The House of Favourite Newspapers

Waziri Wa Mambo Ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni, Akabidhi Mitungi 700 Ya Gesi

0
Waziri wa Mambo ya Ndani Mhandisi Hamad Yusuf Masauni (wa pili kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman (wa kwanza kushoto) wakimkabidhi mtungi wa kupikia wa gesi ya Orxy Hudhaima Shaban Sururu katika hafla ya ugawaji wa mitungi 700 ya kupikia ya Oryx kwa baba lishe na mama lishe Machi 13, 2024 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Visiwani Zanzibar.

KATIKA muendelezo wa utekelezaji wa mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia uliozinduliwa na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amekabidhi mitungi 700 ya gesi ya kupikia iliyotolewa na kampuni ya Oryx Gas Tanzania.

Akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji wa mitungi hiyo iliyoambatana na semina juu ya matumizi sahihi ya gesi ya kupikia, aliwataka wananchi wa jimbo la Kikwajuni, Masauni aliwataka wananchi hao kuunga mkono mkakati huo kwani una faida kiafya, kiuchumi na kijamii.

Waziri wa Mambo ya Ndani Mhandisi Hamad Yusuf Masauni akizungumza katika hafla ya ugawaji wa mitungi 700 ya kupikia ya Oryx kwa baba lishe na mama lishe Machi 13, 2024 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Visiwani Zanzibar.

Alieleza kuwa matumizi ya gesi mbali ya kuokoa muda katika mapishi, huondoa matumizi ya kuni na mkaa hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa athari za mabadiliko ya tabia nchi.

“Agenda ya nishati  safi ya kupikia ni muhimu kiuchumi wa familia kwani mbakibya kuepusha madhara ya kiafya kama ilivyoelezwa na wataalamu pia huokoa miti ambayo husaidia kupunguza joto ambalo ni miongoni mwa athari za mabadiliko wa tabia nchi”, alieleza Mhandisi Masauni ambaye pia ni Mbunge wa jimbo hilo.

Aidha aliupongeza uongozi wa kampuni ya gesi ya Oryx kwa kuunga mkono mkakati huo na kuwapatia wananchi jimbo hilo ili kubadilisha maisha yao.

Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman akizungumza katika hafla ya ugawaji wa mitungi 700 ya kupikia ya Oryx kwa wananchi wa Jimbo la Kikwajuni wakiwemo Mama na Baba lishe katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Visiwani Zanzibar.

“Tunawapongeza kwa kutupatia watu wa Kikwajuni mitungi hii ambayo itawasaidia wananchi wetu kuimarisha maisha yao na ningeomba sisi tuliopatiwa mitungi hii tuwe mabalozi wa kuhamasisha matumizi ya gesi lakini pia kuitangaza kampuni hii kama njia ya kurudisha shukrani kwao”, alieleza Masauni.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania, Benoit Araman, alieleza kuwa kampuni yake imeibeba ajenda hiyo kwa kutekeleza miradi mikubwa nchini Tanzania hasa Zanzibar ili kuwanufaisha wananchi wa maeneo mbalimbali.

Akitaja faida za kutumia gesi ya kupikia ya Oryx, Araman alieleza kuwa ni pamoja na kuondoa hatari za kiafya kwa watumiaji wa wa kuni na mkaa kama nishati ya kupikia lakini pia hatari za kimazingira na ustawi wa jamii.

“Takribani watu 33,000 wanapoteza maisha nchini Tanzania kwa maradhi yanayotokana na kuvuta moshi unaotokana na mkaa au kuni hiyo ndio sababu ya Oryx gas kuja na suluhisho la kuwahamasisha wananchi kutumia gesi kwa matumizi ya kupikia”, alieleza Araman.

Aliongeza kuwa matumizi ya gesi yanaepusha wamama na watoto kuumika kubeba kuni  hivyo kuepuka kujeuriwa na wanyama wakali wakiwa katika harakati za kutafuta kuni pia kuimarisha maisha ya wanawake na kuwalinda dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.

“Kuanzia mwezi wa saba mwaka 2021 tumekuwa mstari wa mbele kuunga mkono utekelezaji wa mkakati wa serikali uliopewa nguvu na Raisi wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania , Dk. Samia Suluhu Hassan kwa lengo kwamba ifikapo mwaka 2033 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia”, alieleza Araman.

Nae Katibu Tawala wa wilaya wa wilaya ya Mjini Unguja, Dk. Said Haji Mrisho, alieleza kuwa serikali inafanya jitihada mbali mbali kuwawezesha wananchi kutumia nishati mbadala ya kupikia hivyo aliwapongeza Oryx Gas kwa msaada wanaoutoa katika kubadili mitazamo ya jamii juu ya matumizi ya gesi safi ya kupikia.

Alieleza kuwa mipango ya kampuni hiyo kutokomeza matumizi ya nishati ya kuni na mkaa ambayo ina madhara ya afya inapaswa kuungwa mkono na kuwahimiza wananchi wa wilaya hiyo kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Leave A Reply