The House of Favourite Newspapers

Hawa Ndiyo Vijana 5 Wanaotikisa kwa Mkwanja Duniani

zuckerberg-at-mobile-world-congressBado kuna watu hawaamini kama mtu anaweza kuwa bilionea akiwa na miaka midogo. Wanachokiamini ni kwamba ili uwe bilionea, ni lazima ujanani upambane sana na mafanikio yanakuja kupatikana ukiwa na miaka hamsini, ndugu yangu, kama ulikuwa ukifikiri hivyo, umekosea sana.

Kuna vijana wanatengeneza pesa kwa sasa, wana umri mdogo lakini akaunti zao benki zimenona ile mbaya. Achana na mabilionea wenye umri mkubwa kama Bill Gates, Carlos Slim na wengineo, hebu cheki mabilionea vijana ambao wanaogelea katika mabwawa yaliyojaa pesa.

evan_spiegel_at_techcrunchEvan Spiegel

Huyu jamaa ni Mmarekani, ana umri wa miaka 25 tu. Ni Mmarekani aliyezaliwa Los Angeles, California huko nchini Marekani. Mara baada ya kusoma katika Shule ya Crossroads, akamalizia elimu yake katika Chuo cha Stanford kilichokuwa hukohuko nchini Marekani.

Baada ya kuona mitandao ya kijamii ikishika kasi, akamuita mshikaji wake, Bobby Murphy na kumpa wazo la kutengeneza mtandao wa kijamii, wazo hilo likaonekana kufaa hivyo kutengeneza Mtandao wa Kijamii wa Snapchat ambao umekuwa maarufu kwa sasa.

Mpaka sasa, mtandao huo umempa jamaa utajiri dola bilioni 2.1 (zaidi ya trilioni 5.2) na kumfanya kuwa kijana mdogo mwenye pesa nyingi.

bobby-murphyBoby Murphy

Huyu Jamaa ni Mmarekani mwenye asili ya Ufilipino mwenye umri wa miaka 27. Alisoma katika Shule ya Madeleine iliyokuwa Calfornia nchini Marekani. Baada ya kuona anajua sana hesabu, akaomba kujiunga na Chuo cha Stanford ambapo huko ndipo alipokutana na mshikaji wake, Spiegel na kuamua kutengeneza Mtandao wa Kijamii wa Snapchat ambao ulimuingizia fedha nyingi tu.

Leo unapomzungumzia Murphy, ni miongoni mwa mabilionea wadogo ambapo anamiliki mkwanja wa dola bilioni 1.8 ambazo ni zaidi ya shilingi trilioni 3.5.

mark-zuckerbergMark Zuckerberg

Wengi wanamjua, na kama humjui basi bila shaka utakuwa ukitumia mitandao yake ya Facebook, Instagram au WhatsApp. Mshikaji ana miaka 31, alizaliwa huko White Plans, New York nchini Marekani. Alipokua, jamaa alisomea katika Shule ya Ardsley, baadaye akaenda katika Akademi ya Phillip Exteter na kumalizia katika Chuo Kikuu cha Harvard hukohuko Marekani.

Alipofika hapo, akaamua kuanzisha Mtandao wa Kijamii wa Facebook kwa kuamini kwamba ungempa pesa ndefu. Alifanikiwa, mtandao ukapata watumiaji wengi, akanogewa, akanunua mitandao mingine ya WhatsApp na Instagram ambayo mpaka leo inamuingizia fedha na kumfanya bilionea wa tano duniani huku akiwa na utajiri wa dola bilioni 50 ambazo ni zaidi ya shilingi trilioni 100.

dustin-moskovitzDustin Moskovitz

Wakati Mark Zuckerberg alipopata wazo la kuanzisha Mtandao wa Facebook, ndani ya chumba alikuwa na watu wengine watatu. Mmoja wa watu hao ni huyu jamaa ambaye alizaliwa Gainesvile, Florida hukohuko nchini Marekani japokuwa baba yake ni Muisrael.

Mwaka 2008 jamaa akaamua kujitoa katika Kampuni ya Facebook na hivyo kuanzisha programu yake ya Asana akiwa pamoja na rafiki yake ambaye naye alikuwa akifanya kazi Facebook, Justin Rusenstein. Hapo, jamaa akaanza kupata mafanikio mpaka kuwa na utajiri wa dola bilioni 20 ambazo ni zaidi ya shilingi trilioni 40. Kwa sasa jamaa ana miaka 31.

elizabethElizabeth Holmes

Ni mwanadada mrembo, anayewavutia wanaume wengi. Ni mdogo, ana miaka 31. Katika maisha yake, Holmes alisoma masuala ya utabibu katika Chuo cha Stanford kilichokuwa nchini Marekani. Mwaka 2003 alipokuwa na miaka 19, akagundua kifaa kinachoitwa Fingestick (kifaa maalumu kidogo kinachotumika kuangalia wingi wa damu na magonjwa mbalimbali ya damu) ambacho kiliweza kumpatia kiasi cha dola milioni 400 (zaidi ya bilioni 800) kwa mwaka wa kwanza tu.

Amekuwa akiishi katika ulimwengu wa mabilionea, aliendelea kuingiza fedha kila siku, akaunti yake kusoma dola milioni 30 zimeingia ni kitu cha kawaida sana. Mpaka sasa, mrembo huyu ana utajiri wa dola bilioni 4.8 ambazo ni zaidi ya shilingi trilioni 9.5.

Comments are closed.