The House of Favourite Newspapers

Simba: Tunamaliza mchezo Taifa

UONGOZI wa Klabu ya Simba umefunguka kuwa unataka kuwamaliza TP Mazembe hapa nyumbani ili iwe rahisi kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Kauli hiyo imekuja wakati kesho Jumamosi timu hizo zikitarajiwa kupambana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, kisha zitarudiana Aprili 13, kule
Lubumbashi, DR Congo.

 

Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, ameliambia gazeti hili kuwa wanataka kuimaliza mechi hiyo jijini Dar, ili iwe rahisi wakienda ugenini na kuvuka hatua hiyo ya robo fainali.

Simba itavaana na mabingwa hao wa Ligi ya Mabingwa mara tano Afrika katika robo fainali ya michuano hiyo ambayo Simba imeweza kufika hatua hiyo kwa miaka ya hivi karibuni.

 

Magori alisema wanahitaji ushindi hapa nyumbani na kusisitiza kuwa mashabiki wa Simba na Watanzania kwa jumla wajitokeze kwenda kuwasapoti sababu utakuwa ni mchezo mgumu.

 

“Tunataka kuimaliza hii mechi hapa nyumbani kwa kuondoka na ushindi wa nguvu ili ikawe rahisi hata kwenye ule mchezo wa marudiano ambao tutakuwa ugenini kule Lubumbashi.

 

“Mazembe si timu ndogo, hilo linafahamika, wale ni mabingwa wa Afrika mara kadhaa, hivyo kwetu hautakuwa mchezo rahisi ndiyo maana tumejipanga kuona timu inaweza kufanya vizuri hapa nyumbani kwanza,” alisema Magori.

 

Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi bora ya kutopoteza kwenye Uwanja wa Taifa baada ya kuzifunga timu tano kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika, waliifunga Al Ahly bao 1-0, AS Vita Club (2-1), JS Saoura (3-0), Nkana (3-1) na Mbabane Swallows (4-1).

NA Martha Mboma, Dar es Salaam

Comments are closed.