moroco zilitajwa kumuwania mshambuliaji huyo aliyejiunga Simba msimu huu akitokea Gor Mahia.

 

Hivi karibuni uongozi wa Raja Casablanca ulikutana na wakala Kagere, Patrick Gakumba na kumwambia kuwa umetenga dau la dola 400,000 ambazo ni sawa na Sh 919,068,000 kwa ajili ya kumsajili mchezaji huyo ambaye alijiunga na Simba msimu huu akitokea GorMahia ya Kenya.

 

Sababu kubwa ya kufikia uamuzi huo ni kutokana na kuvutiwa na uwezo wake ambao amekuwa akiuonyesha uwanjani tangu alipojiunga na Simba na kuweza kufanya vizuri katika michuano ya Ligi Kuu Bara na pia katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Katika ligi kuu, Kagere amefanikiwa kufunga mabao 12 sasa wakati kwenye Ligi ya Mabingwa katika mechi za hatua ya makundi ametupia mabao matatu na ukihesabu hadi yale ya mtoano basi anayo sita.

 

Hata hivyo, juzi Alhamisi uongozi wa Zamalek ya Misri ulikutana na Gakumba nchini humo na kuzungumza naye mambo mengi kuhusiana na Kagere.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Gakumba alisema kuwa, Zamalek wametangaza kitita cha dola 400,000 kama kile ambacho Casablanca wamekitenga kwa ajili ya kuhakikisha wanasajili mchezaji huyo.

 

“Hivi sasa tunavyoongea nipo nchini Misri kuna wachezaji wawili nimewaletea Zamalek kwani waliniambia niwatafutie, lakini pia katika mazungumzo wameniambia kuwa wanamuhitaji Kagere na wapo tayari kutoa kitita cha dola 400,000 na mshahara wa dola 10,000 (Sh mil 23.3) kwa mwezi.

 

“Lakini nimewaambia kuwa kwa sasa kumpata mchezaji huyo itakuwa ni ngumu kidogo kutoka na kuwa na mkataba na Simba na wao hawapo tayari kumwachia kwa sababu ni msaada mkubwa kwao.

 

“Hata hivyo nimewaomba kama kweli wanamuhitaji basi wawe wavumilivu, mkataba wake utakapomalizika basi huo ndiyo utakuwa muda mzuri kwao kumpata kwani wanatakiwa kuwa na mkwanja wa kutosha sababu anawindwa na timu nyingi,” alisema Gakumba.

Stori: SweetbertLukonge, Dar es Salaam

Comments are closed.