The House of Favourite Newspapers

Yanga Yabeba Kombe Moro, Yaipiga Mawenzi Market 1-0

YANGA imeendeleza wimbi la ushindi kwa asilimia mia moja katika mechi zake za maandalizi ya msimu baada ya jana Jumapili kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mawenzi Market.

 

Katika mchezo huo wa jana uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, bao la Yanga lilipatikana dakika ya 79 likifungwa na Issa Bigirimana aliyeunganisha krosi ya Deus Kaseke.

Hilo linakuwa ni bao la pili kwa Bigirimana katika mechi za maandalizi. Mchezo huo ulikuwa maalum kwa ajili ya Tamasha la Faith Baptist Church Morogoro. Timu hiyo ambayo Julai 7, mwaka huu ilikimbilia Morogoro kuweka kambi ya maandalizi ya msimu ujao wa 2019/20, mpaka sasa imecheza jumla ya mechi tano za kirafiki na kushinda zote.

 

Mechi ya kwanza ilianza kwa kuifunga Tanzanite mabao 101, ikaifunga Moro Kids 2-0, Moro Athletics Academy ikafungwa 7-0, Mwere Academy wakafungwa 3-0, kabla ya jana kuichapa Mawenzi 1-0.

Timu hizo zote ni za mkoani Morogoro. Baada ya ushindi katika mchezo huo wa jana, Yanga ilikabidhiwa kombe maalum na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, huku Mrisho Ngassa akikabidhiwa zawadi kutokana na kuibuka mchezaji bora wa mchezo huo.

 

Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, ambaye amechelewa kufika kambini kutokana na ruhusa maalum, jana aliwasili na kuingia kambini moja kwa moja huku Championi likimshuhudia.

Wakati anafika kambini, aliwakuta wachezaji wakijiandaa kwenda uwanjani kucheza mechi hiyo, akawasalimia na kuachana nao huku akiwaahidi watakutana uwanjani.

Alipoingia uwanjani, aliomba kukaa jukwaani ili awashuhudie vijana wake vizuri kabla ya kuanza rasmi kuwanoa katika maandalizi yao ya mwisho kabla ya msimu kuanza. Muda wote wa mchezo huo, Zahera alionekana kuwa bize kuwafuatilia vijana wake huku akitikisa kichwa kuonekana amekubali uwezo waliouonyesha.

(HABARI NA PICHA NA MUSA MATEJA, MOROGORO, GPL)

Comments are closed.