The House of Favourite Newspapers

Usajili wa Makusu wa AS Vita Kutua Yanga

MASHABIKI wa Yanga wanamtamani, straika wa AS Vita, Jean Makusu lakini Kocha Mwinyi Zahera amewaambia hata wasihangaike kwa vile ni kazi bure. Zahera amekwenda mbali zaidi kwa kusema kwamba hata hao Simba wanaomnyemelea hawawezi kumpata kwavile hawezi kuja Tanzania kwa namna yoyote ile.

 

Kocha huyo akizungumza kwenye ofisi za Spoti Xtra zilizopo Sinza Mori, Jijini Dar es Salaam hivi karibuni, alisema kwamba atakuwa muongo kama akiwapa matumaini mashabiki ya kumpata mchezaji huyo ghali.

 

Zahera anamnoa mchezaji huyo kwenye timu ya Taifa ya DR Congo na Spoti Xtra linajua ni miongoni mwa
marafiki zake wakubwa. Kocha huyo alisema kwamba hata akilipwa Dola 30,000(Sh.70 Milioni) hawezi kuja Tanzania kwa vile miundombinu na vitu vingi ni vya hovyo.

 

“Leo hii nikisema namuhitaji Makusu katika kikosi changu nitakuwa muongo hata kama ni mwakani haitawezekana sababu hatuna fedha za kusajili na aweze kuja hapa Tanzania hata Simba na wakimtaka hawezi kuja.

 

“Halafu mimi ninamfahamu vizuri Makusu hawezi kukubali kuja kucheza huku Tanzania kwenye viwanja hivi vibovu eti akacheze huku sijui Singida mnaweza kumpa hata dola 30,000 akachukua na asije.

 

“Hatakuwa tayari kuona anaumia au anasafiri kwa masaa mengi na basi kwenda kucheza huku mikoani sidhani kama anaweza kuja,”alisema Zahera ambaye mashabiki wa Simba wanamlaani kwa madai kwamba amewasaidia AS Vita kwenye mechi ya jana usiku.

 

Makusu ni miongoni mwa wachezaji nyota wanaocheza ligi ya ndani ya Congo maarufu kama Linafoot na habari za ndani zinadai kwamba tayari ameshaingia makubaliano na klabu moja ya Morocco na huenda akajiunga nayo baadae mwaka huu.

 

Habari zinasema kwamba AS Vita wameshamalizana na klabu hiyo lakini bado hawajaweka mambo hadharani ila Zahera ameshaambiwa ukweli na Kocha wa Vita, Florent Ibenge ambaye wanaishi nae mtaa mmoja Ufaransa na ni bosi wake timu ya Taifa.

 

Ibenge amewaambia Simba kwamba kama wakimsajili Makusu yeye atamchukua Meddie Kagere kwa dau lolote lile. Zahera tangu atue Yanga alimsajili kipa Klaus Kindoki na straika Heritier Makambo na wote kutoka DR Congo.

 

Kwa mujibu wa mtandao unaohusika na ishu za usajili duniani wa Transfer Markt wa Ujerumani, thamani ya Makusu ni zaidi ya Sh.357milioni. Thamani hiyo inatokana na umri mdogo wa mchezaji huyo ambao ni 26 pamoja na ufanisi wake.

Comments are closed.